Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Kaf Ha Ya A'yn S'ad. 1

2. Huu ni Ukumbusho wa rehema ya Mola wako Mlezi kwa
mja wake, Zakariya. 2

3. Alipo mwita Mola wake Mlezi kwa siri. 3

4. Akasema: Mola wangu Mlezi! Mafupa yangu
yamedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi; wala, Mola wangu Mlezi, sikuwa
mwenye bahati mbaya kwa kukuomba Wewe. 4

5. Na hakika mimi nawakhofia jamaa zangu baada yangu.
Na mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako. 5

6. Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo wa Yaaqub. Ewe
Mola wangu Mlezi! Na umjaalie awe mwenye kuridhisha. 6

7. (Akaambiwa): Ewe Zakariya! Hakika Sisi
tunakubashiria mwana; jina lake ni Yahya. Hatujapata kumpa jina hilo yeyote
kabla yake. 7

8. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nitakuwa na
mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimesha fikia ukongwe katika uzee? 8

9. Akasema: Ndio hivyo hivyo amesema Mola wako Mlezi:
Haya ni mepesi kwangu. Na hakika Mimi nilikwisha kuumba wewe zamani na hali
hukuwa kitu. 9

10. Akasema: Mola wangu Mlezi nijaalie Ishara. Akasema
Ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima. 10

11. Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni.
Akawaashiria: Msabihini Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni. 11

12. Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa
hikima angali mtoto. 19

13. Na tukampa huruma itokayo kwetu, na utakaso, na
akawa mcha mungu. 13

14. Na akawa mwema kwa wazazi wake, wala hakuwa jabari
muasi 14

15. Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya
kufa, na siku ya kufufuliwa. 15

16. Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipo jitenga
na jamaa zake mahali upande wa mashariki. 16

17. Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho
wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu. 17

18. (Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi
wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mchamngu. 18

19. (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na
Mola wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliye takasika. 19

20. Akasema: Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote
hajanigusa, wala mimi si kahaba? 20

21. (Malaika) akasema: Ndio hivyo hivyo! Mola wako
Mlezi amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu,
na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lilio kwisha hukumiwa. 21

22. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka
mahali pa mbali. 22

23. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende;
akasema: Laiti ningeli kufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa! 23

24.
Pakatangazwa kutoka chini yake: Usihuzunike! Hakika
Mola wako Mlezi amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji! 24

25. Na litikise kwako hilo shina la mtende,
utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu. 25

26. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi
ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu
ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu. 26

27. Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba.
Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu! 27

28. Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu,
wala mama yako hakuwa kahaba. 28

29.
Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze
aliye bado mdogo yumo katika mlezi. 29

30. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale
niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai. 30

31. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale
niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai. 31

32. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe
jeuri, mwovu. 32

33. Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku
nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai. 33

34. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya
haki ambayo wanaifanyia shaka. 34

35. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu,
Yeye ametakasika! Anapo lihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa. 35

36. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na
Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. 36

37. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi
ole wao hao walio kufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu! 37

38. Watasikia na wataona vizuri vilioje Siku watakayo
tufikia! Lakini madhaalimu sasa wamo katika upotofu ulio dhaahiri. 38

39. Na waonye siku ya majuto itapo katwa amri. Nao wamo
katika ghafla, wala hawaamini. 39

40. Hakika Sisi tutairithi ardhi na walio juu yake. Na
kwetu watarejeshwa. 40

41. Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa
mkweli, Nabii. 41

42. Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini
unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote? 42

43. Ewe baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyo
kufikia wewe. Basi nifuate mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa. 43

44. Ewe baba yangu! Usimuabudu Shet'ani. Hakika
Shet'ani ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rehema. 44

45. Ewe baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate
adhabu inayo toka kwa Mwingi wa Rehema ukaja kuwa mwenziwe Shetani. 45

46. (Baba) akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe
Ibrahim? Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa
muda! 46

47. (Ibrahim) akasema: Salamun a'laika! Amani iwe juu
yako! Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ananihurumia
sana. 47

48. Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala
ya Mwenyezi Mungu. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa
bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi. 48

49. Basi alipo jitenga nao na yale waliyo kuwa
wakiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na Yaaqub, na kila mmoja
tukamfanya Nabii. 49

50. Na tukawapa rehema zetu na tukawajaalia kupewa sifa
za kweli tukufu. 50

51. Na mtaje Musa katika Kitabu. Hakika yeye alikuwa ni
mwenye kuchaguliwa, na alikuwa Mtume, Nabii. 51

52. Na tulimwita upande wa kulia wa mlima na
tukamsogeza kunong'ona naye. 52

53. Nasi kwa rehema zetu tukampa nduguye, Harun, awe
Nabii. 53

54. Na mtaje katika Kitabu Ismail. Bila ya shaka yeye
alikuwa ni mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume, Nabii. 54

55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake Sala na Zaka, na
alikuwa mbele ya Mola wake Mlezi mwenye kuridhiwa. 55

