1. Ewe Muhammad! Soma unayo funuliwa kwa kufunguliwa kwa Jina la Mola wako Mlezi ambaye ni Yeye tu peke yake ndiye Mwenye uweza wa kuumba.

 

2. Amemuumba mtu kwa ukamilifu wa mwili wake na ilimu kutokana na kipande cha damu ambacho hakina chochote cha kupelekea kujiona bora.

 

3. Endelea na kusoma, na Mola wako Mlezi aliye Karimu kushinda wote, atakutukuza wala hatakudharau.

 

4. Yeye ndiye ambaye aliye mfunza mtu kuandika kwa kalamu, na wala kwanza hakuwa anajua hayo.

 

5. Amemfunza mtu yasiyo kuwa yanampitia katika mawazo yake.

 

6,7. Ni hakika kweli mtu hupindukia mpaka na hupanda kiburi mbele ya Mola wake Mlezi anapo jiona si mhitaji, katajirika.

 

8. Ewe Muhammad! Hakika ni kwa Mola wako Mlezi peke yake ndiyo yako marejeo ya wote kwa kufufuliwa na kulipwa.

 

9,10. Je! Umemwona huyu jeuri anaye mzuia mja asisali anapo taka kusali?

 

11,12. Hebu niambie khabari za jeuri huyu kama yeye yumo katika uwongofu katika huku kuzuia kwake, au kwamba ndio anaamrisha uchamngu katika hayo anayo amrisha!

 

13. Niambie khabari za huyu mwenye kukataza anapo yakadhibisha aliyo kuja nayo Mtume, na akapuuza Imani na vitendo vyema!

 

14. Hivyo hajui kwamba Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zake, naye atamlipa kwazo?

 

15. Kwa kumkemea huyu mwenye kuzuia, anaambiwa kama hakuacha hayo anayo yafanya, basi hapana shaka tutamkokota kwa nguvu tukimshika kwa shungi lake la nywele mpaka Motoni!

 

16. Hilo shungi lilio juu ya uso wake mwenye kuropokwa uwongo na mwenye athari za ukosefu!

 

17. Basi yeye awaite wenziwe na watu wa baraza lake wawe ndio wasaidizi duniani au Akhera.

 

18. Sisi tutawaita askari wetu wamsaidie Muhammad na walio pamoja naye, na wapambane na huyo mwenye kukanya na wasaidizi wawasukume kwenye Jahannamu!

 

19. Kumnyamazisha huyu mwenye kuzuia, wewe usimkubalie kwa hayo anayo kukataza nayo, na dumu juu ya Sala zako, na endelea na sijida zako, na jijongeze kwa Mola wako Mlezi kwa hivyo.