1. Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake, na tukamwambia:
Waonye watu wako kabla haijawajia adhabu yenye machungu makali.
2,3,4. Nuh'u akasema: Enyi watu wangu!
Hakika mimi ni mwonyaji kwenu, nina risala kutoka kwa Mola wenu Mlezi kwa lugha
mnayo ijua, ya kwamba mumt'ii Mwenyezi Mungu, na mumnyenyekee katika kutimiza
waajibu zote; na mwogopeni Yeye kwa kuacha mnayo katazwa, na nit'iini mimi
katika ninayo kunasihini. Ndipo Mwenyezi Mungu atapo kusameheni madhambi yenu,
na atakupeni umri mrefu mpaka ifike ajali iliyo wekwa mwisho wa umri wenu.
Hakika mauti yakija hayaakhirishwi kabisa! Lau kuwa mngeli jua majuto mtakayo
kuwa nayo utapo kwisha muda wenu mngeli amini.
5,6. Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi
nimewaita watu wangu waamini usiku na mchana bila ya kuchoka, hawakuzidishwa na
wito wangu ila kuukimbia ut'iifu wako.
7. Na mimi kila nikiwataka wakuamini Wewe upate kuwasamehe,
hubandika vidole vyao kwenye masikio yao ili wasisikie wito wangu, na hujifunika
kwa maguo yao ili wasiuone uso wangu! Na wakasimama kidete juu ya ukafiri wao,
na wakatakabari kutakabari kukubwa mno!
8,9. Kisha nikawaita waje kwako kwa sauti ya juu,
kisha nikaudhihirisha wito kwa namna moja, na nikawaita kisirisiri kwa namna
nyengine, ili nijaribu kila njia.
10,11,12. Nikawambia watu wangu: Takeni
kwa Mola wenu Mlezi maghfira kwa kufru zenu na maasi yenu. Kwani Yeye bado ni
Mwingi wa kusamehe madhambi ya mwenye kurejea kwake. Atakuleteeni mawingu
yatakayo miminika mvua kwa wingi, na atakupeni mali na wana, na hayo ndiyo
mapambo ya dunia, na atakupeni mashamba mtayo starehea kwa uzuri wake na matunda
yake, na atakujaalieni mito ya kunyweshea mazao yenu na mifugo yenu.
13,14. Mna nini nyinyi hata hamumtukuzi Mwenyezi
Mungu kama anavyo stahiki kutukuzwa, ili mtaraji akukirimuni kwa kukuokoeni na
adhabu, na hali Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa madaraja, tangu tone ya manii,
kisha pande la damu, kisha pande la nyama, kisha mafupa na nyama?
15,16. Kwani huoni vipi Mwenyezi Mungu alivyo
ziumba mbingu saba, moja juu ya moja, na akaufanya mwezi katika mbingu hizo
unatoa nuru, na akalifanya jua ni taa ambayo kwayo watu wa duniani ndio wanaona
kwa mwangaza wake yote wanayo hitajia kuyaona?
17,18. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni
kutokana na ardhi, akakuotesheni kama miema kwa njia ya ajabu, kisha baada ya
kufa atakurejesheni huko huko kwenye ardhi, na tena atakutoeni huko kwa hakika
hapana hivi wala hivi.
19,20. Na Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi iliyo
kunjuliwa ili mpate kwenda humo katika njia zenye wasaa.
21,22. Alisema Nuh'u: Mola wangu Mlezi! Hakika watu
wangu wamenikatalia mimi niliyo waamrisha ya kuamini na kutaka msamaha, na
wakawafuata madhaifu miongoni mwao ambao mali yao na watoto wao hawawazidishii
ila khasara tupu katika Akhera. Na vitimbi vya hao wenye mali mengi, na wana
wengi, kwa wanyonge wanao wafuata ni vitimbi vilivyo fika ukomo kwa ukubwa.
23,24. Na wao wakiwaambia: Msiache kuiabudu miungu
yenu, wala msimwache Wadda, wala Suwaa' , wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala
Nasra. Na hawa walikuwa miungu ya masanamu iliyo chongwa kwa sura ya wanyama
namna mbali mbali. Na miungu hii iliwapoteza watu wengi. Na wala huwazidishii
wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na inda, ili kuzidi kubaidika na Haki.
25. Kwa sababu ya madhambi yao wakazamishwa kwa tofani, na
baada ya kuangamizwa kwao wakatiwa Motoni kwenye moto mkali wa kuwaka na
kuteketeza, na wala wasipate yeyote baada ya kumkosa Mwenyezi Mungu, wa
kuwanusuru na kuwakinga na adhabu!
26. Na Nuh'u akasema baada ya kukata tamaa nao watu wake: Mola
wangu Mlezi! Usimwache yeyote katika hao wanao kukataa Wewe akabaki akizunguka
juu ya ardhi!
27. Ewe Mola wangu Mlezi! Ukiwaacha hao bila ya kuwateketeza
na kuwang'oa watawatia waja wako katika upotovu, na wao hawatozaa ila wenye
kupotoka vile vile wakaiacha haki, na wakakithiri kukukanya na kukuasi.
28. Mola wangu Mlezi! Nisamehe mimi na wazazi wangu ambao ndio walio kuwa ni sababu ya kuzaliwa mimi, na kila mwenye kuingia nyumbani kwangu kwa kukuamini Wewe, na uwasamehe Waumini wote wanaume na wanawake. Na usiwazidishie makafiri ila kuwaangamiza.