Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake: Uwaonye
kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu. 1

2. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni
mwonyaji wa dhaahiri kwenu, 2

3. Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye,
na mumt'ii. 3

4. Atakughufirieni madhambi yenu, na atakuakhirisheni
mpaka muda ulio wekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapo fika haucheleweshwi.
Laiti mngejua! 4

5. Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita
watu wangu usiku na mchana, 5

6. Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia.
6

7. Na hakika mimi kila nilipo waita ili upate
kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao,
na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno! 7

8. Tena niliwaita kwa uwazi, 8

9. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao
kwa siri. 9

10. Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi;
hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. 10

11. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. 11

12. Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani
na atakufanyieni mito. 12

13. Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu?
13

14. Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja?
14

15. Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba
mbingu saba kwa matabaka? 15

16. Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na
akalifanya jua kuwa taa? 16

17. Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama
mimea. 17

18. Kisha atakurudsheni humo na atakutoeni tena.
18

19. Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kama
busati. 19

20. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana. 20

21. Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika hao
wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila
khasara. 21

22. Na wakapanga vitimbi vikubwa. 22

23. Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache
Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. 23

24. Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala
usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea. 24

25. Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa
wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
25

26. Na Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Usimwache juu
ya ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri! 26

27. Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao
hawatazaa ila waovu makafiri. 27

28. Mola wangu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu,
na kila aliye ingia nyumbani mwangu kuwa ni mwenye kuamini, na Waumini wote
wanaume, na Waumini wanawake. Na wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea.
28
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani