1. Naapa kwa mbingu na nyota inayo tokeza usiku!
2,3. Na kitu gani kitakujuvya ukweli wa nyota hii? Ni
hiyo inayotoa mwanga wake katika giza.
4. Hapana nafsi ila inayo mlinzi wa kuiangalia na kudhibiti
vitendo vyake.
5. Basi naafikiri mtu, yeye kaumbwa kutokana na nini?
6. Ameumbwa mtu kutokana na maji yanayo toka kwa nguvu.
7. Maji haya yanatoka baina ya uti wa mgongo na mbavu za
mwanamume na mwanamke.
S'ULB ni sehemu za uti wa mgongo; na TARAAIB
ni mafupa ya vifua, yaani mbavu. Masomo ya watoto wanapo kuwa ndani ya matumbo
ya mama zao (Embryology). yamedhihirisha kuwa viini vya vyombo vya uzazi na
mkojo katika mtoto ndani ya tumbo la mama yake vinadhihiri baina ya khalaya
(cells) za mishipa itakayo kuwa mafupa ya uti wa mgongo, na baina ya khalaya
zitakazo kuwa mafupa ya kifua.
Mafigo hubakia pahala pake, na kokwa
huteremka kwenye pahala pake pa kawaida katika pumbu wakati wa kuzaliwa. Na juu
ya kuteremka kokwa chini mishipa inayo inywesha damu maisha yake yote inatokana
na mishipa ya mafigo.
Hali kadhaalika mishipa ya Navo inayo peleka
kuhisi na ikasaidia kuzalisha vitu vya uhai na yaliyo khusiana na hayo kama maji
yanayo toka kwenye mshipa wa kifua wa kumi unao tokana na ubongo wa uti wa
mgongo kwenye kipingili cha kumi na kumi na moja.
Yaliyo wazi
kutokana na hayo ni kwamba vyombo vya uzazi na vinavyo lisha vyombo hivyo, na
vyombo vya damu, vipo katika kiwiliwili baina ya uti wa mgongo na mbavu.
8. Hakika Mwenyezi Mungu aliye muumba hivi hapo mwanzo, bila ya
shaka ni Muweza wa kumuumba tena baada ya kufa kwake.
9. Siku dhamiri zitapo fanyiwa mtihani, na zitengwe mbali mbali
baina ya ziliyo kuwa nzuri na ziliyo kuwa mbovu.
10. Basi hapana mtu wakati huo ataye kuwa na nguvu ya
kujikinga nafsi yake, wala hatakuwa na msaidizi wa kumnusuru.
11. Naapa kwa mbingu yenye mvua inayo rejea na kuja mara kwa
mara!
12. Na ardhi inayo pasuka kwa kuchipuka mimea!
13,14. Hakika hii Qur'ani ni yenye kupambanua baina
ya kweli na uwongo. Wala haina nuksani yoyote ya mchezo au maskhara.
15. Hakika hao wanao ikadhibisha Qur'ani wanaipangia njama
kutaka kuiharibia, njama zenye kufikia ukomo!
16. Lakini Mimi nitawalipa, na nitavipambanisha hivyo vitimbi
vyao kwa vitimbi madhubuti ambavyo hawataweza kujikinga navyo.
17. Basi wangojee hao makafiri! Wape muhula wa karibu mpaka nikuamrishe amri gani kali ya kuwatendea.