1. Ninaapa kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuving'oa vitu
kutokana na pahala pao kwa nguvu,
2. Na kwa kila kilicho pewa uwezo wa kuvitoa vitu kwa utaratibu
na ulaini,
3. Na kwa kila kilicho pewa mbio za kutekeleza kazi yake kwa
sahala na wepesi.
4. Na kwa vinavyo shindania kutimiza waajibu ulio twikwa juu
yao kushindania kwa juhudi,
5,6,7. Na vinavyo dabiri, kupanga, mambo na
kuyaendesha kwa mujibu wa vilivyo khusishwa, bila ya shaka Saa ya Kiyama
itafika; hiyo siku ambayo mpulizo wa mwanzo wa barugumu utavitikisa viumbe
vyote, na mpulizo huo utafuatiwa na wa pili ambao ndio utakao kuwa wa kufufuliwa
watu.
8. Siku hiyo nyoyo zitapapatika kwa khofu.
9. Macho ya watu yatakuwa na huzuni, manyonge.
10. Watu hawa husema duniani kwa kukanya kufufuliwa: Ati
tutarudishwa sisi baada ya kwisha kufa, tuumbwe tena kama tulivyo kuwa?
11. Tukisha kuwa mafupa yaliyo chakaa, ati tutarejeshwa
tufufuliwe upya?
12. Wanasema, kwa kukanya na kejeli: Kurejea huko kama
kukitokea basi ni marejeo ya khasara, na sisi si watu wa kukhasiri.
13,14. Msidhani kurejea huko ni kuzito. Kwani hayo
ni ukelele mmoja tu, mara maiti wote watahudhurishwa kwenye ardhi ya mkusanyiko!
15,16. Ewe Muhammad! Imekufikilia hadithi ya Musa,
alipo mwita Mola wake Mlezi katika bonde lilio takaswa, linalo itwa "T'uwa"?
17. Akaambiwa: Nenda kwa Firauni aliye pindukia mpaka katika
udhalimu.
18. Umwambie: Je! Huelekei kut'ahirika?
19. Na mimi nikuongoze upate kumjua Mola wako Mlezi, umwogope.
20. Musa akamwonyesha Firauni miujiza mikubwa.
21. Lakini Firauni alimkadhibisha Musa kwa aliyo kuja nayo, na
akamuasi kwa aliyo mwitia.
22. Kisha akamgeuzia mgongo, akenda kujitahidi kumpinga.
23,24. Akawakusanya wachawi, na akawaita watu,
akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa.
25. Mwenyezi Mungu akampa adhabu kwa kauli yake ya mwisho,
nayo ni vile kusema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa. Na akampa
adhabu kwa kauli yake ya mwanzo, nayo ni kumkadhibisha Musa a.s.
26. Hakika katika hadithi hiyo yapo mawaidha kwa mwenye
kumkhofu Mwenyezi Mungu.
27,28. Enyi mnao kanya kufufuliwa! Kukuumbeni
nyinyi ni taabu zaidi au kuziumba mbingu, kuzikusanya sehemu zake zilio
tawanyika mbali mbali, na kunyanyua kimo chake, na zikakaa sawa hazina tafauti
wala ila?
29. Na akatia kiza katika usiku wake, na akautokeza mchana
wake ukawa na mwangaza?
30. Na ardhi baada ya hayo akaikunjua, na akaisawazisha,
ikasilihi kukaliwa na watu wake?
31. Akatoa ndani yake maji yake yanayo tibuka katika chemchem
zake, na ikamiminika mito yake, na ikawa na mimea yake ya chakula kwa ajili ya
watu na wanyama;
32. Na milima akaithibitisha imara
33. Kwa ajili ya manufaa yenu na wanyama wenu mnao wafuga!
34. Kitakapo fika Kiyama ambacho vitisho vyake vitaenea kote,
35. Siku atakapo kumbuka mtu vitendo vyake vya kheri au shari,
36. Na Jahannamu ikadhihirishwa wazi, akaiona kila mwenye
macho kuwa ndio malipo,
37,38,39. Basi ama mwenye kupita mpaka
kwa maasi yake, na akajichagulia nafsi yake maisha yanayo pita njia, basi Moto
wa Jahannamu unao babua upepo wake ndio makaazi yake wala hana mengineyo.
40,41. Na ama mwenye kukhofu ukubwa na utukufu wa
Mola wake Mlezi, na akaizuia nafsi yake na matamanio ya kumpumbaza, basi huyo
nyumba ya neema ya Peponi ndio makaazi yake, wala hana penginepo.
42. Ewe Muhammad! Wanakuuliza, ati, khabari za Saa ya Kiyama,
itakuwa lini?
43. Ujuzi wa hayo hauko kwako hata uwatajie.
44. Ujuzi wa hayo uko kwa Mola wako Mlezi tu, si kwa
mwenginewe. (Nabii Isa a.s. ambaye Wakristo wanasema ni Mwana wa Mungu, au ndiye
Mungu, pia anasimuliwa katika Biblia kuwa hakuijua Saa na Siku ya Kiyama. Injili
ya Mathayo 24.36 inanukulu maneno ya Yesu: "Walakini habari ya siku ile na saa
ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke
yake.")
45. Kwani waajibu wako ni kuwaonya wanao khofu si kuwatangazia
wakati wake.
46. Na wao siku watakayo iona hiyo Saa ya Kiyama ni kama kwamba hawakuishi duniani zaidi kuliko jioni moja tu, au mchana wake.