1. Litakase jina la Mola wako Mlezi lilio tukufu na kila kitu
kisicho kuwa kinaelekeana nalo.
2. Aliye umba kila kitu, na akajaalia uumbaji wote sawa sawa
katika hukumu na kupangana.
3. Na akakadiria kwa kila kitu kwa mujibu wa maslaha yake, na
akakiongoza.
4. Na ambaye akatoa kwenye ardhi mimea namna mbali mbali ya
kuwalisha wanyama.
5. Na akaifanya mimea hiyo baada ya kuwa kijani imestawi,
ikakauka na imekuwa myeusi!
6. Ewe Muhammad! Sisi tutakujaalia uwe ni mwenye kuisoma
Qur'ani kwa ufunuo kutoka kwetu, na wala hutosahau utacho kihifadhi.
7. Isipo kuwa anacho taka Mwenyezi Mungu ukisahau, kwani hakika
Yeye Mtukufu anayajua wanayo yadhihirisha waja wake na wanayo yaficha, ikiwa
maneno au vitendo.
8. Na tutakuwezesha kupita njia ya kufikilia kwa wepesi mambo
yako yote.
9. Basi wakumbushe watu ikiwa kukumbusha kutaleta manufaa,
kwani inavyo faa ndio kuwanafiisha.
10. Watanafiika kwa ukumbusho wako wanao mwogopa Mwenyezi
Mungu.
11. Na atajitenga na ukumbusho mpotovu anaye shikilia kufanya
inda na ukafiri.
12. Ambaye ataingia kwenye Moto mkubwa ulio andaliwa kuwa ndio
malipo yake.
13. Tena hatokufa huko Motoni akapumzika kwa kifo, wala hawi
hai kwa uhai wa kustarehe nao.
14. Hakika amefuzu mwenye kujisafisha na ukafiri na maasi.
15. Na akalikumbuka jina la Muumba wake kwa moyo wake na ulimi
wake, na akasali kwa unyenyekevu kama itakikanavyo.
16. Bali nyinyi hamfanyi hayo yanayo pelekea kufanikiwa,
lakini katika hima zenu mnatanguliza maisha ya duniani kuliko ya Akhera.
17. Na Akhera ni bora kuliko dunia, kwa usafi wa neema zake, na ni yenye kubaki na kudumu zaidi.
18,19. Hakika haya yote yaliyo tajwa katika Sura hii bila ya shaka yamethibitishwa katika Vitabu vya zamani, Vitabu vya Ibrahimu na Musa; kwani haya yamewafikiana na mafunzo ya dini zote na yamesajiliwa katika Vitabu vya mbinguni.