Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Alif Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitabu chenye Hikima. 1

2. Je! Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mmoja
wao kuwa: Waonye watu, na wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa na cheo
cha juu kwa Mola wao Mlezi? Wakasema makafiri: Hakika huyu ni mchawi
dhaahiri! 2

3. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye
ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, na ametawala kwenye ufalme wake,
anaendesha mambo yote. Hapana mwombezi ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye
Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki? 3

4. Kwake Yeye tu ndio marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi
ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika Yeye ndiye aliye anzisha uumbaji, na
kisha ataurejesha ili awalipe kwa uadilifu wale walio amini na wakatenda mema.
Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa
sababu ya walivyo kuwa wakikufuru. 4

5. Yeye ndiye aliye lijaalia jua kuwa na mwangaza, na
mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu.
Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa Haki. Anazipambanua Ishara kwa watu
wanao jua. 5

6. Hakika katika kukhitalifiana usiku na mchana, na
katika alivyo umba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, zipo Ishara kwa watu
wanao mcha-Mngu. 6

7. Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia
maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu, 7

8. Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo kuwa
wakiyachuma. 8

9. Hakika walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi
atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itakuwa inapita mito kati yao katika
Mabustani yenye neema. 9

10. Wito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma
"Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!" Na maamkio yao humo ni "Salama". Na mwisho wa
wito wao ni: Alhamdulillahi Rabbil A'lamiin "Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote." 10

11. Na lau kama Mwenyezi Mungu angeli wafanyia watu
haraka kuwaletea shari kama wanavyo jihimizia kuletewa kheri, bila ya shaka
wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasio tumainia kukutana
nasi wakihangaika katika upotovu wao. 11

12. Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha
ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama
kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna hiyo
wamepambiwa warukao mipaka yale waliyo kuwa wakiyatenda. 12

13. Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza kaumu za kabla
yenu walipo dhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi; lakini
hawakuwa wenye kuamini. Ndio kama hivyo tunavyo walipa watu wakosefu. 13

14. Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika mahala
pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyo tenda. 14

15. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasio
taraji kukutana na Sisi husema: Lete Qur'ani isiyo kuwa hii, au ibadilishe.
Sema: Hainifalii mimi kuibadilisha kwa nitakavyo nafsi yangu. Mimi sifuati ila
ninayo funuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa, nikimuasi Mola wangu Mlezi,
adhabu ya Siku iliyo kuu.15

16. Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli
kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima kabla
yake! Basi, je! Hamzingatii? 16

17. Basi ni nani aliye dhaalimu zaidi kuliko yule anaye
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha Ishara zake? Hakika hawafanikiwi
wakosefu. 17

18. Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasio
wadhuru wala kuwanufaisha,na wanasema: Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi
Mungu! Sema: Je! Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyo yajua ya katika mbingu wala
katika ardhi? Subhanahu wa Taa'la! Ametakasika na ametukuka na hao wanao
mshirikisha naye. 18

19. Wala watu hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha
wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutokana na Mola
wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingeli kwisha katwa baina yao katika hayo wanayo
khitalifiana. 19

20. Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka
kwa Mola wake Mlezi? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu. Basi nyinyi
ngojeni, na mimi ni pamoja nanyi katika wanao ngojea. 20

21. Na tunapo waonjesha watu rehema baada ya shida
waliyo ipata, utawaona wana vitimbi kuzipangia Ishara zetu. Sema: Mwenyezi Mungu
ni Mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayo yapanga. 21

22. Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini. Hata
mnapo kuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia,
upepo mkali ukawazukia, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona
wameshazongwa, basi hapo humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa
na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru. 22

23. Lakini akisha waokoa, mara wanafanya jeuri tena
katika nchi bila ya haki. Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Hii ni
starehe ya maisha ya dunia tu. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo
tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda. 23

24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyo
yateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayo ila
watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika, na
wenyewe wakadhani wamesha iweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifanya
kama iliyo fyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara
zetu kwa watu wanao fikiri. 24

25. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya Amani, na
anamwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka. 25

26. Kwa wafanyao wema ni wema na zaidi. Wala vumbi
halitawafunika nyuso zao, wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi. Humo watadumu. 26

27. Na wale walio chuma maovu, malipo ya uovu ni mfano
wake vile vile, na yatawafika madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi
Mungu. Nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio
watu wa Motoni, wao humo watadumu. 27

28. Na siku tutakapo wakusanya wote, kisha tutawaambia
walio shirikisha:Simameni mahali penu nyinyi na wale mlio wafanya washirika.
Kisha tutawatenga baina yao. Na hao walio washirikisha watasema: Nyinyi hamkuwa
mkituabudu sisi. 28

29. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yetu
na nyinyi. Hakika sisi tulikuwa hatuna khabari ya ibada yenu. 29

30. Huko kila mtu atayajua aliyo yatanguliza. Na
watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki, na yote waliyo kuwa wakiyazua
yatawapotea. 30

31. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na
kwenye ardhi? Au ni nani anaye miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye hai
kutoka maiti, na akamtoa maiti kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri mambo
yote? Watasema:Allah, Mwenyezi Mungu. Basi sema: Je! Hamchi? 31

