1,2,3. Ninaapa na natilia mkazo kiapo hichi
kwa Siku ya Kiyama, na hiyo ni kweli iliyo thibiti; na ninaapa na natilia mkazo
kiapo hichi kwa nafsi inayo mlaumu mtu kwa dhambi zake na upungufu wake, ya
kwamba bila ya shaka yoyote mtafufuliwa baada ya kukusanywa mafupa yenu yaliyo
tawanyika. Hivyo mtu anadhani baada ya kuwa Sisi tulimuumba naye hakuwa kitu
chochote, tutakuja shindwa kuyakusanya mafupa yake yaliyooza na yakatapanyika?
4. Hasha! Sisi tuna uweza wa kuviweka sawa hata vifupa vya
vidole vyake vilivyo vurugika, wachilia mbali mafupa yake makubwa makubwa ya
mwili wake.
5. Hivyo mtu anakanya kufufuliwa? Anataka abakie katika
uasi wake katika siku zote zilizo mbakilia katika umri wake ulio salia?
6. Anauliza kwa kuona haiwezi kutokea saa ya Kiyama: Lini
itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?
7,8,9,10. Jicho litapo tahayari
kwa kufazaika na kushtuka, na mwangaza wa mwezi ukapotea, na jua likakusanyika
na mwezi kuchomoza magharibi, mtu hapo atasema: Yako wapi makimbilio kuikimbia
hii adhabu?
11,12. Huachi, ewe mtu, kutafuta makimbilio?
Leo huna pa kukimbilia wewe, ila kwa Mola wako Mlezi peke yake, ndipo penye
matulivu ya waja, Peponi au Motoni.
13. Siku hiyo mtu ataambiwa vitendo vyake alivyo vitanguliza
na alivyo viakhirisha.
14,15. Bali mtu yeye mwenyewe ni hoja iliyo wazi
juu ya nafsi yake inayo mkazania kwa anayo yatenda na anayo yaacha. Na
ijapo kuwa atajitolea chungu nzima ya udhuru na akazieneza, hawezi kabisa
kuepukana na hoja hizo.
16,17. Usiuharikishe ulimi wako kwa kuisoma Qur'ani
na kujaribu kuihifadhi kwa haraka pale unapo teremshiwa kwa Wahyi. Hakika ni juu
yetu Sisi kuikusanya hiyo katika kifua chako, na kuithibitisha katika ulimi
wako.
18,19. Akikusomea Mjumbe wetu (Jibril) basi nawe
ifuatilize kama unavyo isikia. Kisha baada ya hayo ni juu yetu kuibainisha
ikiingia tatizo lolote juu yako.
20,21. Wacheni kukanya kufufuliwa, na hilo ni jambo
la kweli. Lakini nyinyi mnaipenda dunia na starehe zake, na mnaiacha Akhera na
neema zake.
22,23. Siku hiyo zitakuwapo nyuso nzuri, zenye
kumwangalia Mola wao Mlezi bila ya kusema kwa sifa gani, wajihi gani, au masafa
gani.
24,25. Na nyuso nyengine zitakuwapo zimenuna,
zimekunjana mno, zinangojea zitendewe jambo ambalo kwa kitisho chake linavunja
uti wa mgongo.
26,27,28,29,30.
Mna nini na kuipenda dunia ambayo mnaifariki roho inapo fika katika mafupa ya
kooni, na walio hudhuria wakasema: Yupo wa kumganga huyu kwa haya aliyo nayo?
Akayakinisha yule yaliyo mfika mauti kama lililo mshukia ni kuiacha dunia inayo
pendwa, na imekwisha mfika shida yake kikomo cha mwisho. Na muundi wa mguu
umekwisha ambatana na wa pili wakati wa kutoka roho. Kwa Mola wako Mlezi tu siku
hiyo ndio machungio ya waja, ama Peponi au Motoni.
31,32,33. Binaadamu amekanya kufufuliwa,
na kwa hivyo hakumsadiki Mtume wala Qur'ani. Wala hakumtimizia Mwenyezi Mungu
faridha za Sala. Lakini aliikadhibisha Qur'ani, akaipuuza Imani, na akatoka
kwenda kwa watu wake wa nyumbani kwa maringo na kujitapa.
34,35. Ewe unaye kadhibisha, utaangamia! Tena
utaangamia! Na tena utaangamia, na utaangamia!
36. Hivyo anadhani huyu mtu anaye kanya kufufuliwa kuwa
ataachwa hivi hivi akiringa tu katika maisha yake, na akisha kufa iwe basi, wala
asifufuliwe akahisabiwa kwa vitendo vyake?
37,38. Kwani yeye mtu hakuwa ni tone tu ya manii,
ilio jaaliwa kuwemo katika tumbo la uzazi? Kisha hiyo tone ikawa kipande cha
damu iliyo ganda, na Mwenyezi Mungu akaiumba, akaisawazisha mpaka ikawa na umbo
zuri?
39. Akajaalia namna mbili, mwanamume na mwanamke?
40. Je! Huyo Muumba wa mwanzo aliye fanya yote haya, basi si muweza wa kuwahuisha maiti baada ya kuyakusanya mafupa yao?