1. Hawakuwa walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake miongoni
mwa Mayahudi na Wakristo, na miongoni mwa washirikina, waache kughafilika kwao
na ujinga wao kuto ijua Haki mpaka iwajie hoja ya kukata.
2,3. Na hoja hiyo ni Mtume aliye tumwa kutokana na
Mwenyezi Mungu awasomee kurasa zilizo takasika na upotovu, ndani yake zimo
hukumu zilizo sawa zenye kutamka kwa haki na kwa yaliyo ndiyo.
4. Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu katika Mayahudi na
Wakristo, ila baada ya kuwajia hiyo hoja iliyo wazi yenye kuonyesha ya kwamba
Muhammad ndiye huyo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliye ahidiwa katika Vitabu vyao.
5. Na hawakulazimishwa jambo katika walio lazimishwa ila iwe
ibada yao kwa Mwenyezi Mungu ni kumsafia Yeye Dini, waache upotovu wasimame sawa
kwenye Haki, na wazihifadhi Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Mila Iliyo
Nyooka.
6. Hakika wale walio kufuru katika Watu wa Kitabu na
washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu, wala hawatatoka humo. Hao ndio
waovu wa viumbe kwa itikadi na vitendo.
7. Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
wakatenda vitendo vyema, hao ndio bora ya viumbe kwa itikadi na vitendo.
8. Malipo yao Akhera kwa Imani na vitendo vyema walivyo vitanguliza, ni Mabustani ya kudumu yenye kupitiwa na mito kati yake, watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu amepokea a'mali zao, na wao watamshukuru kwa hisani yake aliyo wafanyia. Hiyo ndiyo jaza ya mwenye kuiogopa adhabu ya Mola wake Mlezi, akaamini na akatenda mema.