KUCHIMBWA UPYA KISIMA CHA ZAMZAM
Kwa kifupi ni kuwa Abdul-Muttalib alipata agizo kutoka ndotoni kuwa achimbe kisima cha zamzam, na akaelekezwa sehemu ya kupachimba. Basi akachimba na ndipo akakuta chini ya kisima vitu ambavyo vilifukiwa pamoja na kisima. Walofukia vitu hivi ni watu kutoka kabila la Jurhum. Hawa pindi walipolazimika kuondoka Maka walikifukia kisima cha zamzam na kufukia baadhi ya vitu vya thamani kama mapanga, nguo za vita, na dhahabu. Baada ya hapo mlango wa alka’aba ukatengenezwa kwa hii dhahabu waloipata. Na unyweshwaji wa maji ya zamzam kwa mahujaji ukarudi upya.
Basi kisima cha zamzam kilipoanza kutoa maji, watu kutoka kabila la quraysh walitaka kufanya makubaliano juu ya maji yale lakini Abdul Al-Muttalib alikataa kwa kudai kuwa Allah amempa mamlaka yeye tu. Basi wakakubaliana wakamuulize kuhani kutoka ukoo wa Bani Sa’ad juu ya swala hili. Basi Allah akawaonesha alama za ukweli juu ya madai ya Abdul Al-Muttalib. Baada ya hapo mzee Abdul Al-Muttalib kwa shukran yake kwa Allah akaapa kumtoa kafara mtoto wake kwa Mwenyezi Mungu.