1,2,3. Ameita, mwenye kuita, kuhimiza kama
kufanya kejeli, iletwe upesi adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo hapana
shaka itawashukia makafiri. Wala hapana chochote cha kuzuia adhabu hiyo, kwani
hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu, ambako huko ndiko zinatoka nguvu
zinazo simama, na hukumu inayo tekelezwa.
4. Malaika na Jibrili wanapanda kwenda kunako toka amri yake
kwa siku ambayo urefu wake ni miaka khamsini elfu kwa mujibu wa hisabu ya miaka
ya duniani.
5,6,7. Basi, ewe Muhammad! Subiri
uwastahamilie hizo kejeli zao, na kuhimiza kwao adhabu, kwa subira isiyo kuwa na
mbabaiko ndani yake wala mashtaka. Hakika hao makafiri wanaiona hiyo Siku ya
Kiyama ni kitu cha muhali kutokea. Na Sisi tunaona kuwa ni jambo jepesi katika
uweza wetu, wala halina uzito wowote.
8,9,10. Siku mbingu itakapo kuwa kama
fedha iliyo yayuka, na milima itakapo kuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na
ikapigwa, wala jamaa hamuulizi jamaa yake: Nini hali yako? Kwa sababu kila mmoja
kajishughulikia nafsi yake!
11,12,13,14. Watakuwa
wakijuulishana wao kwa wao mpaka wajuane baraabara, na ilhali hapana amuulizae
mwenzie kitu. Kafiri atatamani lau ange pata kujikomboa nafsi yake na adhabu
hiyo Siku ya Kiyama kwa kumtoa mwanawe awe ni fidia yake, au mkewe, au nduguye,
au jamaa zake aliyo khusiana nao, na wote waliomo duniani, apate kuokoka yeye
tu!
15,16,17,18. Ewe mkosefu!
Wacha hayo unayo yatamani ya kutaka kujikomboa kwa fidia! Hakika huo moto,
unawaka kweli! Utakubabua mikono yako, na miguu yako, na viungo vyako vyote,
utanadi kwa jina la huyo aliye iacha Haki, na akaacha ut'iifu, na akakusanya
mali akayaweka katika mabweta yake, wala hakutoa haki ya Mwenyezi Mungu iliomo
katika hayo mali!
19,20,21,22,23.
Hakika tabia ya binaadamu ni papara, mwingi wa kupapatika, na kutoridhika
akifikiwa na lolote la karaha na uzito, na ni mwingi wa kuzuia na kunyima
akipata kheri na neema. Isipo kuwa wanao sali, ambao wanadumisha Sala zao,
hawakikosi hata kipindi kimoja. Hao Mwenyezi Mungu huwakinga, na
huwawezesha kutenda yaliyo kuwa ya kheri.
24,25. Na wale ambao katika mali yao ipo haki iliyo
ainiwa iliyo wekwa kwa ajili ya masikini mwenye kuomba kutaka msaada, na anaye
jizuilia kuomba pia. (Katika wanao zuilika kuomba wanaingia si wenye
kustahi na kuona vibaya tu, bali pia wasio weza kuomba kama watoto wachanga,
wagonjwa, na wanyama pia.)
26,27,28. Na wale wanao isadiki Siku ya
Malipo, basi wanajitayarisha kwa ajili yake; na wale wanao iogopa adhabu ya Mola
wao Mlezi basi wanajikinga nayo wala hawajitii katika jambo la kuwaletea adhabu
hiyo. Kwani hakika adhabu ya Mola wao Mlezi hapana hata mmoja anaye weza
kuaminika nayo isimpate.
29,30,31. Na ambao wanazihifadhi tupu
zao hata hawaemewi na matamanio yao. Lakini kwa wake zao na masuria wao
hawazihifadhi; kwa sababu hapo hawalaumiwi kuifuata tabia ya maumbile. Basi
mwenye kutafuta starehe ya maingiliano kwa wasio kuwa wake na masuria, basi hao
tena ni wenye kuikiuka halali na kuingia katika haramu.
32,33,34. Na hao wenye kuzihifadhi amana
za sharia na amana za waja wa Mwenyezi Mungu, na walio lazimika nayo kwa
Mwenyezi Mungu na kwa watu bila ya kukhuni wala kupunja, na ambao kwa shahada
zao wamesimama sawa sawa kwa haki bila ya kuficha wanalo lijua, na wanao hifadhi
Sala zao wakizisali sawasawa kwa ukamilifu -
35. Watu wenye sifa kama hizo nzuri watakuwa ni wenye
kuhishimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu huko Peponi.
36,37,38. Kitu gani kinawapelekea hao
walio kufuru kukujia mbio mbio kutoka kuliani na kushotoni kwa makundi? Je,
kwani kila mmoja wao ana tamaa ya kuingia kwenye Pepo yenye neema, baada ya
kusikia kuwa Mwenyezi Mungu amemuahidi Mtume wake na Waumini kuwatia Peponi?
39. Basi nawaache hiyo tamaa yao ya kuingia Peponi. Hakika
Sisi tumewaumba wao kutokana na maji ya kudharauliwa.
40,41. Naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote, na
magharibi zote za siku, na sayari na hidaya, kwamba hakika bila ya shaka Sisi
tuna uweza wa kuwaangamiza, na kuwaleta walio wat'iifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu
kuliko wao. Wala Sisi hatushindwi kubadilisha huko.
Huenda ikawa
inakusudiwa kwa "mashariki zote" na "magharibi zote" ni maeneo ya mamlaka ya
Mwenyezi Mungu yote ambayo hayana mpaka kama ilivyo ashiriwa katika Aya 137 ya
Surat Al-A'araf: "Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki za
nchi na magharibi zake ambayo tuliitia baraka", kuonyesha sehemu zote za hiyo
nchi inayo tajwa.
Na huenda ikawa makusudio yake ni mashariki za jua
na mwezi na nyota zote na sayari, na magharibi zao, kwa ajili ya kuonyesha vile
vile ufalme wa Mwenyezi Mungu wote. Na kwa hivyo inadhihirika kwetu kuwa vyombo
vinavyo kwenda katika qubba la mbingu vinachomoza kwenye upeo wa mashariki na
kuchwa kwenye upeo wa magharibi, au kwa uchache vinazunguka kutoka mashariki
kwendea magharibi kuizunguka nyota ya Pole, katika sehemu ya kaskazini ya dunia.
Kwani umbali wa Pole kwa nyota ni mdogo kuliko pahala unapo angalia, basi nyota
hapo haichomozi wala haichwi, bali hupiga duru ndogo kuizunguka North Pole. Na
kwa hiyo Aya inaashiria saa za usiku. Rejea kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu: " Na alama na kwa nyota wao wanaongoka." Na kwa udhaahiri wa kuchomoza
na kuchwa ipo ishara ya kuzunguka kwa dunia, na hiyo ni neema kubwa kabisa
katika neema za Mwenyezi Mungu juu ya maisha katika sayari hii. Kwani bila ya
kuzunguka kwa dunia juu ya msumari-kati wake nusu ya dunia ingeli pigwa na jua
mfululizo muda wa nusu mwaka kaamili, na ingeli nyimwa mwangaza kabisa nusu
nyengine. Kwa hivyo uhai kama tulivyo uzoea usinge kuwako.
Na
tukifanya hizo mashariki na hizo magharibi ni za jua peke yake, wachilia mbali
nyota nyengine na sayari, basi itakuwa ishara ni kule kuchomoza jua kila siku
pahala pengine na kuchwa pahala pengine kila siku, au hata katika kila dakika
linapo pita juu ya dunia. Kwani jua kila dakika linakuchwa pahala na linachomoza
pahala papili mfululizo. Na haya ni katika mipango ya Mwenyezi Mungu na miujiza
ya uweza wake. Tazama pia maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 5 katika Surat
Assaffat, na Aya 17 ya Surat Arrah'man.
42. Basi waachilie wakiporojoka katika upotovu wao, na
wakicheza na dunia yao, mpaka wakutane na siku yao waliyo ahidiwa kupewa adhabu.
43,44. Siku watakapo tolewa makaburini mbio mbio kumwendea huyo ataye waita, kama kwamba wamemweka ufundo na wakimuabudu duniani walivyo kuwa wakimkimbilia badala ya Mwenyezi Mungu, macho yameinama chini, hawawezi kuyanyanyua, yamegubikwa na unyonge na udhalili. Hiyo ndiyo siku waliyo kuwa wakiahidiwa duniani na wao wakiikanusha.