1. Ametukuka, na amezidi baraka zake Mwenye kumiliki peke yake
uwezo wa kuendesha mambo ya viumbe vyote. Na Yeye, juu ya kila kitu, anao uwezo
ulio timia.
2. Ambaye ndiye aliye umba mauti na uhai kwa makusudio anayo
yataka Yeye, ili akufanyieni mtihani ni yupi katika nyinyi anaye fanya vitendo
sawa, na mwenye niya safi. Na Yeye ni Mwenye kushinda, wala hashindiki kwa kitu,
Mwenye msamaha kwa wenye upungufu.
3. Yeye ndiye aliye zizua mbingu saba zilizo pandana kwa mpango
mmoja sawa sawa. Huoni tafauti yoyote katika uundaji wa Mwenyezi Mungu, ambaye
rehema yake imeenea kwenye viumbe vyake vyote. Basi hebu tazama tena, unaona
khitilafu yoyote?
4. Kisha tazama tena, na tena! Jicho lako linakurejea mwenyewe
bila ya kugundua aibu yoyote, nalo limechoka.
5. Na hakika Sisi tumeipamba mbingu hii ya karibu, unayo iona
kwa macho, tumeipamba kwa nyota zinazo ng'aa. Na tumefanya katika hizo vimondo
vya kuwapopolea mashetani; na Akhera tumewaandalia adhabu ya moto
unao waka.
Mbingu ni kila kilicho juu yetu kikatufunika. Amesema
Ibn Sayyidih: Hiyo ni bahari ya anga na vyombo vyote viliomo ndani yake na
vimondo. Na sura wanayo iona wakaazi wa duniani katika masiku yaliyo safi
ni kama qubba la kibuluu lilio pambwa kwa nyota na sayari kama kwamba ni taa,
kama unavyo ziona nyota za mkia, au vimondo, vinakwenda angani vikiungua huko
juu ya ardhi. Na hilo qubba la kibuluu si chochote ila ni matokeo ya mwangaza wa
jua na nyota pamoja na takataka za vumbi zinazo ning'inia katika hewa, na sehemu
za hewa molecules zinazo tawanyika. Haya mbali na yanayo onekana katika mwangaza
nafsi yake ambayo huipamba mbingu hii ya karibu, kama vile zile rangi nzuri
nzuri za wakati wa kuchwa jua, au wakati wa kuchomoza jua alfajiri, na mianga ya
njia za nyota, miangaza ya kaskazini, na miangaza ya katika sehema za Polar
regions. Na hayo yote yanayo onekana ni matokeo ya kuingiliana mwanga pamoja na
funiko la anga la ardhi na uwanja wake wa smaku, magnetic field.
6. Na kwa ajili ya wasio muamini Mola wao Mlezi tumewawekea
adhabu ya Jahannamu. Na huo ndio mwisho muovu kweli kwao.
7,8. Wakitiwa humo watasikia sauti mbaya ya kuchusha,
na huo moto unatokota kwa ukali, unakaribia kukatika na kutawanyika kwa wingi wa
kuwaghadhibikia. Kila likitumbukizwa kundi mojapo kati yao walinzi wake
huwauliza kwa kuwakejeli: Kwani hakukujieni Mtume kukuhadharisheni na mkutano wa
siku hii ya leo?
9. Na wao watajibu: Ametujia mwonyaji, lakini sisi tulimkanusha
tukamwambia mwongo, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakukuteremshia chochote wewe
wala Mitume wenginewe. Nyinyi mnao dai Utume si chochote ila ni watu walio
potoka, na mko mbali na haki.
10. Na watasema: Lau kuwa tulikuwa tunasikia kama inavyo faa
asikie mwenye kutaka ukweli wa mambo, au tunafikiri tunayo itiwa, tusinge kuwa
miongoni mwa watu wa Motoni.
11. Basi wataungama kukadhibisha kwao na kukufuru kwao. Watu
wa Motoni wamepotelea mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu!
12. Hakika wenye kumkhofu Mola wao Mlezi, na hali wao
hawamwoni, watafutiwa madhambi yao, na watapata thawabu kubwa kwa mema yao.
13. Na ficheni kauli yenu, au itangazeni. Yote mawili kwa
Mwenyezi Mungu ni sawa, kwani Yeye ni Mkuu wa kuyazunguka yote kwa kuyajua,
Mjuzi wa vinavyo ficha vifua.
14. Kwani Muumba si Mwenye kujua mambo yote ya waja wake? Na
Yeye ni Mjuzi wa dogo na kubwa
15. Yeye ndiye aliye ifanya ardhi dhalili inakut'iini. Basi
tembeeni pande zake kote kote. Na kuleni katika riziki zake zinazo toka
ndani yake. Na kwake Yeye peke yake ndio kufufuliwa na kulipwa.
16. Je! Mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa
hatakukatieni ardhi, akakuchukulieni kwa ghafla kwa mtikiso mkubwa?
17. Bali, mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa
hatakupelekeeni upepo wa kukupopoeni kwa changarawe? Hapo basi mtakijiua kitisho
cha onyo langu kwenu!
18. Na hakika walikwisha wakanusha Mitume wao hao walio kuwa
kabla ya kaumu yako. Basi ghadhabu yangu juu yao ilikuwa hali gani kwa nilivyo
waangamiza na kuwashika!
19. Wameingia upofu? Wala hawakuwaangalia ndege walio juu yao,
vipi wanavyo kunjua mbawa zao mara kwa mara, na mara nyingine wakizikunja?
Hapana anaye washikilia wasianguke ila Mwingi wa Rehema. Hakika Yeye ni Mwingi
wa ujuzi na khabari kwa kila kitu. Anakipa kila kitu jambo kwa mujibu wa
maslaha yake.
Kukunjua huku ni kukunjua ndege mbawa zake bila ya
kuziendesha. Katika kuruka kwa ndege ipo miujiza ambayo haikufahamika baadhi
yake ila baada ya kuendelea ilimu ya kuruka na nadhariya ya kutembea
katika hewa. Lakini katika yanayo staajabisha ni kupita ndege katika anga na
mbawa zote mbili zimetulia mpaka apite upeo wa macho. Na ilimu imevumbua kuwa
ndege wanao kunjua mbawa zao hupanda juu ya mikondo ya hewa inayo saidia inayo
timbuka ama kwa kupigana dafrau na kiziwizi fulani au kwa kunyanyuka nguzo za
hewa imoto. Ukiwa upepo ni mzuri hizo nguzo za hewa husimama wima na ndege hupaa
kwa namna ya mzunguko kama skurubu. Na ukiwa mkali hizo nguzo hugeuka
kuelekea juu na ndege huruka bila ya kupiga mbawa kwa njia ya sawa moja kwa moja
na kufikia mbali.
Na ndege kwa jumla wana sifa maalumu, katika hizo ni kuwa
ni wepesi, na wana umbo la nguvu, na nyoyo zao ni madhubuti, na kadhaalika
mzunguko wao wa damu, na vyombo vya kuvutia pumzi, na namna lilivyo pimika umbo
lao, na vikawa sawa sawa viwiliwili vyao kwa kusahilisha kuruka katika hewa. Na
sifa hizi Mwenyezi Mungu Mjuzi Mwenye kuona kawajaalia ndege , kwa ajili ya
kuwahifadhi hao ndege katika hewa pale wanapo kunjua mbawa zao au wanapo
zikunja.
Ama videge vidogo vinavyo tegemea kuruka kwao juu ya mbio, hivyo
hupiga mbawa zao kwa chini na mbele ili vipate kujisukuma na kupaa. Na hayo ni
dharura kwa sababu ya kuruka kwao. Kisha huzikunja mbawa zao, lakini nao
wanabaki kuwa wanaruka kwa zile nguvu za msukumo wao.
Na hivyo linawafikiana
umbo lao hao ndege wa kila namna na muundo wa kifundi wa miili yao kwa kuwazesha
kuruka na kujilinda sawa wakati wa kuruka.
20. Bali ni nani huyo mwenye nguvu kwenu atakaye kulindeni na
adhabu asiye kuwa Mwenyewe Arrahman, Mwingi wa Rehema? Makafiri hawamo ila
katika udanganyifu tu kwa hayo wanayo yadhania.
21. Bali ni nani huyo atakaye kuruzukuni kwa yanayo kupeni
uhai wenu na starehe zenu, ikiwa Mwenyezi Mungu akizuia riziki zake asikupeni?
Bali makafiri wamekakamia katika kutakabari kwao na kuikimbia Haki.
22. Je! Hali itageuka? Mwenye kwenda akijikwaa na kusinukia
juu ya uso wake ni mwongofu zaidi katika mwendo wake, au yule anaye tembea
sawasawa kwenye njia isiyo kwenda upogo?
23. Sema: Huyo aliye kuumbeni nanyi hamjakuwa chochote, na
akakupeni usikizi na kuona, na fahamu ambazo ni sababu za vitendo vyenu na
uwongofu wenu - ama ni kuchache mno kushukuru kwenu kwa neema hizi kumshukuru
huyo aliye kupeni.
24. Sema: Huyo ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake
Yeye peke yake ndio mtarejea kwa ajili ya kukuhisabuni na kukulipeni.
25. Na wanasema wanao kanya kufufuliwa: Yatatokea lini haya ya
kukusanywa watu? Twambieni yatakuwa lini, kama nyinyi mnasema kweli!
26. Ewe Muhammad! Sema: Ujuzi wa hayo ni wa Mwenyezi Mungu
peke yake. Ama mimi ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji tu.
27. Watakapo yaona hayo yaliyo ahidiwa yapo karibu nao, nyuso
za makafiri zitajaa huzuni na unyonge, na wataambiwa kwa kuwakejeli na kuwatia
uchungu: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyataka yaje kwa haraka!
28. Sema: Nambieni, ikiwa Mwenyezi Mungu akinifisha mimi na
Waumini walio pamoja nami, kama mnavyo tamani yawe, au akaturehemu akaakhirisha
ajali yetu, na akatusamehe asituadhibu, maana itakuwa katuokoa katika hali zote
mbili, basi nani atakaye wakinga makafiri na adhabu chungu wanayo istahiki
kuipata kwa sababu ya ukafiri wao, na kudanganyika kwao na miungu yao?
29. Yeye huyo ndiye Arrahman, Mwingi wa Rehema, tunaye msadiki
sisi, na nyinyi hamumsadiki. Yeye tu peke yake ndiye tunaye mtegemea, na nyinyi
mnawategemea wenginewe. Mtakuja jua itakapo teremka adhabu ni kundi gani kati
yetu lilio tengeka mbali na Haki.
30. Sema: Hebu nipeni khabari, maji yenu yakitoweka chini ya ardhi msiweze kuyapata kwa namna yoyote, ni nani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni maji ya dhaahiri yanayo miminika anayo weza kuyapata kila atakaye?