1. Je! Ewe Muhammad! Imepata kukujia hadithi ya Kiyama ambacho
kwa vitisho vyake kitawafanya watu wazimie?
2,3. Siku hiyo ya Kiyama zitakuwepo nyuso
zimedhalilika, zimechoka, taabani kwa shughuli na mashaka ya Motoni,
4. Zinaingia kwenye Moto unao waka kwa nguvu!
5. Wananywesha maji yanayo toka kwenye chemchem inayo tokota.
6. Hawana chakula ila chakula kiovu kabisa, anaadhibika mwenye
kukila.
7. Hakileti nafuu yoyote katika mwili, wala hakiondoi njaa.
8,9,10. Na pia zitakuwapo nyuso zenye
kutoa nuru Siku ya Kiyama, kwa malipo ya vitendo vyao walivyo fanya duniani. Hao
watakuwa wameridhia kwa watayo yapata katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.
11,12. Humo halisikilizani neno la upuuzi. Humo mna
chemchem isiyo katika.
13. Humo vitakuwamo viti vilivyo nyanyuliwa kwa cheo na kwa
hakika, kama ni ziada ya neema.
14. Na bilauri (gilasi) zilio wekwa mbele yao,
15. Na mito na matakia yalio pangwa kwa safu.
16. Na mazulia mengi yaliyo tandazwa hapo barazani.
17. Je! Wanapuuza kuzingatia Ishara, basi hebu na wamuangalie
ngamia, vipi alivyo umbwa kwa namna ya peke yake kwa uweza wa Mwenyezi Mungu?
Katika kuumbwa ngamia zipo Ishara na miujiza yenye kuthibitisha uweza wa
Mwenyezi Mungu ambao yafaa wenye kuzingatia wauzingatie. Katika sifa zake zinazo
onekana ni hizo zinazo mfanya kweli awe ni jahazi ya jangwani. Macho yake
yamenyanyuka yako juu ya kichwa, na yanaelekea nyuma, na tena yana kope za
kuyakinga na mchanga na vumbi. Kadhaalika pua na masikio yamefunikwa na nywele
kwa sababu hiyo hiyo. Ukivuma mdharuba wa mchanga pua hufunga na masikio
hupinda, juu ya kuwa tokea hapo ni madogo na si yenye kudhihiri mno,
ukilinganisha na mwili wake. Ama miguu ni mirefu kwa kusaidia wepesi wa kwenda,
pamoja na kunasibiana na urefu wa shingo yake. Ama nyayo ni pana zimetanda kwa
ukhafifu ili kumwezesha ngamia kwenda juu ya mchanga laini. Na ngamia kwa jumla
chini ya kifua chake na chini ya viungo vyake vya miguu pana kama mito inayo
msaidia ngamia kupiga magoti na kulala juu ya ardhi ngumu na imoto, kama vile
vile pande zote mbili za mkia wake yapo manyoya marefu ya kumlinda sehemu zake
za nyuma na vitu vya kumuudhi.
Ama vipawa alivyo pewa ngamia kwa
ajili ya kazi yake ni vya ajabu zaidi. Siku za baridi hahitajii maji, bali
anaweza asinywe maji muda wa miezi miwili mfululizo, ikiwa chakula kimajimaji na
laini, au wiki mbili ikiwa kikavu. Pia anaweza kustahamili kiu hata siku za joto
muda wa wiki au wiki mbili, na hupungua muda huo zaidi ya thuluthi mbili ya
uzito wake. Na anapo yapata maji huyagugumia maji kwa wingi mno arejeshe uzito
wake wa zamani kwa dakika chache tu. Na ngamia hayarimbiki maji katika tumbo
lake kama ilivyo kuwa ikidhaniwa, bali katika mfumo wa mwili wake, na huyatumia
kwa uangalifu mkubwa mno. Kwa hivyo kabisa hapumui kama anavyo pumua mbwa,
mathalan, wala hatoi pumzi kwa mdomo wake, wala hatoki majasho kwenye ngozi yake
ila kwa uchache kabisa. Na hayo ni kuwa daraja ya joto ya mwili wake inakuwa
chini sana asubuhi mapema. Kisha hupanda kidogo kidogo zaidi ya daraja sita
kabla ya kuhitajia kuipoza kwa jasho na kutoa mvuke. Na juu ya maji mengi mno
yanayo toka katika mwili baada ya kiu kirefu kwa hakika uzito wa damu
hauathiriki ila kwa kiasi tu, na kwa hivyo kiu hakina athari kitu juu yake. Na
imethibiti mafuta ya nunudu yaliyo khaziniwa kwa ajili ya nishat'i yanamkifu
kumkinga na machungu ya njaa, lakini hayamfaidishi sana kwa haja ya maji ambayo
ni lazima kwa mwili wake.
Na bado wataalamu wangali wanagundua mapya
katika ngamia kila wakichungua ya kuhakikisha hadhi aliyo mpa Mwenyezi Mungu
Mtukufu kuwa atazamwe katika uumbaji wake wa muujiza.
18. Na waizingatie mbingu wanayo iona daima, vipi ilivyo
nyanyuliwa huko mbali bila ya nguzo!
19. Na milima wanayo ikwea mpaka wakafika vileleni kwake, vipi
ilivyo simamishwa kwa urefu, imeshikamana na ardhi, haiyumbi wala haitikisiki!
Mara nyingi katika Qur'ani tukufu inatajwa kuwa ardhi "imekunjuliwa". Na
makusudio ya hayo ni kuwa ardhi ijapo kuwa ni duara kama mpira kwa sura yake,
lakini inavyo onekana kwa watazamao ni kuwa imekunjuliwa. Na haya hayagongani na
yaliyo thibitishwa na sayansi katika jambo lolote.
20. Na ardhi wanayo ikalia na kuyendea juu yake, vipi ilivyo
kunjuliwa na kutandazwa!
21,22 Basi kumbusha kwa wito wako, kwani kazi yako
muhimu ni kufikisha wito tu. Hukuwa mtawala juu yao.
23,24 Lakini miongoni mwao ataye puuza na akakataa,
basi Mwenyezi Mungu atampa adhabu iliyo kubwa kabisa, isiyo kuwa na ya kuipita.
25. Hakika ni kwetu Sisi marejeo yao kwa kifo na kufufuliwa,
wala hapana penginepo isipo kuwa kwetu.
26. Tena ni juu yetu Sisi tu peke yetu kuwahisabia na kuwalipa.