Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI
WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Qaaf. Naapa kwa Qur'ani tukufu! 1

2. Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka
miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu! 2

3. Ati tukifa na tukawa udongo...? Kurejea huko kuko
mbali! 3

4. Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa
na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote. 4

5. Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo
katika mambo ya mkorogo. 5

6. Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo
zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa. 6

7. Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na
tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna. 7

8. Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja
mwenye kuelekea. 8

9. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa,
na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. 9

10. Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,
10

11. Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa
maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.
11

12. Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa
Rassi na Thamudi. 12

13. Na A'di na Firauni na kaumu ya Lut'i. 13

14. Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa'. Wote
hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao. 14

15. Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao
wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya. 15

16. Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo
mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni
mwake. 16

17. Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na
kushotoni. 17

18. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.
18

19. Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo
ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia. 19

20. Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
20

21. Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na
shahidi. 21

22. (Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya;
basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.
22

23. Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha
tayarishwa. 23

24. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,
24

25. Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,
25

26. Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Basi mtupeni katika adhabu kali. 26

27. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza
mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali. 27

28. (Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu.
Nilikuleteeni mbele onyo langu. 28

29. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi
siwadhulumu waja wangu. 29

30. Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo
itasema: Je! Kuna ziada? 30

31. Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu,
haitakuwa mbali. 31

32. Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa
Mwenyezi Mungu na akajilinda. 32

33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni,
na akaja kwa moyo ulio elekea 33

34. (Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya
daima dawamu. 34

35. Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
35

36. Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa
na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata
pa kukimbilia? 36

37. Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au
akatega sikio naye yupo anashuhudia. 37

38. Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na
vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu. 38

39. Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa
kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. 39

40. Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
40

41. Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka
pahala karibu. 41

42. Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku
ya kufufuka. 42

43. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi
ndio marejeo. 43

44. Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo
kwetu ni mwepesi. 44

45. Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye
kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur'ani anaye liogopa onyo.
45
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani