1. Wanaulizana nini hao makafiri?
2,3. Wanaulizana khabari kubwa, khabari ya
kufufuliwa, ambayo wao wamezama ndani yake kukhitalifiana baina ya wenye
kuikataa na wenye kuitilia shaka.
4. Kuwazuia kuulizana huko wanaambiwa kuwa watakuja ujua ukweli
wa mambo hapo watapo ona kufufuliwa kumetokea khasa.
5. Tena kuwazuia, watakuja jua itapo wateremkia adhabu.
6. Kwani wao hawaoni Ishara za uweza wetu kwamba Sisi
tumeifanya ardhi imetandikwa upatikane utulivu juu yake na iwezekane kutembea
juu yake?
7. Na tukaifanya milima ni vigingi vya ardhi vya kuituliza?
Sehemu ya gamba gumu lilio juu ya ardhi linfikilia kiasi ya kilomita 60
unene wake, na inazidi mikunjo, mifimbi, inapanda juu kuwa milima, na huteremka
chini kuwa ni vina vya bahari; na hiyo hulingana kwa sababu ya uzito unao
patikana kutokana na milima. Na kulingana huko hakuharibiki ila kwa kubugunyika,
kwani gamba kavu la ardhi linazuiliwa na milima, kama vigingi vinavyo zuilia
khema. (Rejea Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 7 ya Surat Qaf).
8. Na tukakuumbeni kwa jozi, wanaume na wanawake?
9. Na tukafanya kulala kwenu ni mapumziko ya machofu ya kazi?
Kulala usingizi ni kusita nishat'i ya sehemu ya ubongo yenye
kutambua na kuwa macho. Yaani gamba la ubongo, au kupunguka nishat'i yake kwa
wingi, ukilinganisha na daraja za nishat'i ya sehemu za viungo vilio baki. Na
kwa hivyo kunapunguka nguvu na joto la mwili, tena mwili hapo wakati wa usingizi
hupata kutua na kupumzika baada ya kuhangaika viungo au akili au vyote viwili.
Basi kazi za kimwili zote hupunguka isipo kuwa kazi za kusaga chakula, na
kupitisha mkojo katika mafigo, na kutoka majasho katika ngozi, kwani yakisita
hayo hupatikana madhara juu ya maisha ya mtu. Ama kuvuta pumzi huko nako
hupunguka, na huwa ni kwa ndani zaidi, na huwa kwa kifua zaidi kuliko kwa tumbo.
Na mpigo wa mishipa hupungua kasi kwa kunavyo tokana na moyo, na hudhoofika
mkazano wa musulo (muscular tension), na kwa hivyo huwa taabu kupata harakati za
kinyume. Na yote haya ni ili binaadamu apate kupumzika wakati wa kulala.
10. Na tumeufanya usiku ni sitara kwenu kwa kiza kinacho
kufunikeni.
11. Na tumeufanya mchana ni wakati wa kuhangaika kwenu
kutafuta cha kukusaidieni katika maisha yenu.
12. Na tumesimamisha juu yenu mbingu saba zenye nguvu
madhubuti.
13. Na Sisi tumeliumba jua lenye mwangaza na linalo waka.
Makusudio ya Assiraj Alwahhaaj, Taa yenye mwanga na joto, ni Jua.
Na hayo kama ilivyo thibiti katika sayansi kuwa daraja ya joto la uso wake
inafika daraja 6000. Ama kati yake daraja yake inazidi daraja 30 milioni
kwa sababu ya mdidimizo mkubwa unao patikana juu ya madda ziliomo ndani yake. Na
jua linatoa nishat'i hizi zifuatazo: 9 katika 100 ya miale ya Ultraviolet
rays, 46 katika 100 ya miale ya mwangaza, 45 katika 100 miale ya joto, au Infra
red rays. Na kwa hivyo hii Aya tukufu imeliita kuwa ni Taa yenye mwangaza na
joto.
