Tanzu za Hadith
(1) Tanzu ya Usahihi
Kulingana na kiwango cha usahihi wa Hadith, Hadith zimegawanywa katika makundi makuu manne:
(a) Sahihi 
(b) Hasan/Nzuri. 
(c) Dhaifu. 
(d) maudhu’u 

(a)Sahihi
Hadith sahihi ni zile Hadith zenye wasimulizi wote wenye sifa zilizokamilika kutokea mpokezi wa mwisho mpaka kufikia kwa Mtume (s.a.w). Kwa ufupi mambo yafuatayo ni muhimu yapatikane yote kwa pamoja ndio Hadith iitwe sahihi.

1. Pawepo Muungano wa Wapokezi wa Hadith. Kila mpokezi awe amepokea moja kwa moja kutoka kwa yule aliyeko juu yake kutoka mwanzo wa Isnadi mpaka mwisho wake.

2. Uadilifu wa Mpokezi. Kila mpokezi wa Hadith awe ni Muislamu, balegh, mwenye akili na asiwe fasiki na mwenye kufanya mambo ya ovyo ovyo.

3. Udhibitifu wa Mpokezi. Ni kuwa kila mpokezi awe amekamilika katika udhibitifu wake, ama awe mdhibitifu wa kifua (kuhifadhi) au awe mdhibitifu wa kuandika.

4. Kutokwenda kinyume na aliyekuwa mdhibitifu zaidi. Asimukhalifu ambaye anajulikana kuwa mdhibitifu zaidi kuliko yeye.

5. Kutokuwa na Ila. Isiwe Hadith yenye ila wala sababu iliyojificha ambayo inasababisha kutokusihi kwa Hadith ijapokuwa nje yake haina wasi wasi.

Mfano wa Hadith Sahihi
Hadith aliyoipokea Bukhari katika kitabu chake kasema: Ametuadithia 'Abdallah bin Yusuf akasema: Ametupa habari Malik kutoka kwa Ibn Shihab kutoka kwa Muhammad bin Ubair bin Mut-'im kutoka kwa baba yake kwamba: "Nimemsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu anasoma Wat-tur katika swala ya Maghrib." Hadith hii ni sahihi kwa sababu: Wapokezi wake wameshikamana na wapokezi wake ni wadhibitifu.
1. 'Abdullah bin Yusuf ni mdhibitifu.
2. Malik bin Anas ni Imamu Hafiidh.
3. Ibn Shihab ni Faqihi Hafidh.
4. Muhammad bin Jubair ni mdhibitifu.
5. Jubair bin Mut-im-Sahaba.

Hadith Sahihi ziko katika daraja saba:

(i) Hadith iliyokubaliwa kwa pamoja na Imamu Bukhari na Muslim, huwekwa katika daraja la juu kabisa ya usahihi - na Hadith hii huelekezwa kwa: "Makubaliano (ya Bukhari na Muslim)."
(i) Hadith iliyopokelewa na Bukhari mwenyewe huchukua nafasi ya pili ya Usahihi.
(iii)Hadith iliyosimuliwa na Muslimu mwenyewe huchukua daraja la Tatu ya Usahihi.
(iv)Hadith iliyokubaliwa kwa kufuata masharti ya kuchambua Hadith aliyoweka Muslim na Bukhari, huwa katika daraja la nne ya Hadith Sahihi.
(v)Hadith yenye kufuata masharti aliyoweka Bukhari mwenyewe huchukua nafasi ya tano ya Usahihi.
(vi)Hadith iliyochambuliwa kwa masharti aliyoyaweka Muslim mwenyewe huchukua nafasi ya sita ya Usahihi.
(vii)Hadith iliyokubaliwa na Muhaddithina wote isipokuwa Bukhari na Muslim huchukua nafasi ya saba ya Usahihi.

(b)Hasan/Nzuri
Ni Hadith iliyofanana na Hadith sahihi bali kasoro yake ni kwamba wasimulizi wake wote au baadhi yao wamekuwa dhaifu katika udhibitifu wao ukiwalinganisha na wale wasimulizi wa Hadith sahihi. 

(c)Dhaifu
Ni Hadith ambayo miongoni mwa wasimulizi wake wana kasoro zilizojitokeza. Hadith za namna hii si zenye kuaminika na kwa hiyo si za kutegemea.

(d)Maudhu’u
Hii ni Hadith ya uongo ambapo Mtume (s.a.w) amezuliwa na wakapachikwa wapokezi wa kughushi. Ni Hadith ambayo hupingana na Qur,an na Hadith nyingine iliyo sahihi.

(2.) Tanzu ya umashuhuri(umaarufu)
Pia Hadith zimegawanywa katika sehemu mbili zifuatazo ili kuonyesha uzito wa kukubalika au kutokubalika kwake.

(a) Mutawatir
- ni Hadith yenye kusimuliwa na watu wengi, wanne au zaidi wote wakiwa wanasifa zilizokamilika na wakawa wameisimulia kwa nyakati mbali mbali kwa kiasi ambacho huifanya Hadith hiyo iwe ni muhali kuwa na tone la doa la uwongo ndani yake. Pia Hadith Mutawatir ni zile zinazokubalika na watu wote wa nyakati zote tangu wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w). Kwa mfano Hadith ifuatayo imesimuliwa na Masahaba wengi na imekubaliwa na watu wote. Mtume (s.a.w) amesema: "Mwenye kunizulia uwongo makusudi, atarajie (angojee) makazi ya Motoni." Hadith hii ni Mutawatir - yaani ni yenye kukubalika pasina tone la shaka.

(b)Ahad
ni Hadith ambayo japo wasimulizi wake ni wenye sifa zilizokamilika, hawana mfungamano yaani msururu wa wasimulizi una mapengo mapengo katikati (Isnad haikukamilika). Pia Hadith Ahad ni ile isiyokubaliwa na watu wengi. Hadith za namna hii ni za mashaka mashaka na si zenye kuaminika na si vizuri kuzitegemea.