1. Naapa kwa mwangaza wa asubuhi unapo ufukuza usiku.

 

2. Na kwa masiku kumi yaliyo tukuzwa na Mwenyezi Mungu. (Na hayo ni masiku kumi ya mwanzo wa Mwezi wa Alhaj, Mfungo Tatu).

 

3. Na shafi' yaani hisabu inayo gawika kwa mbili, kama 4, 6, 8 n.k. na witri, yaani isiyo gawika kwa mbili, kama 1, 3, 5 n.k. katika kila kitu.

 

4. Na kwa usiku unapo pita kwa kwenda ulimwengu kwa namna ya ajabu.

 

5. Je! Katika vitu vilivyo tajwa vinavyo onekana kwa akili hapana kiapo cha kukinaisha?

 

6,7. Kwani hujui jinsi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake kaumu ya Hud, watu wa Iram wenye majengo marefu?

 

8. Ambayo haikupata kujengwa mfano wake kwa umadhubuti na ujenzi katika nchi.

 

9. Kwani hukujua jinsi Mola wako Mlezi alivyo teremsha adhabu yake kwa Thamudi, kaumu ya Saleh, walio chonga majabali kujengea nyumba zao huko bondeni?

 

10. Au kwani hukujua vipi Mola wako Mlezi alivyo wateremshia adhabu yake Firauni mwenye majeshi yaliyo upa nguvu ufalme wake kama vigingi vinavyo simamisha makhema?

 

11. Ambao walipita mipaka katika nchi?

 

12. Na wakazidisha kufanya uharibifu kwa ukafiri na udhalimu?

 

13. Basi Mola wako Mlezi aliwateremshia adhabu kali ya kuwaunguza.

 

14. Hakika Mola wako Mlezi anaviangalia vitendo vya watu, na anawahisabia, na atakuja kuwalipa kwavyo.

 

15. Ama mtu akijaribiwa na Mola wake Mlezi na akamkirimu, na akamneemesha kwa mali na cheo na nguvu, basi husema kwa kughurika na hayo: Mola wangu Mlezi amenitukuza kwa kuwa ninastahiki haya!

 

16. Na pindi Mola wake Mlezi akimjaribu mtu kwa kumdhikisha riziki, basi hughafilika na hikima ya hayo na husema: Mola wangu Mlezi kanidhalilisha!

 

17. Wacheni mtindo huo! Mambo siyo hayo kama msemavyo; bali nyinyi hamumkirimu yatima;

 

18. Wala hamhimizani kuwalisha masikini;

 

19. Na mnakula mali ya urithi kwa pupa, hamchagui linalo faa na lisilo faa.

 

20. Na mnayapenda mali mno, yanayo kupelekeeni kupapatika katika kuyakusanya na ubakhili wa kuyatumia.

 

21. Wacheni vitendo hivyo! Kwani inakungojeeni siku itapo lazwa ardhi iwe sawa sawa,

 

22. Na aje Mola wako Mlezi kama anavyo stahiki kuja kwake Subhanahu na Malaika waje kwa safu safu;

 

23. Na siku hiyo iletwe Jahannamu, nyumba ya adhabu,  siku hiyo yatapo tokea hayo mwanaadamu atakumbuka aliyo yaharibu - lakini wapi! Kukumbuka huko kumfae nini, na wakati umekwisha pita?

 

24. Atasema kwa majuto: Laiti ningeli jitangulizia katika dunia vitendo vyema vya kunifaa katika maisha ya Akhera!

 

25,26. Siku hiyo zitakuwa hali hizi, haadhibu mtu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hafungi mtu kama afungavyo Yeye.

 

27. Ewe nafsi uliye tulia juu ya Haki!

 

28. Rejea kwenye radhi ya Mola wako Mlezi nawe uradhi kwa neema ulio pewa, nawe umemridhisha kwa a'mali uliyo ikadimisha.

 

29. Basi ingia katika kundi la waja wangu walio wema!

 

30. Na ingia katika Pepo yangu, nyumba ya neema ya milele!