1. Ninaapa kwa farasi wa Jihadi wendao mbio, na huku pumzi zao zinasikilizana kwa sauti inayo itwa "Dh'abh'an".

 

2. Na kwa farasi hao ambao hutoa cheche za moto zinapo gonga kwato zao kwenye ardhi wanapo kwenda.

 

3. Na kwa farasi hao wanao washambulia maadui asubuhi kabla jua halijachomoza;

 

4. Wakatimua mavumbia mengi, farasi hao, kati ya makundi ya maadui!

 

5. Ikawa vumbi limewagubika maadui hata wakaingiwa kiwewe na kufazaika.

 

6. Hakika mwanaadamu ni mwingi wa kuzikufuru neema za Mola wake Mlezi ambazo hazikadiriki.

 

7. Na hakika yeye mwenyewe bila ya shaka atakuwa mwingi wa kuja jishuhudia huko Akhera kwa kuungama madhambi yake.

 

8. Na hakika yeye kwa uchoyo na kuyapenda mali alio nayo, ni bakhili, hatoi kama inavyo mwajibikia katika mali yake.

 

9,10. Kwani hajui mwisho wa hali yake, hata hajui wakitolewa maiti waliomo makaburini, na vikakusanywa viliomo vifuani navyo vimekwisha sajiliwa katika madaftari yao, yakiwa mema au mabaya waliyo yatenda?

 

11. Kwamba hakika Mlezi wao na Muumba wao bila ya shaka anajua vyema vitendo vyao na malipo yao Siku ya Kufufuliwa na Kulipwa.