Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye
mawaidha. 1

2. Lakini walio kufuru wamo
katika majivuno na upinzani 2

3. Mataifa mangapi tumeyaangamiza
kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita. 
4. Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana nao
wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo. 4

5. Amewafanya miungu wote kuwa ni
Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. 5

6. Na wakaondoka wakubwa wao
wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo
pangwa. 6

7. Sisi hatukusikia haya katika
mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu. 7

8. Ati yeye tu ndiye aliye
teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha
yangu, bali hawajaionja adhabu yangu. 8

9. Au wanazo wao khazina za
rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji? 9

10. Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo
kati yao? Basi nawazipande njia za kwendea huko! 10

11. Hao ni askari watao shindwa miongoni mwa makundi
yatayo shindwa. 11

12. Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi
na Firauni mwenye majengo. 12

13. Na Thamud na kaumu Lut'i na watu wa Machakani. Hayo
ndiyo makundi. 13

14. Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki
adhabu yangu. 14

15. Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na
muda. 15

16. Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu
yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu. 16

17. Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu
Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia. 17

18. Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi
jioni na asubuhi pamoja naye. 18

19. Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi;
wote walikuwa wanyenyekevu kwake. 19

20. Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na
kukata hukumu. 20

21. Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo
pindukia ukuta kuingia chumbani? 21

22. Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema:
Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi
tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa. 22

23. Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini
na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na
amenishinda kwa maneno. 23

24. Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako
mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao
kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi
akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na
akaanguka kusujudu na kutubia. 24

25. Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao
mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu. 25

26. Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa
katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza
kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu
wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu. 26

27. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao
bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata. 27

28. Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama
wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu? 28
29. Na hiki Kitabu,
tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike
wenye akili.
29

30. Na Daudi tukamtunukia Suleiman.
Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia.
30
31. Alipo pelekewa jioni farasi wasimamao kidete, tayari
kutoka shoti;

32. Basi
akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha
wakafichikana nyuma ya boma.
33. Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo.
34. Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili
juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu.

35. Akasema: Mola wangu Mlezi!
Nisamehe na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye
Mpaji.
36. Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri
yake, popote alipo taka kufika.
37. Na tukayafanya mashet'ani yamtumikie, wote wajenzi
na wapiga mbizi.
38. Na wengine wafungwao kwa
minyororo.
39. Hichi ndicho kipawa chetu. Basi toa au zuia, bila
ya hisabu.
40. Na hakika yeye kwetu Sisi ana cheo cha kukaribishwa
kwetu, na pahala pazuri pa kurejea.

41. Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake
Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu. 41

42.
(Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi
haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa. 42

43. Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja
nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili. 43
44. Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha
ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa
waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.
44
45. Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na
Yaa'qubu walio kuwa na nguvu na busara.
45
46. Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa
Akhera.
46
47. Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora.
47
48. Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote
hao ni katika walio bora.
48
49. Huu ni ukumbusho. Na hakika wachamngu wana marudio
mazuri.
49
50. Bustani za milele zitazo funguliwa milango yao kwa
ajili yao.
50
51. Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda
mengi na vinywaji.
51
52. Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu
zao.
52
53. aya ndiyo mliyo ahidiwa kwa Siku ya Hisabu.
53

54. Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika. 54

55. Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka
watapata marudio maovu kabisa; 55

56. Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni
kitanda kiovu mno cha kulalia. 56

57. Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya
usaha! 57

58. Na adhabu nyenginezo za namna hii. 58

59. Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana
makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni. 59

60. Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi
ndio mlio tusabibisha haya, napo ni pahala paovu kabisa! 60

61. Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliye tusabibisha haya
mzidishie adhabu mara mbili Motoni. 61

62. Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao
tukiwahisabu ndio katika waovu? 62

63. Tulikosea tulipo wafanyia maskhara, au macho yetu tu
hayawaoni ? 63

64. Hakika hayo bila ya shaka ndiyo makhasimiano ya watu
wa Motoni. 64

65. Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu
ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu, 65

66. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yake,
Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe. 66

67. Sema: Hii ni khabari kubwa kabisa. 67

68. Ambayo nyinyi mnaipuuza. 68

69. Sikuwa na ilimu ya mambo ya viumbe wakuu watukufu
walipo kuwa wakishindana. 69

70.
Haikufunuliwa kwangu isipo kuwa ya kwamba hakika
mimi ni mwonyaji dhaahiri. 70

71. Mola wako Mlezi alipo
waambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo.

72. Na nitakapo mkamilisha na
kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kumt'ii.

73. Basi Malaika wakat'ii wote
pamoja.

74. Isipo kuwa Iblisi;
alijivuna na akawa katika makafiri.

75. Mwenyezi Mungu akamwambia:
Ewe Iblisi! Kipi kilicho kuzuia kumt'ii yule niliye muumba kwa mikono yangu? Je!
Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli?

76. Akasema: Mimi ni bora
kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo.

77. Akasema: Basi toka humo,
kwani hakika wewe umelaanika.

78. Na hakika laana yangu
itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo.

79. Akasema: Mola wangu Mlezi!
Nipe muhula mpaka siku watayo fufuliwa viumbe.

80. Mwenyezi Mungu akasema:
Basi umekwisha kuwa miongoni mwa walio pewa muhula,

81. Mpaka siku ya wakati maalumu. 81

82. Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya
shaka nitawapoteza wote, 82

83. Isipo kuwa wale waja wako miongoni mwao walio
khitariwa. 83

84. kasema: Haki! Na haki ninaisema. 84

85. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa
hao wote wenye kukufuata miongoni mwao. 85

86. Sema (Ewe Mtume) : Sikuombeni ujira juu ya haya,
wala mimi si katika wadanganyifu. 86

87. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. 87

88. Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda. 88
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani