1. Naapa kiapo cha mkazo kwa mji wa Makka, mji mtakatifu;

 

2. Na wewe unaishi katika mji huu, unauzidisha utukufu wake na cheo chake.

 

3. Na naapa kwa mzazi na anacho kizaa, na kwa hao wawili ndio jinsi inahifadhika na maendeleo yanabakia.

 

4. Hakika Sisi tumemuumba mtu katika mashaka na taabu tangu mwanzo wake mpaka kumalizika mambo yake.

 

5. Je! Anadhani mtu aliye umbwa katika mashaka haya kuwa hapana awezae kumdhalilisha?

 

6. Anasema: Nimetumia katika kupambana na Muhammad s.a.w. na kuupinga wito wake mali mengi ukiyakusanya pamoja.

 

7. Ati anadhani kwamba mambo yake hayo yamefichikana, hayajui yeyote hata huyo aliye muumba?

 

8,9. Kwani Sisi hatukumuumba na macho mawili ya kutazamia, na ulimi na midomo miwili ili aweze kutamka na kusema sawa?

 

10. Na tukamwonyesha njia ya kheri na ya shari, na tukamtengenezea aweze kuchagua mojawapo?

 

11. Basi huyo hakunafiika kwa tuliyo mtengenezea, wala hakuivuka njia ya milimani inayo mzuia asifikie uwokovu, nayo ni choyo wa nafsi yake.

 

12. Na kitu gani kitakufunza nini huko kujitoma kwenye njia ya milimani?

 

13. Kumkomboa mtu kutokana na utumwa,

 

14. Au kumlisha siku ya njaa

 

15. Yatima aliye jamaa wa kumliwaza kwa ujamaa na ufakiri.

 

16. Au masikini mwingi wa haja na kufakirika.

 

17. Tena awe pamoja na hayo miongoni mwa wenye Imani wanao usiana na wenzao kwa subira na kuoneana huruma.

 

18. Hao wanao sifika kwa sifa hizi, ndio watu wa kheri, wa mkono wa kulia.

 

19. Na walio zikataa dalili tulizo zisimamisha kuthibitisha Haki kutoka na Kitabu na hoja zake, hao ndio wapotovu watu waovu walio kosa kheri na watapata adhabu.

 

20. Juu yao utakuwa Moto ulio bebeana na milango yake ikafungwa.