56. Na mtaje katika Kitabu Idris. Hakika yeye alikuwa
ni mkweli Nabii. 56

57. Na tulimuinua daraja ya juu. 57

58. Hao ndio alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni
mwa Manabii katika uzao wa Adam, na katika uzao wa wale tulio wapandisha pamoja
na Nuhu, na katika uzao wa Ibrahim na Israil, na katika wale tulio waongoa na
tukawateuwa. Wanapo somewa Aya za Mwingi wa Rehema huanguka kusujudu na kulia. 58
![image]()
59. Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Sala, na wakafuata matamanio.
Basi watakuja kuta malipo ya ubaya. 59

60. Isipo kuwa walio tubu, wakaamini, na wakatenda
mema. Hao, basi, wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa chochote. 60

61. Bustani za milele alizo waahidi Rahmani waja wake
katika siri. Hakika ahadi yake hapana shaka itafika. 61

62. Humo hawatasikia upuuzi, ila Salama tu. Na watapata
humo riziki zao asubuhi na jioni. 62

63. Hiyo ndiyo Pepo tutayo warithisha katika waja wetu
walio kuwa wachamngu. 63

64. (Nao watasema:) Wala hatuteremki ila kwa amri ya
Mola wako Mlezi. Ni yake Yeye yaliyoko mbele yetu na yaliyoko nyuma yetu, na
yaliyomo katikati ya hayo. Na Mola wako Mlezi si mwenye kusahau. 64

19. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyo baina
yake. Basi muabudu Yeye tu, na udumu katika ibada yake. Je, mnamjua mwenye jina
kama lake? 65

66. Na mwanaadamu husema: Hivyo, nitakapo kufa, ni
kweli nitafufuliwa niwe hai tena? 66

67. Je! Hakumbuki mwanaadamu ya kwamba tulimuumba
kabla, na hali hakuwa chochote? 67

68. Basi naapa kwa Mola wako Mlezi! Kwa yakini
tutawakusanya wao pamoja na mashet'ani; kisha tutawahudhurisha kuizunguka
Jahannamu, nao wamepiga magoti. 68

69. Kisha kwa yakini tutawatoa katika kila kundi wale
miongoni mwao walio zidi kumuasi Arrahmani, Mwingi wa Rahema. 69

70. Tena hakika Sisi tunawajua vyema zaidi wanao
stahiki kuunguzwa humo. 70

71. Wala hapana yeyote katika nyinyi ila ni mwenye
kuifikia. Hiyo ni hukumu ya Mola wako Mlezi ambayo lazima itimizwe. 71

72. Kisha tutawaokoa wale walio mchamngu; na tutawaacha
madhaalimu humo wamepiga magoti. 72

73. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru
huwaambia walio amini: Lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lilio
bora barazani? 73

74. Na kaumu ngapi tuliziangamiza zilizo kuwa na
mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa kuwatazama! 74

75. Sema: Walio katika upotofu basi Arrahmani Mwingi wa
Rahema atawapururia muda mpaka wayaone waliyo onywa - ama ni adhabu au ni Saa.
Hapo ndipo watapo jua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu. 75

76. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wenye
kushika uwongofu. Na mema yenye kudumu ni bora katika malipo mbele ya Mola wako
Mlezi na yana mwisho mwema. 76

77. Je, umemwona aliye zikanya Ishara zetu na akasema:
Kwa hakika mimi nitapewa mali na wana! 77

78. Kwani yeye amepata khabari za ghaibu, au amechukua
ahadi kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema? 78

79 Hasha! Tutaandika anayo yasema, tutamkunjulia muda
wa adhabu. 79

80. Na tutamrithi hayo anayo yasema, na atatufikia
mtupu peke yake! 80

81. Na wamechukua miungu mingine badala ya Mwenyezi
Mungu ili ati iwape nguvu. 81

19. Sivyo kabisa! Wataikataa hiyo ibada yao, na
watakuwa ndio dhidi yao. 82

19. Kwani huoni ya kwamba tumewatuma mashet'ani kwa
makafiri wawachochee kwa uchochezi?. 83

19. Basi usiwafanyie haraka. Sisi tunawahisabia idadi
ya siku zao. 84

19. Siku tutayo wakusanya wachamngu kuwapeleka kwa
Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa ni wageni wake. 86

19. Na tukawachunga wakhalifu kuwapeleka Jahannamu hali
ya kuwa wana kiu. 86

19.
Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale walio
chukua ahadi kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema. 87

19. Na wao ati husema kuwa Arrahmani Mwingi wa Rehema
ana mwana! 88

19. Hakika mmeleta jambo la kuchusha mno! 89

19.
Zinakaribia mbingu kutatuka kwa hilo, na ardhi
kupasuka, na milima kuanguka vipande vipande. 90

19. Kwa kudai kwao kuwa Arrahmani Mwingi wa Rehema ana
mwana. 91

19. Wala hahitajii Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa na
mwana. 92

19. Hapana yeyote aliomo mbinguni na ardhini ila
atafika kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa ni mtumwa wake. 93

19. Yeye hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa. 94

19. Na kila mmoja katika wao atamfikia Siku ya Kiyama
peke yake. 95

19. Hakika walio amini na wakatenda mema Arrahmani
Mwingi wa Rehema atawajaalia mapenzi. 96

19. Na hakika tumeifanya nyepesi (Qur'ani) kwa ulimi
wako, ili uwabashirie kwayo wachamngu, na uwaonye kwayo watu wabishi. 97

19. Na kaumu ngapi tumezihiliki kabla yao. Je! Unawaona
hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao. 98
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani