Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. T'AHA! 1

2.
Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka.
2

3. Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea. 3

4. Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu
zilizo juu. 4

5. Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya
Kiti cha Enzi. 5

6. Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika
ardhi, na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi. 6

7. Na ukinyanyua sauti kwa kusema...basi hakika Yeye
anajua siri na duni kuliko siri. 7

8. Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye
ana majina mazuri kabisa. 8

9. Na je! Imekufikia hadithi ya Musa? 9

10. Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni!
Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata
uongofu kwenye moto. 10

11. Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa! 11

12. Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu
vyako. Kwani upo katika bonde takatifu la T'uwa. 12

13. Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa.
13

14. Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila
Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
14

15. Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia
kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya. 15

16. Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini
na akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki. 16

17. Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe
Musa? 17

18. Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na
ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine.
18

19. Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na
radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo,
kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri. 19

20. Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio.
20

21. Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali
yake ya kwanza. 21

22. Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka
mweupe pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine. 22

23. Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa.
23

24. Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepindukia
mipaka. 24

25. (Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie
kifua changu, 25

26. Na unifanyie nyepesi kazi yangu, 26

27. Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu,
27

28. Wapate kufahamu maneno yangu. 28

29. Na nipe waziri katika watu wangu, 29

30. Harun, ndugu yangu. 30

31. Kwake yeye niongeze nguvu zangu. 31

32. Na umshirikishe katika kazi yangu. 32

33. Ili tukutakase sana. 33

34. Na tukukumbuke sana. 34

35. Hakika Wewe unatuona. 35

36. Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa!
36

37. Na hakika tulikwisha kufanyia hisani mara
nyengine... 37

38. Pale tulipo mfunulia mama yako yaliyo funuliwa,
38

39. Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie
mtoni, na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu naye ni adui yake. Na
nimekutilia mapenzi yanayo tokana kwangu, na ili ulelewe machoni mwangu.
39

40. Dada yako alipo kwenda na akasema: Je!
Nikujuulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho
yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ulimuuwa mtu, nasi tukakuokoa katika
dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana.
Kisha ukaja kama ilivyo kadiriwa, ewe Musa! 40

41. Na nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu. 41

42. Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu,
wala msichoke kunikumbuka. 42

43. Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia
mipaka. 43

44. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au
akaogopa. 44

45. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi
tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri. 45

46. Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi.
Nasikia na ninaona. 46

47. Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume
wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu.
Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya
aliye fuata uwongofu. 47

48. Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hapana shaka adhabu
itamsibu anaye kadhibisha na akapuuza. 48

49. (Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani,
ewe Musa? 49

50. Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila
kitu umbo lake, kisha akakiongoa. 50

51. Akasema: Nini hali ya karne za kwanza? 51

52. Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika
Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau. 52

53. Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate
kuongoka. 53

54. Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo
zipo ishara kwa wenye akili. 54

55. Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka
tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia. 55

56. Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini
alikadhibisha na akakataa. 56

57. Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika
nchi yetu kwa uchawi wako? 57

58. Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi
weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo
kuwa sawa. 58

59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu
wakusanywe kabla ya adhuhuri. 59

60. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake,
kisha akaja. 60

61. Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu
uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe!
61

62. Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe,
na wakanong'ona kwa siri. 62

63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka
kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora
kabisa. 63

64. Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa
kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda. 64

65. Wakasema: Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa
sisi wa kwanza kutupa? 65

66. Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na
fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio. 66

67. Basi Musa akaingia khofu nafsi yake. 67

68. Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye
shinda. 68

69. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia;
kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi
hafanikiwi popote afikapo. 69

70. Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema:
Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa! 70

71. (Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni
ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini
nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni
misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika
sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake. 71

72. Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara
waziwazi zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu;
kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu. 72

73. Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili
atusamehe makosa yetu na uchawi ulio tulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu
ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi. 73

74. Hakika ataye mjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu,
basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi. 74

75. Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema,
basi hao ndio wenye vyeo vya juu. 75

76. Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu
humo. Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa. 76

77. Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na
uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu kukamatwa, wala usiogope. 77

78. Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi
kiliwafudikiza humo baharini kilicho wafudikiza. 78

79. Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.
79

80. Enyi Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui
yenu, na tukakuahidini upande wa kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na
Salwa. 80

81. Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni,
wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye
mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia. 81

82. Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye
tubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka. 82

83. Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako,
ewe Musa? 83

84. Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na
nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike. 84

85. (Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani
watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza. 85

86. Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na
kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakukuahidini ahadi
nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu
Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu? 86

87. Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari
yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo
ndivyo alivyo toa shauri Msamaria. 87

88. Na akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na
wakasema: Huyu ndiye mungu wenu, na mungu wa Musa, lakini alisahau. 88

89. Je! Hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala
hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa? 89

90. Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi
watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola
wenu Mlezi ni Arrahmani, Mwingi wa Rehema. Basi nifuateni mimi, na t'iini amri
yangu! 90

91. Wakasema: Hatutaacha kumuabudu mpaka Musa atapo
rejea kwetu. 91

92. (Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilicho kuzuia,
ulipo waona wamepotea, 92

93. Hata usinifuate? Je, umeasi amri yangu? 93

94. Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu
zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usije sema: Umewafarikisha Wana
wa Israil, na hukungojea kauli yangu. 94

95. (Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini ?
95

96. Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao
katika unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi
yangu. 96

97. (Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa
katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na
mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma
moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike. 97

98. Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu.
Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu. 98

99. Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo
tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa. 99

100. Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya
Kiyama atabeba mzigo. 100

101. 101. Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba
Siku ya Kiyama! 101

102. Siku litakapo pulizwa barugumu, na tukawakusanya
wakhalifu Siku hiyo, hali macho yao ya kibuluu. 102

103.
Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku
kumi tu. 103

104. Sisi tunajua zaidi watakayo yasema, atakapo sema
mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu. 104

105. Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola
wangu Mlezi ataivuruga vuruga. 105

106. Na ataiacha tambarare, uwanda. 106

107. Hutaona humo mdidimio wala muinuko. 107

108. Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na
sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa Rahema. Basi husikii ila mchakato
na mnong'ono. 108

109. Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila wa aliye
mruhusu Arrahmani Mwingi wa Rehema na akamridhia kusema. 109

110. Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao.
Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo. 110

111. Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai Milele,
Mwangalizi Mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma. 111

112. Na anaye tenda mema, naye ni Muumini, basi
hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa. 112

113. Na namna hivi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu,
na tumekariri humo maonyo ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee
makumbusho. 113

114.
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala
usiifanyie haraka hii Qur'ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola
wangu Mlezi! Nizidishie ilimu. 114

115. Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau,
wala hatukuona kwake azma kubwa. 115

116. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam!
Wakasujudu, isipo kuwa Iblisi, alikataa. 116

117.
Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa
mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani. 117

118. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
118

119. Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto.
119

120. Lakini Shet'ani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe
Adam! Nikujuulishe mti wa kuishi milele na ufalme usio koma? 120

121. Basi wakaula wote wawili, na uchi wao
ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola
wake Mlezi, na akapotea njia. 121

122. Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia
toba yake, naye akamwongoa. 122

123. Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni
maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye
ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika. 123

124. Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa
yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa
kipofu. 124

125. Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua
kipofu, nami nilikuwa nikiona? 125

126.
(Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo.
Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa.
126

127. Na hivi ndivyo tutakavyo mlipa kila apitaye kiasi,
na asiye amini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali
zaidi, na inadumu zaidi. 127

128. Je! Haikuwabainikia tu; vizazi vingapi
tuliviangamiza kabla yao, nao wanatembea katika maskani zao? Hakika katika hayo
zimo ishara kwa wenye akili. 128

129. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka
kwa Mola wako Mlezi na muda ulio wekwa, bila ya shaka inge fika adhabu (hapa
hapa). 129

130.
Yavumilie haya wayasemayo. Na umtakase Mola wako
Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za
usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha. 130

131. Wala usivikodolee macho tulivyo wastareheshea
baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani, ili tuwajaribu.
Na riziki ya Mola wako Mlezi ni bora na inadumu zaidi. 131

132. Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee
mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na
mwisho mwema ni kwa mchamngu. 132

133. Na walisema: Kwa nini hakutuletea muujiza kutoka
kwa Mola wake Mlezi? Je! Haikuwafikilia dalili wazi ya yaliyomo katika Vitabu
vya kale? 133

134. Na lau kuwa tuliwaangamiza kwa adhabu kabla yake,
wangeli sema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini usituletee Mtume tukazifuata ishara
zako kabla hatujadhilika na kuhizika. 134

135. Sema: Kila mmoja anangoja. Basi ngojeni! Hivi
karibuni mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliye ongoka. 135
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright © 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani