1. Naapa kwa tini na zaituni, kwa baraka zao na ubora wa
manufaa yao.
2. Na kwa mlima ambao juu yake ndio Mwenyezi Mungu alimsemeza
Musa.
3. Na kwa huu mji mtukufu wa Makka, ambao anaushuhudia utukufu
wake mwenye kwenda uzuru, na anapata amani mwenye kuuingia.
4. Kwa hakika bila ya shaka yoyote Sisi tumemuumba mtu
amesimama sawa kwa umbo bora kabisa lilio nyooka, na akasifika kwa sifa nzuri
kabisa.
5. Kisha tukamteremsha cheo mpaka akawa ni wa chini kabisa
katika hao walioko chini, kwa kuacha kufanya waajibu wa hayo tuliyo muumbia.
6. Lakini walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao basi
watapata ujira usio wakatikia wala kuwapungukia.
7. Basi kitu gani kinacho kupelekea kukadhibisha kufufuliwa na
kulipwa baada ya kuwekwa wazi uweza wetu wa hayo?
8. Kwani Mwenyezi Mungu aliye yatenda hayo tuliyo kueleza si muadilifu kuliko mahakimu wote kwa kufanya na kupanga?