1. Hakika kimempitia mwanaadamu kipindi cha zama kabla
hajapuliziwa roho, naye hata bado hakuwa ni kitu cha kutajika kwa jina lake,
wala hajuulikani nini atakuwa.
2. Hakika Sisi tumemuumba mwanaadamu naye ana sifa namna
mbali mbali, kwa ajili ya kumtia mtihanini, majaribioni, baadaye. Kwa hivyo
tukamjaalia awe anasikia na anaona, ili apate kuzisikia Aya na azione Ishara.
3. Hakika Sisi tumembainishia Njia ya Uwongofu, ama awe Muumini
au awe kafiri.
4. Hakika Sisi tumewawekea tayari makafiri minyororo kuwafungia
miguu yao, pingu za kuwafungia mikono na shingo, na moto unao waka.
5,6. Hakika walio kuwa wakweli katika Imani yao
watakunywa mvinyo iliyo changanywa na maji ya kafuri. Hiyo ni chemchem wanayo
inywa waja wa Mwenyezi Mungu, na wanaipitisha watakapo kwa sahala.
7. Wanatekeleza yaliyo wajibikia , na wanaikhofu
Siku kubwa hiyo ambayo madhara yake yataenea kote kote,
8. Na huwalisha chakula mafakiri wasio weza kazi, na watoto
walio fiwa na wazee wao, na wafungwa wasio miliki kitu, ijapo kuwa wao wenyewe
hao watoaji wanakipenda hicho wanacho kitoa, na wanakihitajia.
9. Na hujiambia nafsi zao: Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili
ya kutaka thawa;bu za Mwenyezi Mungu. Sisi hatutaki kwenu malipo au
zawadi, wala hatutaki kushukuriwa na kusifiwa.
10. Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku ya
kumletea msiba atakaye kuwapo siku hiyo, na siku ya watu kukunja nyuso zao na
vipaji vyao.
11,12. Basi Mwenyezi Mungu akawalinda na shida za
siku hiyo, na badala ya mkunjo wa wenye maasi, akawapa nyuso za kupendeza,
na ukunjufu na furaha katika nyoyo zao, na akawajazi kwa ile subira yao Pepo
imeenea furaha, na nguo zake ni hariri laini.
13. Wakiegemea huko Peponi juu ya makochi, hawaoni joto la
jua, wala shida ya baridi.
14. Na Pepo ambayo vivuli vya miti yake vimeenea kote kote, na
matunda yake mepesi kuyachuma.
15,16. Na wakiwazungukia watumishi wao kwa bilauri
za kunywea zilio fanywa kwa fedha, lakini unaona kiliomo ndani kama kwamba ni
kigae, na vinapimwa vinywaji kwa kadiri wanavyo penda wanywaji.
17,18. Na watu wema hupewa kunywa huko Peponi
mvinyo inayo fanana na sharubati ya tangawizi kwa utamu. Hiyo ni kutokana na
chemchem ya Peponi inayo itwa Salsabil, kwa sababu ya wepesi wa unywaji wake na
uzuri wake.
19. Na watakuwa wanawazunguka vijana ambao hawabadiliki hali
yao, kwa furaha na sururi. Ukiwaona wanapo zunguka kwa wepesi na uchangamfu,
utawadhania kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao, kama lulu zilizo tandazwa mbele
yako zinang'ara.
20. Na ukitazama popote katika hiyo Pepo utaona neema kubwa,
na ufalme ulio tanda.
21. Juu yao zipo nguo za hariri nyepesi za kijani, na nguo za
hariri nzito. Na mapambo yao yaliomo mikononi mwao ni vikuku vya fedha. Na
Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji kingine kilio safi, hakina uchafu wala
najisi.
22. Hakika neema hizi ameziandaa kwa kukulipeni kwa vitendo
vyenu. Na hizo juhudi zenu duniani ni zenye kusifika kwa Mwenyezi Mungu, na
zinampendeza, na zimekubaliwa.
23. Hakika Sisi, kwa rehema yetu na hikima yetu,
tumekuteremshia wewe Qur'ani kwa njia ya kukutuza moyo wako, na uweze daima
kuihifadhi, basi huto isahau kabisa.
24. Basi subiri, uivumilie hikima ya Mola wako Mlezi kwa
kuakhirisha kushinda kwako kuwashinda maadui zako, na wewe ukapata mitihani kwa
maudhi yao. Wala usiwat'ii washirikina, wingi wa madhambi, walio zama katika
ukafiri.
25,26. Na dumisha kumkumbuka na kumtaja Mola wako
Mlezi, na sali alfajiri mapema, na adhuhuri, na alasiri jioni, na usiku sali
magharibi na isha. Na fanya ibada za usiku kwa muda mrefu.
27. Hakika hawa makafiri wanaipenda dunia, na wanaifadhilisha
kuliko Akhera. Na wanaiacha migongoni mwao siku yenye misiba mikubwa, na vitisho
vikali. Wala wao hawajui nini cha kuwaokoa wao na hayo!
28. Sisi tumewaumba wao, na tumefanya kwa hikima kuumbwa
kwao. Na tukitaka tutawateketeza wao na tutawaleta mfano ya wao badala
yao, ambao hao watakuja kumt'ii Mwenyezi Mungu kinyume na wao.
29. Hakika Sura hii ni mawaidha kwa walimwengu wote. Basi
mwenye kutaka atafuata njia ya Imani na uchamngu kwendea kwa Mola wake Mlezi
imfikishe kwenye maghfira yake na Pepo yake.
30. Wala nyinyi hamwezi kutaka kitu chochote ila wakati anapo
taka Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zenu, Mwenye
hikima kwa anayo yataka na akayakhiari.
31. Humuingiza amtakaye katika Pepo yake. Basi kuingia Peponi ni kwa fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu. Naye amewadhalilisha wenye kudhulumu, amewatengenezea adhabu iliyo chungu.