14. Na tumeteremsha kutokana na mawingu yaliyo karibia
kunyesha maji yenye kumiminika kwa nguvu.
Mvua ndio kitu pekee kinacho
toka asli yake maji matamu katika ardhi. Na asli ya mvua ni kukusanyika
vijisehemu vya maji yanayo panda kutoka baharini, na maziwa na mito,
yakakusanyika kama mawingu na yakageuka chembe za mvua au vipande vya barafu, na
khatimaye yakaanguka kwa sura ya mvua au theluji.
15. Ili tutoe kwa maji haya nafaka na mimea kuwa ni chakula
kwa ajili ya watu na wanyama.
16. Na mabustani yenye miti iliyo fungamana na matawi yake
yameingiliana.
17. Hakika siku ya uamuzi baina ya viumbe imewekewa miadi ilio
kwisha kadiriwa kwa ajili ya kufufuliwa.
18. Siku litakapo pulizwa barugumu na kufufuliwa watu, mtakuja
kwenye mkutano makundi kwa makundi.
19. Na mbingu zitapasuliwa kila upande hata zitakuwa ni
milango milango.
20. Na milima itaondolewa baada ya kung'olewa mwahala mwake,
na kuvurugwa, ikawa unaiona kama sura ya milima na hali hiyo ni kifusi tu
kilicho rindikwa, kama uonavyo mangati, sarabi, unaona kama sura ya maji nayo si
maji.
21. Hakika Jahannamu imekuwa kama ni kitu kinacho ngojea,
walinzi wake wanawangojea watu watakao kuja kuingia.
22. Yawe ni marejeo na mafikio kwa wenye kupindukia mipaka ya
Mwenyezi Mungu.
23. Watakaa humo dahari baada ya dahari.
24. Hawataonja humo hata chembe ya upepo wa kuburudisha joto
lake, wala kinywaji cha kupoza kiu chao.
25. Lakini watakunywa maji yalio pita ukomo kwa umoto wake, na
usaha unao miminika kutokana na ngozi za watu wa Motoni.
26. Malipo ya kuwafikiana na vitendo vyao viovu.
27. Kwani hao hawakutaraji kuwa itakuwapo kuhisabiwa, hata
watende ya kuwaokoa humo.
28. Wakazikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye
kuthibitisha kufufuliwa kwa mkadhibisho mkali.
29. Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.
30. Basi onjeni, wala hampati kwetu ila kuzidishiwa adhabu tu.
31. Hakika wenye kumcha Mola wao Mlezi watapata kuokoka na
adhabu, na wataipata Pepo,
32. Na mabustani yenye matunda, na mizabibu mizuri,
33. Na wanawari walio watipwatipwa wa hirimu yao,
34. Na bilauri safi zilizo jaa pomoni,
35. Hawasikii huko Peponi upuuzi wala uwongo.
36. Ni malipo kutokana na Mola wako Mlezi, kwa fadhila yake na
ihsani ya kutosha.
37. Mola Mlezi wa mbinguni na duniani na vilio baina yao,
ambaye rehema yake imeenea juu ya kila kitu. Hapana yeyote mwenye madaraka ya
kusema mbele yake.
38. Siku atakapo simama Jibrili na Malaika walio teuliwa nao
wamenyenyekea, hasemi mmoja wao ila akipewa idhini na Arrahman, Mwingi wa
rehema, kuwa aseme, naye atasema lilio sawa tu.
39. Hiyo ndiyo siku isiyo na shaka. Basi atakaye na ashike
njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi arejee kwa Imani, na a'mali njema.
40. Hakika Sisi tumekuhadharisheni na adhabu itakayo tokea karibu, siku atakapo angalia mtu vitendo vyake vilivyo tangulizwa na mikono yake, na atakapo sema kafiri kwa kutamani kuokoka: Laiti ningeli bakia udongo baada ya kufa, nisifufuliwe wala nisihisabiwe!