1. Mbingu itapo chanika, ikaamrishwa iondoke,

 

2. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi na ikamt'ii, na ndio maelekeo yake isikie na kut'ii,

 

3. Na ardhi ikazidi upana wake kwa kulazwa milima na kuondolewa kifusi chake,

 

4. Na ardhi ikatoa nje maiti na khazina ziliyo kuwamo ndani yake, na ikaachana navyo vyote hivyo,

 

5. Na ikamwelekea Mola wake Mlezi kwa kuzidi kutanuka kwake na kutoa vilio kuwemo ndani yake na kuachana navyo, na hayo ni haki yake kuwa. Yakitokea yote hayo yaliyo tangulia kusimuliwa basi kila mtu atapata malipo ya vitendo vyake.

 

6. Ewe mtu! Hakika wewe unafanya juhudi katika vitendo vyako vikufikishie lengo lako. Basi utakuja kukutana na Mola wako Mlezi kwa a'mali yako, naye atakulipa kwayo.

 

7,8,9. Ama mwenye kupewa daftari la vitendo vyake kwa mkono wake wa kulia basi atahisabiwa kwa hisabu nyepesi, na atarejea kwa jamaa zake Waumini naye furahani.

 

10,11,12. Ama mwenye kupewa daftari lake kwa mkono wa kushoto wake nyuma ya mgongo wake kwa kudharauliwa shani yake, huyo atatamani ajiue, na ataingia Motoni aungulie mbali!

 

13. Kwani huyo hakika duniani alikuwa furahani kati ya jamaa zake akitanaamu na pumbao alilo kuwa nalo hata akapuuza a'mali ya kuitenda kwa mustakabali wake.

 

14. Hakika huyo alidhani kuwa kabisa hatorejea kwa Mwenyezi Mungu akamhisabu.

 

15. Bali atarejea, na atahisabiwa! Kwani Mola wake Mlezi alikuwa anamwona vyema yeye na vitendo vyake.

 

16. Basi naapa kiapo cha mkazo kwa wekundu wa mbingu baada ya kuchwa jua!

 

17. Na kwa usiku na unavyo vikusanya vyote katika giza lake, wanaadamu, wanyama na vyenginevyo!

 

18,19. Na mwezi unapo kamilika kupevuka na kutimia nuru yake, hapana shaka yoyote mtakutana na hali baada ya hali, baadhi yake zina shida zaidi kuliko nyenginezo, za kufa na kufufuliwa na vitisho vya Kiyama.

 

20. Wana nini hawa makafiri yanayo wazuia wasimuamini Mwenyezi Mungu na kufufuliwa baada ya kuwekwa wazi dalili zake zote za kuwajibika kwake?

 

21. Na pindi wakizisikia Aya za Qur'ani hawasujudu wakanyenyekea?

 

22. Bali watu hawa, kwa ukafiri wao, wanakanusha kwa inadi na kutakabari kuikataa Haki!

 

23. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kabisa hayo wanayo yadhamiria katika nyoyo zao.

 

24. Basi wabashirie, kwa kejeli,  kuwa watapata adhabu ya kutia uchungu.

 

25. Lakini walio amini na wakatenda mema watapata, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ujira usio wakatikia na wala usio kuwa na hisabu juu yao.