1. Jua litakapo kunjwa na mwangaza wake ukafutwa,

 

2. Na nyota ikazimwa nuru yao,

 

3. Na milima ikaondoshwa hapo ilipo,

 

4. Na ambao wa kuchukua mimba wakaharibu mimba zao,

 

5. Na nyama mwitu wakusanywe kutoka vichakani mwao na mashimoni mwao, hawajijui hawajitambui kwa wingi wa kufazaika.

 

6. Na bahari zikawa zinawaka moto,

 

7. Na roho zikaunganishwa na viwiliwili vyao,

 

8,9. Na mtoto wa kike aliye zikwa hai, akaulizwa kwa kumliwaza yeye, na kumshutumu aliye mzika hai, kwa makosa gani kauliwa, naye hana dhambi? (Ilikuwa ada ya makafiri wa Kiarabu kabla ya Uislamu kuwazika watoto wao wa kike nao wahai!  Baadhi ya Mabaniani wanawauwa watoto wao wa kike hata hivi leo huko India!!)

 

10. Na nyaraka zilizo andikwa ndani vitendo vya watu zikakunjuliwa wakati wa hisabu.

 

11. Na mbingu itapo ondoshwa pahala pake,

 

12. Na Moto ukawashwa kwa mwako mkali,

 

13. Na Pepo ikajongezwa ikawa karibu,

 

14. Yatakapo tokea yote hayo, basi hapo tena kila nafsi itajua nini iliyo tanguliza, ikiwa kheri au shari.

 

15. Naapa kiapo cha mkazo kwa nyota ambazo zinanywea zinapo chomoza, na hapo mwanga wake huwa khafifu,

 

16. Zenye kwenda na hujificha wakati wa kuchwa kwake, kama paa wanapo jificha kwenye mapango yao.

 

17. Na kwa usiku linapo pungua giza lake wakati unapo malizika.

 

18. Na kwa asubuhi unapo anza mwangaza wake na ukavuma upepo wake,

 

19. Hakika Qur'ani bila ya shaka ni kauli ya Mjumbe anaye toka kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwenye kuhishimiwa kwake,

 

20. Mwenye nguvu katika kutekeleza waajibu wake, mwenye cheo na daraja mbele ya Mwenyezi Mungu Mwenye Kiti cha Enzi.

 

21. Tena ni mwenye kut'iiwa, na muaminifu wa kuchukua wahyi miongoni wa walio juu.

 

22. Na huyo Mtume wenu ambaye ni mwenzenu, mnaye mjua kuwa ana akili timamu, si mwendawazimu.

 

23. Na ninaapa kuwa Muhammad s.a.w. bila ya shaka alimwona Jibrili katika upeo wa macho kwa mujibu wa inavyo onekana.

 

24. Na Muhammad si bakhili wa kufikisha wahyi na kuwafunza watu.

 

25. Wala huu wahyi (ufunuo) ulio teremshwa juu yake si kauli ya Shetani aliye fukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.

 

26. Basi njia gani iliyo ya uwongofu zaidi kuliko hii mnayo ifuata?

 

27. Qur'ani si chochote ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.

 

28. Kwa anaye taka, miongoni mwenu, kusimama sawa kufikilia haki na kweli.

 

29. Na nyinyi hamwezi kutaka kitu ila anapo taka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.