1. AL-QAARIA'H, Inayo gonga, ni Kiyama, ambacho kinaanza kwa
mpulizo wa mwanzo wa barugumu, na kinaishia itapo katwa hukumu baina ya watu.
2. Kitu gani kilicho cha ajabu zaidi katika ukuu wake, na
khatari zake na kitisho chake!
3. Na kitu gani kitacho kujuulisha hali ya AL-QAARIA'H katika
kitisho chake juu ya nafsi za watu?
4. Siku hiyo watu watakuwa kama vipepeo kwa wingi na kuhangaika
kulia na kushoto, madhaifu na wanyonge!
5. Na milima itakuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na kuchambuliwa
kwa kutapanyika vipande mbali mbali na kupeperuka katika anga huku na huku.
6,7. Ama yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, mema
yake yakapindukia kuliko maovu yake, basi huyo atakuwa na maisha yatayo
mridhisha mwenyewe, na nafsi yake itue.
8,9. Na ama ambaye mizani yake itakuwa nyepesi, na
maovu yake yakazidi kuliko mema yake, basi makaazi yake yatakuwa Jahannamu.
10. Na nini cha kukujuulisha ni nini Hawiya?
11. Moto ulio mkali, hapana moto unao fikilia ukali wake, hata ukichochewa vipi na kutiwa kuni gani!