32. Basi huyo
ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki,
isipokuwa upotovu tu? Basi huwaje mkageuzwa?
href="c10.html#32">32

33. Ndio kama hivyo kauli ya Mola wako Mlezi itakavyo
wathibitikia wale walio potoka, ya kwamba hawatoamini. 33

34. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina
aliye anzisha kuumba viumbe, na kisha akavirejesha? Huwaje, basi, mkadanganywa? 34

35. Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina
anaye ongoa kwendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je,
anaye stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila
aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani? 35

36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai
kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayo yatenda. 36

37. Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa na haitoki
kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii inasadikisha yaliyo tangulia, na ni mfafanuo wa
Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote. 37

38. Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura
moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu,
ikiwa nyinyi mnasema kweli.38

39. Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla
hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile. Basi
angalia jinsi ulivyo kuwa mwisho wa madhaalimu hao. 39

40. Na miongoni mwao wapo wanao iamini, na miongoni mwao
wapo wasio iamini. Na Mola wako Mlezi anawajua vyema mafisadi. 40

41. Na wakikukanusha wewe, sema: Mimi nina a'mali yangu,
na nyinyi mna a'mali yenu. Nyinyi hamna jukumu kwa niyatendayo, wala mimi sina
jukumu kwa myatendayo. 41

42. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza. Je, wewe
unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapo kuwa hawafahamu?42

43. Na wapo miongoni mwao wanao kutazama. Je, wewe
utawaongoa vipofu ingawa hawaoni? 43

44. Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu
chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao. 44

45. Na Siku atakapo wakusanya, itakuwa kama kwamba
hawakukaa ila saa moja tu ya mchana! Watatambuana. Hakika wamekhasirika walio
kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka. 45

46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayo
waahidi, au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu
ni Shahidi wa wanayo yafanya. 46

47. Na kila umma una Mtume. Alipo wajia Mtume wao
walihukumiwa baina yao kwa uadilifu, wala hawakudhulumiwa. 47

48. . Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli? 48

49. Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri ila
apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao walio wekewa. Ukifika muda wao
hawakawii hata saa moja wala hawatangulii. 49

50. Sema: Mwaonaje ikikufikieni hiyo adhabu yake usiku
au mchana, sehemu gani ya adhabu wanaihimiza wakosefu? 50

51. Tena je! Ikisha tokea mtaiamini? Je! Ndio sasa tena?
Na nyinyi mlikuwa mkiihimiza.51

52. Kisha walio dhulumu wataambiwa: Onjeni adhabu ya
kudumu. Kwani mtalipwa isipo kuwa yale mliyo kuwa mkiyachuma?<52

53. Na wanakuuliza: Je! Ni kweli hayo? Sema: Ehe! Naapa
kwa Mola wangu Mlezi! Hakika hayo ni kweli, na wala nyinyi hamshindi! 53

54. Na lau kuwa kila nafsi iliyo dhulumu inamiliki kila
kiliomo duniani,bila ya shaka ingeli toa vyote kujikombolea. Na watakapo iona
adhabu wataficha majuto. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao
hawatadhulumiwa. 54

55. Jueni kuwa hakika vyote viliomo katika mbingu na
katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni
ya haki. Lakini wengi wao hawajui. 55

56. Yeye ndiye anaye fufua na anaye fisha. Na kwake
mtarejeshwa 56

57. Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu
Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.57

58. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake!
Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya. 58

59. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake!
Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.59

60. Na nini dhana ya wanao mzulia Mwenyezi Mungu kwa
Siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini wengi wao
hawashukuru.60

61. Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu
yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi
juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye
uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho
wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.61

62. Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na
khofu wala hawatahuzunika.62

63. Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu.63

64. Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na
katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko
kufuzu kukubwa.64

65. Wala yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu wote
ni wa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.65

66. Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo
mbinguni na ardhinii.Na wala hawawafuati hao wanao waomba badala ya Mwenyezi
Mungu kuwa ni washirika wake. Wao hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila
uwongo.66

67. Yeye ndiye aliye kujaalieni usiku mpate kutulia
humo, na mchana wa kuonea. Hakika katika haya zipo Ishara kwa watu wanao sikia.67

68. Wamesema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu, Aliye
takasika! Yeye ni Mkwasi, Mwenye Kujitosheleza. Vyote viliomo katika mbingu na
katika ardhi ni vyake peke yake. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya!
Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?68

69. Sema: Hao wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu
hawatafanikiwa.69

70. Hiyo ni starehe ya katika dunia tu, kisha marejeo
yao ni kwetu. Tena tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya kukufuru kwao.70

71. Wasomee khabari za Nuhu alipo waambia watu wake:
Enyi watu wangu!Ikiwa kukaa kwangu nanyi na kukumbusha kwangu kwa Ishara za
Mwenyezi Mungu kunakutieni mashaka basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Nanyi
tengezeni mambo yenu pamoja na washirika wenu, na wala mambo yenu yasifichikane
kwenu.Kisha nihukumuni, wala msinipe muhula.71

