Kusilimu kwa Wachawi wa Firaun


Mawaziri waliokuwa washauri wakuu wa Firauni wakataka wakusanywe magwiji waliobobea katika uchawi nchi nzima, kisha wapambanishwe na Nabii Musa(as).Basi walipofika wachawi, wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira tukiwa sisi ndio tutakaoshinda. Akasema: Naam, na pia mtakuwa miongoni mwa wale wanaowekwa mbele katika (Serikali) (26:41-42)Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni sisi tutakuwa ndio wenye kushinda (26:44)Kisha Musa akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza(vyote) walivyozusha wachawi (26:45)

Wachawi walipoona vitu vyao vya kichawi(viini macho) walivyovitupa uwanjani vimemezwa vyote na nyoka(wa muujiza), walisalimu amri na kutoa shahada:Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola wa walimwengu wote. Mola wa Musa na Harun (26:46-48)Firaun aliwatishia wachawi kuwapa adhabu kubwa kwa kusilimu kwao pasina idhini yake (Qur’an 26:49). Inabainika hapa kuwa uchawi si sawa na muujiza,na ndio maana wachawi walishindwa. Hakika uliwadhihirikia ukweli kwamba Musa(a.s) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ndio maana Firauni alipotangaza kuwa atawasulubu kwa kuwakata miguu na mikono yao kwa sababu wamesilimu pasina ridhaa yake; hawakuyumba katika imani yao.Wakasema: Haidhuru, hakika sisi sote tutarejea kwa Mola wetu. Kwa yakini sisi tunatumai ya kwamba Mola wetu atatusamehe makosa yetu, maana sisi tumekuwa wa kwanza wa wenye kusilimu hapa (26:50-51)