1,2,3,4,5,6,7. Naapa kwa Aya zilizo tumwa kwa ulimi wa Jibrili
kumpelekea Muhammad kwa upole wa kawaida na kheri, na kwa Aya zenye kuzitwaa kwa
nguvu dini nyengine zote za uwongo zikizipeperushia mbali, na kwa Aya zenye
kueneza hikima na uwongofu katika nyoyo za walimwengu kwa uenezi mkubwa mno, na
zenye kufarikisha baina ya kweli na uwongo kwa mfarakano ulio wazi kabisa, na
zenye kuwapa watu mawaidha ya kuwanufaisha, ili iwe ni udhuru kwao na onyo
wasiwe na hoja, hakika haya mliyo ahidiwa ya kuja Kiyama kwa yakini yatatimia tu
bila ya shaka yoyote.
8,9,10,11. Basi nyota zitapo
ondolewa kabisa, na mbingu zitapo pasuka, na milima ikavurugwa na ikapeperushiwa
mbali na upepo, na Mitume wakawekewa wakati maalumu wahudhurie kwa ajili ya
kuwatolea ushahidi kaumu zao.
12,13,14,15. Kwa ajili ya
siku gani yametayarishwa mambo haya makubwa makubwa? Kwa ajili ya siku watakapo
pambanuliwa baina ya viumbe. Na nini cha kukujuvya ina nini hiyo siku ya
kupambanua? Ni maangamio ya milele siku hiyo kwa hao wanao kadhibisha walio
waahidi Mitume!
16,17,18. Kwani hatukuwaangamiza mataifa
ya zamani yaliyo kadhibisha, na kisha tukawafuatilizia hao wenginewe
tukawateketeza hali kadhaalika, kwa madhambi waliyo yafanya na walivyo mkataa
Mwenyezi Mungu?
19. Siku hiyo ni siku ya kuteketezwa walio kadhibisha, kama
tulivyo waahidi.
20,21,22,23,24.
Kwani hatukukuumbeni kutokana na maji yaliyo dhalili, nayo ni manii, na
tukayaweka maji haya katika pahala patulivu, mpaka kutimilia kuumbwa kwake na
kutengenezwa kwake kwa muda anao ujua Mwenyezi Mungu. Nasi tukaweka vipimo
katika kuumbwa kwake, na kutengenezwa kwake, na kutoka kwake. Basi wabora wa
kupima na kukadiria ni Sisi. Ole wao hao wanao kadhibisha neema za kuumba na
kukadiria.
25,26,27,28. Kwani
hatukuifanya ardhi kuwa imekusanya juu ya mgongo wake viumbe vilivyo hai visio
hisabika, na vilio kufa visio kadirika, na tukaweka milima iliyo thibiti imara
mirefu, na tukakunywesheni maji matamu? Wataangamia siku hiyo hao wanao
kadhibisha neema hizi!
29,30,31. Siku ya kupambanua wataambiwa
makafiri: Nendeni huko Motoni mliko kuwa mkikukanusha. Nendeni kwenye joto la
moshi wa Jahannamu ulio gawika kwa ukubwa wake mapande matatu. Hapana cha
kujikinga na joto la siku hiyo, wala kivuli hicho hakipunguzi joto la mwako hata
kidogo.
32,33,34. Moto huo hutupa macheche yenye
ukubwa kama majumba, au utaona hayo macheche kama ngamia weusi wenye kuingia
rangi ya manjano. Wataangamia siku hiyo wanao kanusha kwamba hizi ndizo sifa za
Moto.
35,36,37. Haya uliyo simuliwa yatatokea
katika siku ambayo hawatatamka kitu cha kuwanufaisha, wala hawatakuwa na idhini
ya kutamka, wala hawatatoa udhuru, kwani hawana udhuru. Wataangamia siku hiyo
wanayo ikadhibisha siku hii.
38,39,40. Hii ndiyo siku ya kufafanua
baina ya mwenye ukweli, na mwenye uwongo, kwa kuwa kila mmoja atalipwa kwa
mujibu wa anavyo stahiki. Enyi mnao mkadhibisha Muhammad! Tumekujaalieni nyinyi
na walio kutangulieni walio kadhibisha mfano wenu, kama mnayo hila ya kujikinga
na adhabu basi fanyeni hila hiyo. Basi njooni muepukane na adhabu yangu.
Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha ahadi ya Mwenyezi Mungu.
41,42,43,44,45.
Hakika wachamngu wenye kujikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu watakuwa katika
kivuli kikubwa, na chemchem zinazo miminika, na matunda wanayo yaonea ladha, na
wanayo yapenda, wataambiwa kwa kuamkiwa na kukirimiwa: Kuleni na mnywe chakula
na vinywaji kwa starehe kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kuwa mkivitenda
duniani. Hakika Sisi huwalipa mfano wa malipo hayo matukufu watu wema.
Wataangamia siku hiyo wanayo ikadhibisha Pepo.
46,47. Na makafiri wataambiwa: Kuleni na
mjistareheshe kwa starehe isiyo baki muda mrefu, kwani hakika nyinyi ni wakosefu
kwa kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu. Wataangamia siku hiyo wanao ikadhibisha
neema.
48,49. Na wakiambiwa: Salini kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu, na mnyenyekeeni Yeye, hawanyenyekei wala hawasali; bali hushikilia kiburi
chao! Wataangamia siku wanao kadhibisha amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake.
50. Basi maneno gani hawa watayaamini ikiwa hawaiamini Qur'ani, na hali hii ni muujiza ulio toka mbinguni?