1,2,3,4. Ewe uliye jigubika kwa
maguo! Inuka hapo kitandani, na uwahadharishe watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa hawaamini. Na mkusudie Mola wako Mlezi makhsusi kwa kumtukuza. Na safisha
nguo zako kwa maji kuzitoa najisi.
5,6,7. Na iache adhabu, yaani kuwa daima
mwenye kujitenga na yanayo pelekea kupata adhabu. Wala usimpe mtu yeyote kwa
kutumai kupata zaidi kwake katika kile unacho mpa; na kwa ajili ya
kumridhi Mola wako Mlezi subiri na stahamili juu ya maamrisho na makatazo, na
kila jambo la juhudi na mashaka.
8,9,10. Na litakapo pulizwa barugumu, huo
ndio wakati wa siku ya shida kwa makafiri, wala si wepesi kwao kujitoa na
majadiliano ya hisabu, na vitisho vyenginevyo.
11,12,13,14,15.
Niache peke yangu na huyo niliye muumba. Kwani hakika Mimi ninatosha kukukifia
mambo yake. Nimemjaalia mali yaliyo kunjuliwa yaliyo enea, yasio tindikia, na
wana wanao tokea hadharani naye, na nikamkunjulia cheo na ukubwa kwa ukunjufu
ulio timia. Kisha tena anatumai nimzidishie mali na wana na cheo bila ya
shukrani yoyote!
16,17. Kuivunja hiyo tamaa yake, tunasema kwamba
kwa kuwa yeye alikuwa akiikaadhibisha Qur'ani kwa inda, tutamgubika kwa
adhabu yenye mashaka, wala hataweza kuikwepa.
18,19,20. Hakika yeye amejifikiria nafsi
yake, na akajitengenezea ya kuyasema ya kuitia ila Qur'ani, basi kwa hivyo
amestahiki kuangamia huko. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo! Kisha
akastahiki maangamizo hayo. Vipi alivyo jiandalia kutia ila hiyo!
21,22,23,24. Kisha
akaziangalia nyuso za watu. Kisha akakunja uso wake, na akazidi kuukunja, kisha
akaipa mgongo haki na akajivuna kuwa ati haitambui, na akasema: Haya si chochote
ila ni uchawi ulio nukuliwa kutokana na watu wa kale.
25. Maneno haya si chochote ila ni maneno ya viumbe aliyo
jifundisha Muhammad, na akadai kuwa ati yametoka kwa Mwenyezi Mungu.
26,27,28,29,30.
Nitamtia Motoni aungue humo. Na nini kitakujuvya hiyo Jahannamu ni nini?
Haibakishi nyama wala haisazi fupa ila italiunguza tu, ngozi ibabuke iwe nyeusi.
Juu yake wako kumi na tisa wanao angalia kazi yake, na kuwaadhibu waliomo.
31. Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, na wala
hatukuifanya idadi yao ya kumi na tisa ila kuwapa mtihani walio kufuru wapate
yakini walio pewa Kitabu (yaani Biblia, Mayahudi na Wakristo) kwamba inayo sema
Qur'ani juu ya walinzi wa Motoni ni kweli tupu itokayo kwa Mwenyezi Mungu
Mtukufu, kwa kuwa hayo yanakubaliana na vinavyo sema vitabu vyao; na ili walio
muamini Muhammad ipate kuzidi Imani yao. Na wala wasiyatilie shaka hayo
walio pewa Kitabu na Waumini. Na wenye maradhi ya unaafiki katika nyoyo zao na
makafiri waseme: Mwenyezi Mungu anataka nini kwa idadi hii ya ajabu? Kwa mfano
kama huu ulio tajwa, wa kupoteza na kuongoa, ndio Mwenyezi Mungu huwapoteza
makafiri na huwaongoa Waumini. Na hapana anaye wajua askari wa Mola wako Mlezi,
jinsi walivyo kuwa wengi mno, ila Yeye Subhanahu wa Taala. Na huo Moto si
chochote ila ni kumbusho na kitisho kwa binaadamu.
32,33,34,35,36.
Kuzidi kumhadharisha anaye onywa naye asiogope, ninaapa kwa mwezi na usiku unapo
ondoka, na kwa asubuhi inapo angaza na kuchomoza, kwamba huu Moto ni moja katika
vitisho vikubwa kabisa vya kuonya na kukhofisha.
37. Ni onyo kwa binaadamu kwa atakaye kuja mbele katika nyinyi
kutenda kheri, au kubaki nyuma asitende.
38,39. Kila nafsi itashikwa kwa iliyo yatenda, ila
Waislamu walio zigomboa shingo zao kwa ut'iifu.
40,41,42. Hao watakuwa katika Mabustani
ya Peponi, ambayo hayawezekani kusifika. Wataulizana wao kwa wao khabari za
wakosefu, wakiuliza hali zao nini kilicho watia Motoni?
43,44,45,46,47.
Waseme: Hatukuwa miongoni mwa wenye kusali kama wasalivyo Waislamu. Wala
hatukuwa tukiwalisha masikini kama Waislamu walivyo kuwa wakilisha. Na tulikuwa
tukijisoza na kuzama katika upotovu na mazungumzo ya uwongo pamoja na hao walio
kuwa wakiporojoka. Na tulikuwa tukiikadhibisha Siku ya Hisabu, mpaka ikatujia
yakini, yaani mauti.
48. Basi hao hakuto waokoa kuombewa msamaha na waombezi,
wakiwa ni Malaika, au Manabii, au watu wema.
49. Basi wana nini hata wanajitenga na mawaidha ya Qur'ani?
50,51. Hao hakika wamekuwa kama punda wanao
toka mbio kumkimbia anaye wafukuza.
52. Bali kila mmoja wao anataka apewe ukurasa unao toka
mbinguni uwazi ulio funguliwa unao thibitisha ukweli wa Mtume s.a.w. (yaani kama
shahada ya Ujumbe wake kwao!)
53. Juu ya kuzidi kuwaonya kwa hayo wayatakayo bali hawaikhofu
Akhera, na wakapuuza mawaidha, na wakavumbua mbinu mbali mbali za kutaka miujiza
na Ishara.
56. Na wala hawatakumbuka ila Mwenyezi Mungu atake Mwenyewe, kwani Yeye ndiye anaye stahiki kuogopwa, na Yeye ndiye wa kumsamehe mwenye kumcha.