1,2,3. Wataangamia wanao punja, ambao
wakijipimia wenyewe kwa watu hujitwalia ya kutosha na kuzidi, na wakiwapimia
watu kwa vipimo au mizani huwapunguzia haki yao wanayo stahiki, kwa dhulma!
4,5. Hivyo haiwapitikii katika akili zao hawa wanao
punja wenzao kwamba watakuja fufuliwa katika siku ya vitisho vikuu?
6. Siku watapo simama watu kwa amri ya Mola Mlezi wa walimwengu
wote na hukumu yake?
7. Wacheni kupunja, na kughafilika na kufufuliwa! Kwani
hakika waliyo andikiwa wakosefu katika a'mali zao mbovu, bila ya shaka yamo
katika Sijjin.
8. Na nini kitakujuvya nini hiyo Sijjin?
9. Hicho ni Kitabu kilicho pigwa mistari baina ya maandishi
yake.
10. Wataangamia wanao kadhibisha siku itapo kuwa kufufuliwa na
kuhisabiwa.
11. Ambao wanaikanusha Siku ya Malipo.
12. Na wala haikanushi Siku ya Malipo ila kila mwenye
kupindukia mipaka mwingi wa madhambi.
13. Na akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu zenye kutaja kuwepo
malipo husema: Huo ni uwongo wa walio tangulia!
14. Ewe uliye kiuka mipaka! Wacha kauli hiyo potovu. Bali
nyoyo za wenye kupindukia mipaka imegubikwa na ukafiri na maasi waliyo yatenda.
15. Hakika ni kweli kuwa hao wanao kadhibisha watazuiliwa siku
hiyo rehema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya maasi waliyo yachuma.
16. Kisha hakika hao bila ya shaka wataingia Motoni.
17. Kisha wataambiwa kwa kuwakebehi: Hii basi ndiyo adhabu
inayo kuteremkieni ambayo mlikuwa mkiikanusha duniani!
18. Ni hakika kuwa vitendo vya watu wema bila ya shaka
vimeandikwa katika I'liyyin.
19. Na nini cha kukujuvya nini I'liyyin?
20,21. Hicho ni Kitabu kilicho andikwa wazi
maandishi yake, wanakihudhurisha na kukihifadhi Malaika walio kurubishwa.
22,23. Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa
katika neema za Peponi, juu ya viti vya enzi, wakiziangalia neema na
ukarimu alio wakirimu Mwenyezi Mungu.
24. Utaona katika nyuso zao uchangamfu na mng'aro wa neema.
25,26. Wakinyweshwa kinywaji safi kilicho
hifadhiwa; kuhifadhiwa huko hakukuzidisha ila uzuri wake. Na kupata neema hizo,
basi, na washindanie wanao shindana.
27,28. Cha kuchanganyia kinywaji hicho ni maji ya
Tasniim ya Peponi, nayo ni chemchem wanao inywa walio kurubishwa si wengineo,
katika watu wa Peponi.
29. Wale walio kuwa wakibeba madhambi kuipingia Dini walikuwa
wakiwacheka kuwakejeli Waumini duniani.
30. Na wakipita Waumini mbele yao basi wao hukonyezana kwa
kuwabeza.
31. Na hao wakosefu wakirejea kwa ahali zao hurejea kwa furaha
na kuona ladha kwa vile kuwakejeli Waumini.
32,33. Na wakiwaona Waumini husema: Ama hakika hawa
wamepotea kweli kwa kumuamini Muhammad. Wala hao wakosefu hawakutumwa wawe wa
kuwahukumu Waumini kwa kuwaongoza au kuwapoteza, wala kuwa ni walinzi wa vitendo
vyao.
34. Basi Siku ya Malipo walio amini watakuwa ndio wa kuwacheka
hao makafiri kwa kuwalipizia kile kicheko chao na kejeli yao ya duniani.
35. Ilhali wako juu ya vitanda na matakia watakuwa Waumini
wakiziangalia neema za Mwenyezi Mungu alizo wapa.
36. Je! Makafiri watalipwa huko Akhera kwa waliyo yatenda duniani?