1,2. Kiyama ni Tukio litakalo tukia kwa haki, yaani kwa kweli. Ni nini hicho Kiyama kitacho tokea kweli?

 

3. Na kitu gani kitacho kujuvya ukweli wake, na kitacho kupa sura ya kitisho chake na shida zake?

 

4. Kina Thamudi na kina A'di walikanusha Kiyama kinacho wagutua walimwengu wote kwa kitisho chake na shida zake.

 

5. Ama Thamudi basi walihilikiwa kwa tukio lilio pindukia mipaka yote kwa ukali wake.

 

6. Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo ubaridi na mkali,

 

7. Mwenyezi Mungu aliwasalitisha nao muda wa masiku saba, na siku nane zilizo fuatana mfululizo, utaona walio patikana na upepo huo wamekuwa maiti kama magogo ya mitende yaliyo kuwa matupu ndani yake. ("Masiku" ni wingi wa "Usiku"; "Siku" wingi wake ni "Siku" vile vile.)

 

8. Je! Unamwona yeyote aliye bakia katika hao?

 

9. Akaja Firauni, na mataifa mengine yaliyo kufuru kabla yake, na wale jamaa walio acha mwendo wa haki na vitendo vya maumbile wakafanya vitendo vichafu kabisa hata miji yao ikapinduliwa juu chini.

 

10. Kila umma katika hawa walimuasi Mtume wa Mola wao Mlezi. Naye Mwenyezi Mungu akawashika kwa kuwaadhibu kwa mshiko ulio zidi ukali.

 

11. Maji yalipo zidi ukomo wake, na yakapanda juu ya milima katika tukio la tofani ya Nuhu, Sisi tulikupandisheni, yaani kwa kuwapandisha wazee wenu wa asli, katika safina inayo kwenda baharini.

 

12. Ili kulifanya tukio hilo la kuwaokoa Waumini na kuwazamisha makafiri liwe zingatio na mawaidha kwenu, na lihifadhiwe na kila sikio lenye kuhifadhi linalo sikia.

 

13,14. Litakapo pulizwa barugumu kwa mpulizo mmoja, na ardhi na milima ikaondolewa pahala ilipo, na ikavunjwa mara moja,

 

15,16. Siku hiyo ndiyo kitashuka cha kushuka, na mbingu zitapasuka kwa kuondoka hukumu zake na sharia zake, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu baada ya kuwa madhubuti zenye nguvu.

 

17. Na Malaika pembezoni mwake, na wapo Malaika wanane siku hiyo watakao beba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi, juu ya Malaika hawa wengine.

 

18. Siku hiyo ndio mtaletwa kwa ajili ya kuhisabiwa. Wala haifichikani siri  yenu yoyote mliyo kuwa mkiificha.

 

19. Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono  wake wa kulia, atasema akiwatangazia furaha yake walio karibu naye: Chukueni msome kitabu changu!

 

20. Mimi nilikuwa na yakini tangu duniani kuwa nitapata hisabu yangu, basi nikajitayarisha nafsi yangu kwa mkutano huu.

 

21. Basi huyo atakuwa katika maisha yaliyo enea kupendeza.

 

22. Katika Bustani ya pahali na daraja ya juu.

 

23. Matunda yake yakaribu kwa kuyachuma. (kuyatunda).

 

24. Kuleni na mnywe kwa kula na kunywa kusio na karaha, wala maudhi, kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kwisha vitanguliza katika siku za duniani zilizo pita.

 

25,26. Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto atasema kwa majuto na huzuni: Laiti kuwa sikupewa kitabu changu, wala sikuijua hisabu yangu!

 

27. Laiti kuwa kule kufa niliko kwisha kufa kungeli kuwa ndio kumalizika kwangu kwa mwisho, wala nisingeli fufuliwa tena!

 

28,29. Hapana chochote nilicho kimiliki duniani kilicho nifaa. Uzima wangu umenipotea, na nguvu zangu zimenitoka.

 

30,31,32. Wataambiwa walinzi wa Jahannamu: Mshikeni, na mfungeni mikono yake kwenye shingo yake. Kisha msimtie popote ila ndani ya Moto wa Jahannamu, kisha mfungeni kwenye mnyororo mrefu kabisa.

 

33,34. Hakika huyo alikuwa hamsadiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala hamhimizi yoyote kuwalisha masikini.

 

35,36,37. Basi hii leo huyu kafiri hana jamaa wa kumtetea, wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni, ambao kwa hakika ni mchanganyiko wa damu na usaha. Hawakili chakula hicho ila wakosefu walio kusudia kufanya maasi yao, na wakakamia kuendelea nayo.

 

38,39,40. Basi naapa kwa mnavyo viona katika vinavyo onekana, na msivyo viona katika ulimwengu wa ghaibu, kwamba hakika Qur'ani bila ya shaka inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ulimi wa Mjumbe mwenye cheo cha juu.

 

41. Wala Qur'ani si maneno ya mtunga mashairi kama mnavyo dai. Ama nyinyi ni chache mno imani yenu ya kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu.

 

42. Wala Qur'ani haisemi kwa maneno ya kumunyia munyia kama wanenavyo makuhani mlio wazoea. Ni uchache mno kukumbuka kwenu na kuzingatia khitilafu zilioko baina ya Qur'ani na maneno ya makuhani.

 

43. Hii ni uteremsho unao toka kwa Mwenye kuwaangalia walimwengu wote kwa kuwaumba na kuwalea.

 

44,45,46. Na lau kuwa angeli dai kitu chochote ambacho tusicho kisema basi bila ya shaka tungeli mshika akitoe kama mtu anavyo mkamata mtu kwa mkono wa kulia akammaliza hapo hapo. Kisha bila ya shaka tungeli mkata mshipa wake wa moyo, afe saa ile ile. (Biblia inasema katika Kumbukumbu la Torati 18.20 "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.")

 

47. Na hapana yeyote katika nyinyi, hata ange kuwa na nguvu namna gani, angeli weza kuzuia adhabu yetu isimfikilie.

 

48. Na hakika Qur'ani ni mawaidha kwa wanao fuata amri za Mwenyezi Mungu, na wanaepuka makatazo yake.

 

49. Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba kati yenu wapo wanao ikanusha Qur'ani.

 

50. Na kwamba hakika hiyo bila ya shaka ni sababu ya majuto ya wanao ikataa, wakati watapo iona adhabu yao, na neema za wenye kusadiki.

 

51. Na hakika Qur'ani bila ya shaka ni Haki iliyo thibiti, isiyo na shaka yoyote.

 

52. Basi mtakase Mola wako Mlezi, na dumisha kudhukuru jina lake.