1,2. Yamekushughulisheni mkaacha kutimiza yaliyo
waajibu na ya ut'iifu kule kujitapa kwenu kwa wana na wafwasi, na kujifakhiri
kwa mali, na hisabu, na nasaba, mpaka yakusibuni mauti!
3. Hakika mtakuja jua matokeo ya upumbavu wenu na mapuuza yenu.
4. Na hakika bila ya shaka mtakuja jua natija ya hayo!
5. Ama kwa hakika lau mngeli jua kwa yakini uovu wa mwisho wenu
bila ya shaka mngeli ogopa huko kushindania kurindika mali, na mngeli
jitengenezea Akhera yenu.
6. Nakuapieni na nakutilieni mkazo, enyi watu, kwamba hakika
nyinyi mtakuja ushuhudia Moto unao waka.
7. Kisha ninaapa na natilia mkazo kwamba mtauona wazi na kwa
yakini.
8. Tena naapa na natilia mkazo kwamba hakika nyinyi mtahisabiwa kwa neema mlizo deka nazo na mkazistarehea.