Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
1

2. Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili
mpate kuzingatia. 2

3. Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia
Qur'ani hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio jua. 3

4. Yusuf alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika
mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeota zikinisujudia. 4

5. (Baba) akasema: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo
ndoto yako, wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri
kwa mwanaadamu. 5

6. Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na
atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo
wa Yaa'qub, kama alivyo watimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq.
Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye hikima. 6

7. Kwa yakini katika Yusuf na nduguze ziko ishara kwa
wanao uliza. 7

8. Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa
zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba
yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri. 8

9. 9

10. Akasema msemaji kati yao: Msimuuwe Yusuf. Lakini
mtumbukizeni ndani ya kisima. Wasafiri watakuja mwokota; kama nyinyi mna sharti
ya kufanya jambo. 10

11. Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa
Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia kheri! 11

12. Mpeleke kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze;
na bila ya shaka sisi tutamhifadhi. 12

13. Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi
mwende naye, na ninaogopa asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye. 13

14. Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni
kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa khasarani. 14

15. Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize
ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa
jambo lao hili, na wala wao hawatambui. 15

16. Wakaja kwa baba yao usiku wakilia. 16

17. Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda
kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini
wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema kweli. 17

18. Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema:
Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na
Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza. 18

19. Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye
akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha
ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda. 19

20. . Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa.
Wala hawakuwa na haja naye. 20

21. Na yule aliye mnunua huko Misri alimwambia mkewe:
Mtengenezee makaazi ya hishima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na
kama hivyo tulimweka Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi
hawajui. 21

22. Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu.
Na kama hivi tunawalipa wanao tenda mema. 22

23. Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani
kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema:
Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani
nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi. 23

24. Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli
mtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili
tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio
safishwa. 24

25. Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke
akairarua kanzu yake Yusuf kwa nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke
akasema: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa
au kupewa adhabu chungu. 25

26. Yusuf akasema: Yeye ndiye aliye nitaka bila ya mimi
kumtaka. Na shahidi aliye kuwa katika jamaa za mwanamke alisema: Ikiwa kanzu
yake imechanwa mbele basi mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo. 26

27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi mwanamke
amesema uwongo, naye Yusuf ni katika wakweli. 27

28. Basi yule bwana alipoona kanzu yake imechanwa kwa
nyuma, alisema: Hakika haya ni katika vitimbi vyenu wanawake. Bila ya shaka
vitimbi vyenu ni vikuu. 28

29. Yusuf! Wachilia mbali haya. Na wewe, mwanamke, omba
msamaha kwa dhambi zako. Kwa hakika wewe ni katika walio fanya makosa. 29

30. Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa
Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake ! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi
hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhaahiri. 30

31. Alipo sikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na
akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf:
Tokeza mbele yao. Basi walipo mwona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na
wakajikata mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu
ila ni Malaika mtukufu. 31

32. Yule bibi akasema: Huyu basi ndiye huyo mliye
nilaumia! Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa. Na akitofanya ninayo muamrisha
basi hapana shaka atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini
kabisa. 32

33. Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu
kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi
nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga. 33

34. Basi Mola wake Mlezi akamwitikia, na akamwondoshea
vitimbi vyao. Hakika Yeye ni Msikizi Mjuzi. 34

35. Basi ikawadhihirikia baada ya kuona Ishara kuwa
wamfunge kwa muda.35

36. Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja
wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi
nimeota nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie
tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. 36

37. Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakacho pewa ila
nitakwambieni hakika yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale aliyo
nifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasio muamini
Mwenyezi Mungu, na wakawa hawaiamini Akhera. 37

38. Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq,
na Yaa'qub. Hatuna haki ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni
katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu; lakini watu wengi
hawashukuru. 38

39. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi
wanao farikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu? 39

40. Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga
nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote.
Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo
kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui. 40

41. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu
atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine atasulubiwa, na ndege watamla
kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilo kuwa mkiuliza. 41

42. Na akamwambia yule aliye jua kuwa atavuka katika
wale wawili: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shet'ani alimsahaulisha kumtaja
kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa. 42

43. Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota
ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba
mabichi na mengine makavu. Enyi waheshimiwa! Nambieni maana ya ndoto zangu,
ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto. 43

44. Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo paraganyika, wala
sisi sio wenye kujua tafsiri ya ndoto hizi. 44

45. Hapo akasema yule aliye okoka katika wale wawili
akakumbuka baada ya muda: Mimi nitakwambieni tafsiri yake. Basi nitumeni. 45

46. Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe
saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na
mengine makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua. 46

