1. Naapa kwa jua na mwangaza wake na kuchomoza kwake na kwa
joto lake!
2. Na kwa mwezi unapo lifuata na likawa nyuma yake kwa kutoa
mwangaza baada ya kuchwa jua,
3. Na kwa mchana unapo lidhihirisha jua, likaonekana wazi
halikufichikana.
4. Na kwa usiku unapo lifunika jua, ukawa mwangaza wake
hauonekani.
5. Na kwa mbingu na kwa Mweza Mtukufu aliye inyanyua na
akaijenga kwa hikima yake.
6. Na kwa ardhi na kwa Mweza Mtukufu aliye ikunjua kwa kila
upande, na akaitengeneza kwa ajili ya utulivu, na akaifanya kama tandiko.
7. Na kwa nafsi, na aliye iumba na akaiweka sawa, kwa kuipa
nguvu,
8. Akaifunza jema na baya, na akaipa uweza wa kutenda itakayo
katika hayo,
9. Hakika amefuzu mwenye kuisafisha nafsi yake kwa ut'iifu na
vitendo vya kheri.
10. Na hakika amekhasiri mwenye kuzificha fadhila zake, na
akayaua matayarisho aliyo umbwa nayo ya kutenda kheri.
11,12. Kina Thamudi walimkanusha Nabii wao kwa
upotovu wao na jeuri zao, alipo gutuka mwovu wao mkubwa kabisa kutaka kumchinja
ngamia.
13. Saleh, Mtume wa Mwenyezi Mungu, akawaambia: Mwachilieni
huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ale maridhawa katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na
tahadharini msimzuie maji katika siku yake aliyo wekewa.
14. Wakamkadhibisha Mtume wao katika hilo onyo lake,
wakamchinja. Mola wao Mlezi akazibomoa nyumba zao kwa sababu ya dhambi zao;
akazisawazisha na ardhi!
15. Wala Yeye Mwenyezi Mungu hakhofu matokeo ya adhabu hiyo, kwani hiyo ni malipo ya haki kwa yale waliyo yatenda.