Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Alif Lam Mym Ra. (A.L.M.R.) Hizi ni Ishara za Kitabu.
Na uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu
hawaamini. 1

2. Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo
mnazo ziona, ametawala kwenye Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii,
kila kimoja kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua
Ishara ili mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi. 2

3. Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima
na mito. Na katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya
mchana. Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri. 3

4. Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na
zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye
shina moja na isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na
tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo
ishara kwa watu wanao tia mambo akilini. 4

5. Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo
usemi wao: Ati tukisha kuwa mchanga kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio
walio mkufuru Mola wao Mlezi. Na hao ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao,
na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu. 5

6. Na wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya
kuwa zimekwisha pita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako
Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi
ni Mkali wa kuadhibu. 6

7. Na wale walio kufuru husema: Mbona hakuteremshiwa
muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina
wa kuwaongoa. 7

8. Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila mwanamke, na
kinacho punguka na kuzidi matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo. 8

9. Yeye ndiye Mwenye kujua yanayo onekana na yasio
onekana; Mkuu Aliye tukuka. 9

10. Ni sawa anaye ficha kauli yake kati yenu na anaye
idhihirisha, na anaye jibanza usiku na anaye tembea jahara mchana. 10

11. Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma
yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili
yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu
anapo watakia watu adhabu hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala
yake. 11

12. Yeye ndiye anaye kuonyesheni umeme kwa khofu na
tamaa, na huyaleta mawingu mazito. 12

13. Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na
Malaika pia, kwa kumkhofu. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao
wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali! 13

14. Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba
badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake
kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri
hayako ila katika upotovu. 14

15. Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia
Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni. 15

16. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema:
Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi,
nao hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa
sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu
washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia?
Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye
kushinda! 16

17.
Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde
yakamiminika maji kwa kadiri yake. Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo
kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo yayusha katika moto kwa kutaka
mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo
anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile povu linapita kama takataka tu
basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu
anavyo piga mifano. 17

18. Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na
wasio muitikia, hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa
hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya
kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno! 18

19. Je! Anaye jua ya kwamba yaliyo teremshwa kwako
kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Wenye akili ndio
wanao zingatia, 19

20. Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala
hawavunji maagano. 20

21. Na wale ambao huyaunga aliyo amrisha Mwenyezi Mungu
yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya. 21

22. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao
Mlezi, na wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo
wapa; na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya
Akhera. 22

23. Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio
wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika
wanawaingilia katika kila mlango. 23

24.
(Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu,
kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera. 24

25. Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya
kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi
katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya. 25

26. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na
humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa
kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo. 26

27. Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa
muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea
amtakaye, na humwongoa anaye elekea kwake, 27

28. Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka
Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! 28

29. Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha
na marejeo mazuri. 29

30. Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha
pita kabla yao umati nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao wanamkufuru
Rahmani, Mwingi wa Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hapana mungu isipo
kuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo yangu! 30

31. Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa
milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani
hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba lau
kuwa Mwenyezi Mungu ange penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala
walio kufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia
karibu na nyumbani kwao, mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu havunji miadi yake. 31

32. Na hakika walifanyiwa kejeli Mitume walio kuwa kabla
yako. Na nikawapururia wale walio kufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje
adhabu yangu! 32

33. Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo
yachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au
ndio mnampa khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali
walio kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi
Mungu amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa. 33

34. Wanayo adhabu katika maisha ya dunia, na adhabu ya
Akhera hapana shaka ina mashaka zaidi. Na wala hawatakuwa na wa kuwalinda na
Mwenyezi Mungu. 34

35. Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake
inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa
wale walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto. 35

36. Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa.
Na katika makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa
nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo
ninaita, na kwake Yeye ndio marejeo yangu. 36

37. Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni
hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu
hii, hutakuwa na rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu. 37

38. Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako,
na tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo
kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake. 38

39. Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na
asili ya hukumu zote iko kwake. 39

40. Na ikiwa tukikuonyesha baadhi ya tuliyo waahidi au
tukakufisha kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe na juu yetu ni hisabu.
40

41. Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza
nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye
ni Mwepesi wa kuhisabu. 41

42. Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri
watajua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera! 42

43. Na walio kufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema:
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye
ilimu ya Kitabu. 43
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani