Makataba wa hudaibiya: sababu zake, vipengele vyake, na faida za mkataba wa hudaibiya

Mkataba wa Hudaibiya

- Ni mkataba wa amani baina ya waislamu na Maquraish wa Makkah, mwaka wa 6 A.H, Dhul-Qa’adah (Machi, 628 A.D) katika kitongoji cha Hudaybiyah karibu na
Mji wa Makkah.

- Mkataba ulitiwa saini na Mtume (s.a.w) kwa niaba ya waislamu na Suhail bin Amri
Kwa niaba ya Makafiri wa Kiquraish.



Yaliyopelekea kutokea kwa Mkataba wa Hudaybiyah.
- ilikuwa Mtume (s.a.w) kutimiza ndoto (wahay) aliyoota mwaka 6 A.H. kuwa kuna siku atafanya ‘Umrah’.

- Mtume (s.a.w) akiwa na waislamu 1,400 walikwenda kufanya ibada ya ‘Umrah’ lakini walizuiliwa na Maquraish katika kitongoji cha Hudaibiyah wasiingie Makkah.

- Mtume (s.a.w) alituma wajumbe 2, mmoja baada ya mwingine ili kuwaomba Maquraish wawaruhusu waingie Makkah, lakini walikataliwa.

- Mtume (s.a.w) alituma mjumbe wa 3, ‘Uthman bin Affan’ (r.a) aliyeshikiliwa na Maquraish kwa muda, na kuja tetesi kuwa ameuawa.

- Mtume (s.a.w) aliwakusanya waumini chini ya mti na kuchukua kiapo cha utii (Bai’at) juu ya kulipiza kisasi cha ‘Uthman bin Affan’ (r.a), lakini baadaye alirejea.
Rejea Qur’an (48:18).



- Maquraish kwa kuwaogopa waislamu, walimuomba Mtume (s.a.w) kuweka mkataba wa amani na Mtume (s.a.w) alikubali, na ukaitwa “Mkataba wa Hudaybiyah”.
Rejea Qur’an (48:1).



Vipengele vya Mkataba wa Hudaybiyah.
1.Waislamu warudi Madinah bila kufanya ‘Umrah’.
2.Waislamu wanaweza kurudi mwakani (7 A.H) kufanya ‘Umrah’ lakini wakae siku tatu.
3.Wakija Makkah wasije na silaha ila panga zikiwa ndani yah ala zao.
4.Waislamu hawataenda nao Madinah waislamu wanaoishi Makkah na wala hawatamzuia yeyote miongoni mwao anayetaka kubakia Makkah.
5.Kama yeyote wa Makkah atatoroka kwenda kusilimu, Waislamu hawana budi kumrudisha (wasimpokee), lakini yeyote kutoka Madinah akitoroka kwenda Makkah kuritadi, Maquraish hawatapaswa kumrudisha Madinah (watampokea).
6.Makabila ya Waarabu yatakuwa huru kufanya Itifaki (urafiki) na upande wowote ule yanaoupendelea.
7.Pasiwe na vita kwa kipindi cha miaka 10 baina ya waislamu na Maquraish na baina ya waitifaki (Allies) wa Waislamu na waitifaki wa Maquraish.
8.Hapana ruhusa ya kutengua hata sharti moja katika hizi kabla ya miaka 10 kupita.



Mafunzo yatokanayo na Mkataba wa Hudaybiyah.
1.Ahadi ya Mwenyezi Mungu (s.w) siku zote ni ya kweli na yenye kutimia, kama alivyotimiza ahadi kwa Mtume (s.a.w) alipoota kuwa siku 1 atakwenda ‘Umra’.
Rejea Qur’an (48:27).

2.Katika kusimamisha Uislamu, ni lazima pawepo na mbinu na mipango maalumu ya muda mfupi na muda mrefu ili kufikia malengo yetu katika nyanja yeyote ile.
Kama alivyofanya Mtume (s.a.w) katika mkataba wa Hudaibiyah:
- Kufuta ‘Bismillahir Rahmaanir Rahiim’,
- Kufuta ‘Muhammad Rasulullaah’.
- kukubali kipengele cha 4 na 5 ijapokuwa vilikuwa vinawadhalilisha waislamu.
Rejea Qur’an (48:18), (48:29) na (48:22).

3.Waumini walipata maliwazo ya Mwenyezi Mungu (s.w) baada ya kukata tamaa kutokana na uonevu wa baadhi ya vipengele vya Mkataba wa Hudaibiyah.
Rejea Qur’an (48:20-29) na (48:1-8).

4.Tunajifunza pia, ni wajibu kutekeleza mikataba tuliyoandikiana hata ikiwa na Makafiri, kama alivyotekeleza Mtume (s.a.w) mkataba wa Hudaybiyah.
Rejea Qur’an (48:10) na (60:10-12).

5.Ni wajibu kufikisha ujumbe wa Qur’an kwa wasio waislamu na viongozi wao, kama alivyofanya Mtume (s.a.w) kwa kutuma mabalozi sehemu mbali mbali.

6.Mazingira ya amani na utulivu ni jambo la muhimu sana katika kueneza na kuendeleza ujumbe wa Uislamu, hivyo mapatano ni bora zaidi kuliko kupigana.

7.Waislamu tuwe wepesi katika kutumia fursa zinazopatikana na kupelekea kufikia malengo yetu ya kuusimamisha Uislamu katika jamii.

8.Tuwe tayari kupoteza maslahi madogo madogo katika kutafuta fursa, mazingira na suluhu inayopelekea kufikia lengo kuu.

9.Tuwe na uvumilivu na subira kwa kutotegemea matunda ya kusimamisha Uislamu kupatikana haraka na bila ya misukosuko.

10.Nusura na ushindi kwa waislamu hupatikana baada ya waislamu kufanya juhudi ya dhati mwisho wa uwezo wao.
Rejea Qur’an (48:1).



Matunda (ushindi) yatokanayo na Mkataba wa Hudaybiyah.
1.Waislamu walipata fursa ya kulingania Uislamu na watu wengi walisilimu wakiwemo majemedari kama, Khalid bin Walid, Suhail bin Amr na Amr bin Al-As na wengineo.
Rejea Qur’an (48:1).

2.Kuhamia jangwani kikosi kilichosilimu na kuwa tishio kwa misafara ya Maquraish, Maquraish walimuomba Mtume (s.a.w) kuondoa kipengele kilichowakataza wanaosilimu Makka kwenda Madinah kilichokuwa kero kwa waislamu.

3.Mtume na waislamu walipata fursa ya kuutangaza Uislamu ndani na nje ya Bara Arabu kama vile, Mashariki ya kati, Misr, Uhabeshi na Wafalme mbali mbali.
Rejea Qur’an (3:64).

4.Waislamu walipata fursa ya kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya biashara hasa za masafa ya mbali kwa amani na falme za nje ya Bara Arab.


5.Waislamu waliweza kujizatiti kijeshi na kuweza kuwadhibiti maadui wa Uislamu na waislamu katika mapigano mbali mbali kama;
- Wayahudi (Warumi) katika vita vya Khaibar na Muttah mwaka wa 7 A.H.
- Ushujaa wa waislamu yalisababisha maadui kuwakimbia msafara wa Tabuuk.
6.Mtume (s.a.w) akiwa na waislamu 2,000 walifanikiwa kufanya Umrah mwaka wa 7 A.H (badala ya wale 1,400 waliorudishwa 6 A.H.) na kutimiza ndoto yake ya ushindi.
Rejea Qur’an (48:27).

7.Fat-h Makkah – kilele cha ushindi, baada ya Maquraish na Waitifaki wao kuvunja mkataba wa Hudaybiyah baada ya muda wa miaka 2 tu, na Mtume alitumia fursa hii kuikomboa Makkah bila vita.