1,2. Ewe Muhammad! Waambie watu wako: Nimepata wahyi
kwamba kikundi cha majini kimesikia kusoma kwangu Qur'ani, nao wakawaambia
wenzao: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya namna ya peke yake, hatujapata kusikia
mfano wake kabla yake, inaitia kwenye uwongofu na usawa. Kwa hivyo tumeiamini
hiyo Qur'ani tuliyo isikia; na kabisa hatutamshirikisha Mola wetu Mlezi aliye
tuumba na kutulea na chochote katika waja wake.
3. Na kwamba hakika cheo na utukufu wa Mola wetu Mlezi
umetukuka; hana mke wala mwana.
4. Na hakika wajinga katika sisi walikuwa wakimzulia Mwenyezi
Mungu maneno yaliyo kuwa mbali kabisa na ukweli na kuwa sawa.
5. Na hakika sisi tulikuwa tunadhani kuwa haiwi binaadamu au
jini kumzulia Mwenyezi Mungu jambo ambalo si laiki naye kusifika nalo.
6. Na walikuwako wanaume katika wanaadamu wakitafuta ulinzi kwa
wanaume wa kijini. Basi hao binaadamu hawakuwazidishia majini ila kuzidi uasi na
ujinga na ujeuri.
7. Na hakika majini walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, enyi
binaadamu, kwamba Mwenyezi Mungu hatamfufua yeyote baada ya kwisha kufa, wala
hatowaletea watu Mtume yeyote wa kibinaadamu.
8. Na hakika sisi tulitaka kufikilia mbinguni, tukakuta kumejaa
walinzi wa kimalaika wenye nguvu, na vimondo vinavyo unguza kutoka upande huo.
9. Na sisi kabla ya leo tulikuwa tukikaa pande za mbinguni
kwenye makao kwa ajili ya kuchunguza khabari za mbinguni. Lakini sasa mwenye
kutaka kusikiliza anakuta vimondo vinamngojea kumzuia na kumteketeza.
10. Na hakika sisi hatujui imekusudiwa adhabu kwa walioko
katika ardhi kwa huku kulindwa mbingu hata ikazuiliwa kusikilizwa, au Mola wao
Mlezi anawatakia kheri na uwongofu?
11. Na hakika miongoni mwetu wapo walio wema wachamngu, na
miongoni mwetu pia wapo walio kinyume na hivyo. Na hao ni walio wastani katika
wema wao. Kwa hivyo sisi ni wa makundi mbali mbali.
12. Na hakika sisi tumeyakinika kwamba hatutamshinda Mwenyezi
Mungu popote tutapo kuwapo katika ardhi, wala hatutamshinda hata tukifanya
tuikimbie hukumu yake kwendea mbinguni.
13. Na hakika sisi tulipo isikia Qur'ani tuliiamini. Na mwenye
kumuamini Mola wake Mlezi basi hachelei kupunguziwa chochote katika mema yake,
wala kudhulumiwa kwa kuzidishiwa maovu yake.
14. Na hakika kati yetu wapo Waislamu wenye kuikubali Haki, na
miongoni mwetu wapo wenye kuiacha njia ya uwongofu. Basi wenye kusilimu hao
wameifuata njia ya Haki, na ni wenye kufanya jitihada katika kuikhiari njia
hiyo.
15. Ama majeuri walio iacha njia ya Uislamu basi hao watakuwa
ndio kuni za Jahannamu.
16. Na hakika lau kuwa watu na majini wakifuata Njia ya
Uislamu, wala wasende upogo wakaiwacha, basi bila ya shaka tutawanywesha maji
mengi yatakayo enea nyakati za haja.
17. Ili tuwajaribu tuwaone vipi watavyo mshukuru Mwenyezi
Mungu kwa neema anazo waneemesha. Na mwenye kukengeuka na ibada ya Mola wake
Mlezi atamtia katika adhabu ya mashaka asiyo yaweza kuyachukua.
18. Na imefunuliwa kwangu kwamba kwa hakika misikiti ni ya
Mwenyezi Mungu peke yake. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
19. Na imefunuliwa kwangu kwamba alipo simama Mja wa Mwenyezi
Mungu, Muhammad, katika Sala yake akimuabudu Mwenyezi Mungu, majini
walijikusanya makundi kwa makundi, wakistaajabu kwa waliyo kuwa wakiyaona na
wakiyasikia.
20. Sema: Hakika mimi namuabudu Mola wangu Mlezi peke yake,
wala simshirikishi na yeyote katika ibada.
21. Sema: Mimi sina uweza wowote juu yenu wa kukuondoleeni
madhara, wala kukuleteeni uwongofu na manufaa.
22. Sema: Hakika mimi hapana yeyote awezae kuniondolea adhabu
nikimuasi Mwenyezi Mungu. Wala sipati pa kukimbilia, kuikimbia adhabu yake.
23. Lakini niliwezalo ni kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu na
Risala zake alizo nituma nizifikishe. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, na akaipuuza Dini ya Mwenyezi Mungu, basi hakika mtu huyo atapata Moto wa
Jahannamu abakie humo milele.
24. Hata watakapo iona adhabu waliyo ahidiwaa, hapo basi
watajua wakati itapo shuka, nani mwenye msaidizi dhaifu asiye na nguvu, na yupi
mchache wa idadi. Ni wao au Waumini?
25. Sema: Enyi makafiri! Sijui ni karibu hiyo adhabu mliyo
ahidiwa, au Mola wangu Mlezi ataifanya iwe mbali?
26,27. Yeye ndiye Mjuzi wa ghaibu, yaliyo siri.
Hapana mmoja katika viumbe vyake anaye ijua siri yake, ila Mtume aliye mridhia
kumjuvya baadhi ya hiyo siri. Naye humwekea mbele ya huyo Mtume na nyuma yake
Malaika wa kumkinga na wasiwasi.
28. Ili Mwenyezi Mungu ayajue hayo yametokea kwa kuwafikiana na alivyo kadiria, ya kwamba Manabii hakika wamefikisha Risala za Mola wao Mlezi. Na kwa hakika Yeye kesha jua kwa kufananua yote waliyo nayo, na anajua idadi ya viumbe vyote. Hapana kitu kinacho mpotea Yeye.