1. Naapa kwa usiku kinapo enea kiza chake!

 

2. Na naapa kwa mchana unapo zagaa mwangaza wake!

 

3. Na naapa kwa Mjuzi aliye umba viwili viwili, dume na jike, katika kila vinavyo zaliwa!

 

4. Hakika juhudi zenu bila ya shaka zimekhitalifiana; kwani wapo wenye kubahatika katika juhudi zao, na wako wasio bahatika.

 

5,6,7. Ama mwenye kutoa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na akamkhofu Mola wake Mlezi, na kwa hivyo akaepuka anayo yakataza, na akayakinika kufuata fadhila njema, nayo ni Imani kumuamini Mwenyezi Mungu kwa kumjua, basi Sisi tutamtengenezea awe katika khulka ya wepesi na raha kwa kumwongoza kwenye njia ya kheri.

 

8,9,10. Ama mwenye kufanya ubakhili kwa mali yake asitoe haki ya Mwenyezi Mungu iliomo humo, na akawa hana haja na yatokayo kwa Mwenyezi Mungu, na akakadhibisha khulka nzuri, basi huyo tutamtengenezea khulka ambayo inapelekea uzito na mashaka ya milele.

 

11. Na kitu gani katika adhabu ambacho hayo mali yake yataweza kumkinga nacho, atapo teketea yeye mwenyewe mzima?

 

12. Hakika ni juu yetu, Sisi, kwa kufuatana na hikima yetu, ndio tuwabainishie viumbe njia ya uwongofu.

 

13. Na juu yetu Sisi peke yetu, bila ya shaka, hili jambo la kuendesha yaliomo duniani na Akhera.

 

14. Ndio maana tukakutieni khofu ya Moto unao waka na kuripuka!

 

15,16. Hawauingii kwa kudumu ila kafiri aliye ikadhibisha Haki na akazipuuza Ishara za Mola wake Mlezi.

 

17,18. Na atakuwa mbali na huo Moto aliye mwingi wa kujikinga na ukafiri na maasi, amabye hutoa mali yake wakati wa nafasi ili kujisafisha na uchafu wa ubakhili, na najsi ya uchoyo.

 

19. Na mtoaji huyu si kama anaye mtu yeyote ambaye ndio anamlipa kwa neema aliyo mfanyia zamani,

 

20. Bali anatoa hicho kwa kutafuta radhi ya Mola wake Mlezi Mtukufu tu.

 

21. Na bila ya shaka atakuja pata kutoka kwa Mola wake Mlezi anacho kitaka kwa njia za ukamilifu kabisa, hata itimie radhi kwake.