47. Akasema: Mtalima miaka saba kwa juhudi. Mtacho vuna
kiwacheni katika mashuke yake, isipo kuwa kidogo mtacho kula. 47

48. Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayo
kula kile mlicho iwekea isipo kuwa kidogo mtacho kihifadhi. 48

49. Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka
huo watu watasaidiwa, na watakamua. 49

50. Na mfalme akasema: Mleteni kwangu! Basi mjumbe alipo
mjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako ukamuulize khabari ya wale wanawake
walio jikata mikono yao. Hakika Mola wangu Mlezi anazijua vyema hila zao. 50

51. Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf
kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote
kwake. Mke wa Mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka
kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli. 51

52. Hayo ni apate kujua ya kwamba mimi sikumfanyia
khiyana nyuma yake; na ya kwamba Mwenyezi Mungu haziongoi hila za makhaini. 52

53. NAmi sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno
kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika
Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu. 53

54. Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu
mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani
kwetu na umeaminika. 54

55. Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani
hakika mimi ni mlinzi mjuzi. 55

56. Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi;
anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala
hatupuuzi malipo ya wafanyao mema. 56

57. Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio
amini na wakawa wachamungu. 57

58. Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye
akawajua na wao hawakumjua. 58

59. Na alipo watengenezea tayari haja yao alisema:
Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je! Hamwoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo,
nami ni mbora wa kukirimu? 59

60. Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote
kwangu, wala msinikurubie. 60

61. Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya
shaka tutafanya hayo. 61

62. Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao
katika mizigo yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena. 62

63. Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba
yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate
kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda. 63

64. Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini
kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye
Mbora wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote. 64

65. Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao
wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu
tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na
tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo. 65

66. Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa
Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi
walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo. 66

67. Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja,
bali ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi
Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea,
na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea. 67

68. Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao,
haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika
nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu
tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui. 68

69. Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye
akasema: Mimi hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya. 69

70. Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia
kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi
wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi! 70

71. Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini? 71

72. Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta
atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo. 72

73. Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja
kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi. 73

74. Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa
nyinyi ni waongo. 74

75. Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo
yeye huyo ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu. 75

76. Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa
nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia
Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka
Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo
ajuaye zaidi. 76

77. Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile
aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha.
Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi
hayo mnayo singizia. 77

78. Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana.
Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika
watu wema. 78

79. Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote
yule isipo kuwa tuliye mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye
kudhulumu. 79

80. Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona.
Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu
kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya
Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi
Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu. 80

81. Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu!
Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa
wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu. 81

82. Na waulize watu wa mji tulio kuwako, na msafara
tulio kuja nao. Na hakika sisi tunasema kweli. 82

83. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye
jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja.
Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima. 83

84. Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf!
Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia. 84

85. Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe
mgonjwa au uwe katika walio hiliki. 85

86. Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu
sikitiko langu na huzuni yangu. Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua
nyinyi. 86

87. Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye,
wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji
ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa watu makafiri. 87

88. Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe
Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi
tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa
watoao sadaka. 88

89. Akasema: Je! Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye
mlipo kuwa wajinga? 89

90. Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi
ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika
anaye mcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa
wafanyao mema. 90

91 Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha
wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa. 91

92. Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu
atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu. 92

93. Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba
yangu, atakuwa mwenye kuona. Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani. 93

94. Na ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika
mimi nasikia harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu 94

95. Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu
wako wa zamani. 95

96. Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni
pake alirejea kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi
Mungu msiyo yajua nyinyi? 96

97. Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni
pake alirejea kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi
Mungu msiyo yajua nyinyi. 97

98. Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu
Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe. 98

99. Na walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake
na akasema: Ingieni Misri, Inshallah, mmo katika amani.

100. Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi.
Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri
ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na
Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani
baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi
ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima. 100

101. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na
umenifunza tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi
wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe
na watendao mema. 101

102. Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia.
Na hukuwa pamoja nao walipo azimia shauri yao, walipo fanya njama zao wakizua
vitimbi. 102

103. Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi.
103

104. Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya
ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. 104

105. Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazo
zipitia, na hali ya kuwa wanazipuuza. 105

106. Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu
pasina kuwa ni washirikina. 106

107. Je! Wanaaminisha kuwa haitowajia adhabu ya Mwenyezi
Mungu ya kuwagubika, au haitawafikia Saa ya Kiyama kwa ghafla, na hali
hawatambui? 107

108. Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa
Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu!
Wala mimi si katika washirikina. 108

109. Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa
wanaume tulio wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika
ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba
ya Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu? 109

110. Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa
wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu
yetu haitowawacha kaumu ya wakosefu. 110

111. Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa
wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake,
na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini. 111
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani