Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu, ambaye ni vyake vyote viliomo mbnguni na katika ardhi. Na sifa ni zake
Yeye katika Akhera. Naye ni Mwenye hikima, Mwenye khabari. 1

2. Anajua yanayo ingia katika
ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda
huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwenye kusamehe. 1

3. Na walisema walio kufuru:
Haitatufikia Saa (ya Kiyama). Sema: Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa
haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichikana kwake
hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho
kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu
chake chenye kubainisha. 3

4. Ili awalipe walio amini na
wakatenda mema. Hao watapata msamaha na riziki ya ukarimu. 4

5. Na wale walio jitahidi
kuzipinga Ishara zetu wakaona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye
uchungu. 5

6. Na walio pewa ilimu wanaona ya
kuwa ulio teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni haki, nayo huongoa kwendea
njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa. 6

7. Na walio kufuru walisema: Je!
Tukujuulisheni mtu anaye kuambieni kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande
mtakuwa katika umbo jipya? 7

8. Ama amemzulia Mwenyezi Mungu
uwongo, au ana wazimu. Bali wasio amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali
kabisa. 8

9. Kwani hawaoni yaliyo mbele yao
na yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ndani
ya ardhi, au tungeli wateremshia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya
zipo Ishara kwa kila mja aliye tubia. 9

10. Na tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, (tukasema):
Enyi milima! Karirini kumtakasa Mwenyezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na
tukamlainishia chuma. 10

11.
(Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na
kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema
mnayo yatenda. 11

12. Na Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake
ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi
mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio
kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye
jitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka. 12

13. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na
masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa
mahala pake. Enyi watu wa Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika
waja wangu wanao shukuru. 13

14. Na tulipo mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha
kufa kwake ila mnyama wa ardhi aliye kula fimbo yake. Na alipo anguka majini
walitambua lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya
kufedhehesha. 14

15. Hakika ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa
katika maskani yao - bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya
Mwenyezi Mungu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu. 15

16. Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na
tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda
makali machungu, na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi. 16

17. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi
kwani tunamuadhibu isipo kuwa anaye kufuru? 17

18. Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka
miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni
humo usiku na mchana kwa amani. 18

19. Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu
baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi
tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo Ishara kwa
kila mwenye kusubiri sana na akashukuru.19

20. Na bila ya shaka Iblisi alihakikisha ile dhana yake
juu yao. Nao walimfuata, isipo kuwa kundi la Waumini. 20

21. Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa
sababu ya kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia
shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu. 21

22. Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa
sababu ya kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia
shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu. 22

23. Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa
kwa aliye mpa idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola
wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa.
23

24. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na
kwenye ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko
kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi. 24

25. Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya,
wala sisi hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi. 25

26. Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha
atatuhukumu kwa haki; na Yeye ndiye Hakimu Mwenye kujua. 26

27. Sema: Nionyesheni mlio waunganisha naye kuwa
washirika. Hasha! Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 27

28. Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na
mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui. 28

29. Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi
mnasema kweli? 29

30. Sema: Nyinyi mnayo miadi ya Siku ambayo
hamtaakhirika nayo kwa saa moja, wala hamtaitangulia. 30

31. Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii,
wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele
ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio
takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi. 31

32. Walio takabari watawaambia wanyonge: Kwani sisi ndio
tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ni wakosefu. 32

33. Na wanyonge wakawaambia walio takabari: Bali ni
vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi
Mungu, na tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na
tutaweka makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo
kuwa wakiyatenda? 33

34. Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila
walisema walio jidekeza kwa starehe zao wa mji huo: Hakika sisi tunayakataa hayo
mliyo tumwa nayo. 34

35. Na wakasema: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto,
wala sisi hatutaadhibiwa. 35

36. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na
humdhikisha amtakaye. Lakini watu wengi hawajui. 36

37. Na si mali yenu wala watoto wenu watakao
kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao
basi watapata malipo mardufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika
maghorofa. 37

38. Na wanao jitahidi kuzipinga Ishara zetu, wakaona
watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu. 38

39. Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki
na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye
atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku. 39

40. Na siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia
Malaika: Je! Hawa walikuwa wakikuabuduni? 40

41. Waseme: Subhanak, Umetakasika. Wewe ndiye kipenzi
chetu si hao. Bali wao walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao. 41

42. Hii leo hataweza yeyote kumletea nafuu wala madhara
mwenzie. Na tutawaambia walio dhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mlio kuwa
mkiukanusha. 42

43. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu
si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu.
Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru
waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri. 43

44. Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia
Mwonyaji kabla yako wewe. 44

45. Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na
hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao
waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani! 45

46. Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya
kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha
mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla
ya kufika adhabu kali. 46

47. Sema: Ujira nilio kuombeni ni wenu nyinyi. Sina
ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu. 47

48. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anaondoa upotovu kwa
Haki. Yeye ndiye Mwenye kujua vyema yaliyo ghaibu. 48

49. Sema: Kweli imefika, na uwongo haujitokezi, wala
haurudi. 49

50. Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa
kudhuru nafsi yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya
kunifunulia Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu. 50

51. Na lau ungeli ona watapo babaika, basi hapana pa
kukimbilia! Na watakamatwa mahala pa karibu. 51

52. Na watasema: Tunaiamini! Lakini wataipata wapi
kutoka huko mahala mbali? 52

53. Na hapo kabla yake waliikataa, na wakiyatupilia
mbali maneno ya ghaibu kutoka mahali mbali. 53

54. Na watatiliwa kizuizi baina yao na hayo wanayo
yatamani, kama walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya
kutia wasiwasi. 54
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani