1. Uso wake ulitaghayari kwa kuchukia na akageuka,

 

2. Kwa sababu kamjia kipofu anamuuliza khabari ya Dini yake.

 

3. Na wewe unajuaje, pengine huyo kipofu atatakasika kwa atayo yapata kwako,

 

4. Au atawaidhika na mawaidha yamfae.

 

5,6. Ama yule anaye jiona ametosheka kwa mali yake na nguvu zake, wewe ndio unamkabili na unamshughulikia kumfikishia wito wako.

 

7. Na wewe una lawama gani ikiwa yeye hakutakasika kwa Imani?

 

8,9,10. Ama anaye kukimbilia kutafuta ilimu na uwongofu, naye anamkhofu Mwenyezi Mungu wewe unampuuza.

 

11. Hakika Aya hizi ni mawaidha.

 

12. Mwenye kutaka atawaidhika kwa Qur'ani.

 

13. Nayo Qur'ani imo katika kurasa zilizo tukuzwa kwa Mwenyezi Mungu,

 

14. Zina cheo cha juu, na pahala palipo tukuka, zimetakasika na kila upungufu.

 

15. Katika mikono ya Malaika ambao Mwenyezi Mungu amewafanya ndio mabalozi baina yake na Mitume wake;

 

16. Walio bora, wema.

 

17. Ameangamia mwanaadamu! Nini kilicho mfanya akufuru na hali Mwenyezi Mungu amemfanyia hisani zote hizi?

 

18. Hakumbuki yeye kaumbwa kutokana na nini?

 

19. Kutokana na maji ya kudharauliwa Yeye  Mwenyezi Mungu alimwanzisha kumuumba akamjaalia apitie daraja mbali mbali za kukua.

 

20. Kisha akamfanyia nyepesi njia ya kufikia Imani, na akamfunza njia hiyo.

 

21. Kisha akamfisha na akamtukuza kwa kumtia kaburini.

 

22. Na tena akipenda atamhuisha baada ya kufa kwake.

 

23. Ni kweli mwanaadamu, juu ya kuwa umri wake mrefu duniani, hakutimiza aliyo amrishwa na Mwenyezi Mungu katika mambo ya Imani na ut'iifu.

 

24. Hebu mtu na aangalie shani ya chakula chake - vipi tulivyo kipanga na kumsahilishia!

 

25. Ni Sisi tumeiteremsha mvua kutoka mbinguni, ikateremka.

 

26. Tena tukaipasua pasua ardhi kwa ajili ya mimea.

 

27. Tukaotesha humo nafaka ambazo watu huzila na huweka akiba.

 

28. Na mizabibu na mimea ya majani inayo liwa mibichi.

 

29. Na mizaituni mizuri, na mitende yenye kuzaa,

 

30. Na mabustani yaliyo songamana matawi ya miti yake,

 

31. Na matunda ya kustaladhi nayo, na malisha ya kula nyama hoa (mifugo).

 

32. Tumeotesha yote hayo kwa ajili ya faida yenu na wanyama wenu wa kufuga.

 

33. Basi utakapo kuja ukelele wa Kiyama utakao tia uziwi masikio,

 

34,35,36. Siku mtu atakapo mkimbia ndugu yake, na mama yake, na baba yake, na mkewe, na wanawe!

 

37. Kila mmojapo katika hawa atakuwa na jambo lake la kumshughulisha!

 

38,39. Zipo nyuso siku hii zenye mwangaza, zenye kung'ara na kufurahi kwa neema za Mwenyezi Mungu.

 

40. Na nyuso nyengine siku hii zina vumbi zimesawijika.

 

41. Zimegubikwa na kiza na weusi.

 

42. Wenye nyuso hizi ni makafiri wapotovu, ambao walio kuwa hawabali maasi waliyo kuwa wakiyatenda.