72. Lakini mkigeuka, basi mimi sikukuombeni ujira. Ujira
wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu.72

73.
Wakamkanusha. Basi tukamwokoa, pamoja na walio kuwa
naye, katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio walio bakia, na tukawazamisha walio
zikanusha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walio onywa.73

74. Kisha baada yake tukawatuma Mitume kwa watu wao. Nao
wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa wenye kuyaamini waliyo
yakanusha kabla yake. Ndio kama hivyo tunapiga muhuri juu ya nyoyo za warukao
mipaka.74

75. Kisha
baada yao tukamtuma Musa na Haruni kwa Firauni na waheshimiwa wake, kwa Ishara
zetu. Wakajivuna, na wakawa watu wakosefu.a
href="c10.html#75">75

76. Basi ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Hakika
huu ni uchawi dhaahiri.76

77. Akasema Musa: Mnasema hivi juu ya Haki ilipo
kujieni? Huu ni uchawi? Na wachawi hawafanikiwi!77

78. Wakasema: Je! Umetujia ili utuachishe tuliyo wakuta
nayo baba zetu, na mpate nyinyi wawili ukubwa katika nchi? Wala sisi
hatukuaminini nyinyi.78

79. Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi mjuzi!79

80. Basi walipo kuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni
mnavyo tupa!80

81. Walipo tupa, Musa alisema: Mliyo leta ni uchawi.
Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.81

82. Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake,
hata wanga chukia wakosefu82

83. Basi hawakumuamini Musa isipo kuwa baadhi ya vijana
vya kaumu yake, kwa kumwogopa Firauni na wakuu wao wasiwatese. Kwani hakika
Firauni alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa walio pita
kiasi.83

84. Na Musa alisema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi
mmemuamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu.84

85. Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe Mola wetu
Mlezi! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhaalimu.85

86. Na utuokoe kwa rehema yako na watu makafiri.86

87. Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi huu:
Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu ndio
mwahali mwa ibada, na mshike Sala, na wabashirie Waumini.87

88. Na Musa akasema: Mola wetu Mlezi! Hakika wewe umempa
Firauni na wakuu wake mapambo na mali katika maisha ya dunia. Hivyo wanapoteza
watu na Njia yako. Mola wetu Mlezi! Yafutilie mbali mali yao na zifunge nyoyo
zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu.88

89. Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa.
Basi simameni sawa sawa, wala msifuate njia za wale wasio jua.89

90.
Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Firauni na
askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipo kuwa anataka
kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye muamini Wana wa
Israili, na mimi ni miongoni mwa walio nyenyekea!90

91. Ala! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa
miongoni mwa mafisadi!91

92. Leo, basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara
kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara
zetu.92

93. Na hakika tuliwaweka Wana wa Is raili kikao chema,
na tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipo wafikia ilimu.
Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo
kuwa wakikhitalifiana.93

94. Na ikiwa unayo shaka katika tuliyo kuteremshia, basi
waulize wasomao Kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia Haki kutoka kwa
Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.94

95. Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanao zikanusha
Ishara za Mwenyezi Mungu, usije kuwa katika walio khasiri.95

96. Hakika wale ambao neno la Mola wako Mlezi limekwisha
thibitika juu yao, hawataamini,96

97. Ijapo kuwa itawajia kila Ishara, mpaka waione adhabu
iliyo chungu.97

98. Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na Imani yake
ikawafaa - isipo kuwa kaumu Yunus? Waliamini na Sisi tukawaondolea adhabu ya
hizaya katika maisha ya dunia, na tukawastarehesha kwa muda.98

99. Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote
waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?99

100. Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasio tumia akili zao. 100

101. Sema: Angalieni yaliomo mbinguni na kwenye ardhi!
Na Ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasio amini.101

102. Basi, je! Wanangojea jingine ila kama yaliyo tokea
siku za watu walio pita kabla yao? Ngojeni! Nami ni pamoja nanyi katika wanao
ngoja.102

103. Kisha Sisi huwaokoa Mitume wetu na walio amini.
Ndio kama hivyo,inatustahiki kuwaokoa Waumini.103

104. Sema: Enyi watu! Ikiwa nyinyi mnayo shaka katika
Dini yangu, basi mimi siwaabudu mnao waabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu.
Lakini mimi namuabudu Mwenyezi Mungu anaye kufisheni. Na nimeamrishwa niwe
miongoni mwa Waumini.104

105. Na uelekeze uso wako kwenye Dini ya Kweli, wala
usiwe katika washirikina.105

106. Na wala usiwaombe wasio kuwa Mwenyezi Mungu ambao
hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni mwa walio
dhulumu.106

107. Na Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana
wa kukuondolea ila Yeye. Na akikutakia kheri, basi hapana awezaye kurudisha
fadhila yake.Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.107

108. Sema: Enyi watu! Haki imekwisha kukujieni kutoka
kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye ongoka anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na
anaye potea anapotea kwa khasara ya nafsi yake. Na mimi si mwakilishi juu yenu.108

109. Na wewe fuata yanayo funuliwa kwako kwa wahyi. Na
vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na Yeye ndiye mbora wa mahakimu. 109
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani