1. Ewe Nabii! Mkitaka kuwapa talaka wanawake, basi wapeni talaka kwa kukabiliana na eda zao, (yaani wakati wa tahara kabla ya kuwaingilia), na idhibitini eda, na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe watalaka katika nyumba zao walimo pewa talaka. Wasitoke humo ila ikiwa wamefanya kitendo kichafu wazi. Hukumu hizo zilizo tangulia ni alama za Mwenyezi Mungu amezifanya ni sharia kwa waja wake. Na Mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui pengine Mwenyezi Mungu labda ataleta jambo usilo litaraji baada ya talaka hiyo, na wakapendana.

 

2. Wakikaribia walio achwa mwisho wa eda zao warejeeni mkae nao kwa wema na ihsani, au farikianeni nao bila ya madhara. Na washuhudisheni kuwarejea na kufarikiana watu wawili waadilifu miongoni mwenu, na toeni ushahidi kwa mujibu wake kwa kumsafia Mwenyezi Mungu. Hayo mliyo amrishwa ndiyo anayo waidhiwa mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kumkhofu Mwenyezi Mungu akazishika amri zake na akaepuka makatazo yake atamjaalia njia ya kutokana na kila dhiki.

 

3. Na atamtengezea sababu za kupata riziki kwa jiha ambazo hata hazimpitikii katika fikra zake. Na mwenye kumwachia mambo yake yote Mwenyezi Mungu basi Yeye ni Mwenye kumtosha, hana haja ya mwengine. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimiza alitakalo, ni Mwenye kutekeleza  alipendalo. Amejaalia kila kitu na wakati wake, wala haupitikii, na kipimo hakivuki.

 

4. Na wenye eda ya talaka miongoni mwa wanawake walio sita kuingia myezini kwa utu uzima, kama hawajui wahisabu vipi eda yao, basi eda yao ni miezi mitatu. Na wale ambao hawaingii hedhi kabisa ni kadhaalika.  Na wenye mimba, eda yao inakwisha wanapo jifungua. Na mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, na akazitimiza hukumu zake Mwenyezi Mungu atamsahilishia mambo yake.

 

5. Sharia hizo ni amri ya Mwenyezi Mungu, si ya mwenginewe. Amekuteremshieni Yeye. Na mwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwa kuzihifadhi hukumu zake humfutia makosa yake, na akayafanya makubwa malipo yake.

 

6. Wawekeni wanawake waliomo edani humo humo katika nyumba zenu, kwa kadiri ya uwezo wenu. Wala msiwaletee madhara yoyote, kuwaletea dhiki katika maskani. Na ikiwa wana mimba basi watoleeni gharama za kuwakimu mpaka wazae. Wakikunyonyesheeni watoto wenu hao watalaka, basi wapeni ujira wao. Na amrishaneni mambo mazuri ya kusameheana na kuacha kutaabishana. Na ikitokea kati yenu dhiki na taabu, basi baba atafute mnyonyeshaji mwengine badala ya mama aliye achwa.

 

7. Atoe mwenye nafasi nzuri ya riziki kwa mujibu alicho kunjuliwa na Mwenyezi Mungu, na mwenye dhiki ya pato atoe kwa kadiri alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa mujibu alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.

 

8,9. Na miji mingi ambayo watu wake wamefanya ujabari na wakapuuza amri ya Mola wao Mlezi na Mitume wake, tukaihisabia kwa hisabu kali kwa kuchungua kila walilo litenda na kujadiliana nao, na tukawaadhibu  adhabu ya kuchusha iliyo mbaya, wakagugumia malipo maovu ya mambo yao. Na ukawa mwisho wa mambo yao ni kukhasiri kukubwa mno.

 

10,11.  Mwenyezi Mungu amewaandalia watu wa miji ya watu walio fanya ujabari adhabu ya mwisho wa ukali. Basi tahadharini na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili sawa, ambao mnasifika kwa Imani. Amekuteremshieni mtu mwenye utukufu na cheo, Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zenye kukubainishieni baina yaliyo kweli na ya uwongo, ili awatoe walio amini na wakatenda mema kutoka kwenye giza la upotovu kwenda kwenye mwangaza wa hidaya. Na mwenye kumsadiki Mwenyezi Mungu, na akatenda vitendo vyema atamtia katika Bustani zinazo pita kati yake mito. Watakaa humo milele. Mwenyezi Mungu kamfanyia ihsani Muumini mwema kwa kumpa riziki iliyo njema.

 

12. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye umba mbingu saba, na ardhi mfano wa hizo. Amri yake inapita kote, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni mtimilivu wa uweza, na kwamba Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.