1. Naapa kwa mbingu yenye Buruj au Manaazil, njia au vituo
ambavyo nyota hupitia katika nyendo zake,
Buruuj au Manaazil ndio
huu mkusanyiko wa nyota unao onekana kwa sura namna mbali mbali mbinguni. Hizo
Buruuj zimegawika sehemu kumi na mbili ambazo ardhi inazipitia inapo lizunguka
jua.
2. Na kwa Siku iliyo ahidiwa kuwa ndiyo Siku ya Hisabu na
Malipo,
3. Na kwa viumbe watao hudhuria Siku hiyo wakaona vitisho na
ajabu zitakazo kuwepo,
4. Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani watu walio chimba khandaki
katika ardhi,
5. Wakawasha moto kuwatumbukiza ndani yake Waumini ili
kuwatesa,
6. Na wao wamekaa ukingoni mwake wakishuhudia mateso yanayo
wapata Waumini.
7. Na wao wapo hapo wamehudhuria kwenye mateso wanayo watendea
Waumini.
8. Na hapana walilo lichukia kwa hao Waumini ila ni kuwa
wakimuamini Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu ambaye adhabu yake huogopwa, Msifiwa
anaye tarajiwa thawabu zake.
9. Ambaye, peke yake, ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi.
Na Mwenyezi Mungu ni shahidi anashuhudia yote wayatendayo Waumini na makafiri na
atawalipa kwayo.
10. Hakika walio watia matatani Waumini wanaume na Waumini
wanawake kwa maudhi na kuwaadhibu kwa moto, kisha wasitubu na kurejea nyuma
watapata Akhera adhabu ya Jahannamu kwa ukafiri wao, na watapata adhabu ya
kuunguzwa kwa kule kuwaunguza moto Waumini.
11. Hakika hao walio kusanya kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu
vitendo vyema watapata Mabustani yapitayo mito kati yake. Neema hiyo waliyo
lipwa ni kufuzu kukubwa.
12. Hakika mshiko wa Mola wako Mlezi kuwashika majabari
umefika ukomo kwa ukali wake
13. Ni Yeye peke yake ndiye Mwenye kuanza kuumba, na kisha ni
Yeye anaye rejeza tena,
14. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha kwa mwenye kutubu na
akarejea, na Mwingi wa mapenzi kwa mwenye kumpenda na akamt'ii.
15. Yeye ndiye Mwenye Kiti cha Enzi na Mwenye kukimiliki, na
Mkuu kwa dhati yake na sifa zake.
16. Ni Mtendaji kwa alitakalo, na hendi kinyume na uweza wake
yeyote anaye taka.
17. Je! Imekujia, ewe Muhammad, hadithi ya kile kikundi
kilicho a'si katika mataifa yaliyo kwisha pita?
18. Kaumu ya Firauni na Thamudi na yaliyo washukia katika
malipo ya kushikilia kwao upotovu?
19. Bali hao makafiri katika kaumu yako ni shadidi zaidi
katika kukukadhibisha kuliko hawa walivyo wakadhibisha Mitume wao.
20. Na Mwenyezi Mungu anawaweza hao, na anawajua vilivyo.
21. Bali hii ulio waletea ni Qur'ani tukufu inadhihirisha hoja
za ukweli wako.
22. Imo katika Ubao Ulio Hifadhiwa, hapana uwezo unao weza kuipotoa au kuigeuza.