1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa
Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa laiki na utukufu wake. Yeye ndiye peke yake
Mwenye ufalme ulio timia, na Mwenye sifa njema, na ndiye Mwenye uweza ulio timia
juu ya kila kitu.
2. Yeye peke yake ndiye aliye kuumbeni mlipo kuwa si chochote.
Basi kati yenu yupo anaye kanya Ungu wake, na miongoni mwenu yupo anaye sadiki.
Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda, na atakulipeni kwa mujibu wa vitendo
vyenu.
3. Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa hikima isiyo na
ukomo, na akakuumbeni kwa sura, na akazifanya nzuri sura zenu, kwa kuwa
amewafanya wanaadamu ndio viumbe walio nyooka vizuri. Na kwake Yeye ndiyo
marejeo Siku ya Kiyama.
4. Yeye Mwenyezi Mungu anajua yote yaliomo katika mbingu na
ardhi, na anayajua mnayo yaficha, na mnayo yaeneza, ikiwa maneno au vitendo. Na
Mwenyezi Mungu ametimia ujuzi wake kwa mnayo dhamiria katika nyoyo zenu.
5. Zimekwisha wafikieni khabari za walio kufuru kabla yenu, na
wao wakameza ubaya wa matokeo wa mambo yao katika dunia. Na Akhera watapata
adhabu yenye machungu makali.
6. Masaibu hayo yaliyo wapata ni kwa sababu Mitume wao
waliwajia na miujiza iliyo dhaahiri, nao wakasema kwa kukanya: Ati atujie mtu
kama sisi kutuongoza? Wakakanya kuwa watafufuliwa. Wakaiacha Haki. Mwenyezi
Mungu akadhihirisha kuwa hana haja na imani yao kwa kuwaangamiza. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kutimia ukwasi wake (kujitosha kwake), si Mwenye kuwa na haja na
viumbe vyake. Ni Mwenye kustahiki kusifiwa na kuhimidiwa kwa uzuri wa neema
zake.
7. Makafiri wamedai kwa uwongo kwamba hawatafufuliwa baada ya
kufa kwao. Ewe Muhammad! Waambie: Mambo sio kama mnavyo dai nyinyi. Ninaapa kwa
Mola wangu Mlezi! Hapana shaka yoyote nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa kwenu, na
hapana shaka yoyote kuwa mtaambiwa mliyo yatenda duniani. Kisha mtalipwa kwayo.
Na huko kufufuliwa, na kuhisabiwa, na kulipwa, ni jambo sahali na jepesi kabisa
kwa Mwenyezi Mungu.
8. Basi msadikini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ongokeni kwa
kuifuata Nuru tuliyo mteremshia hata akakufahamisheni kwa uwazi kuwa kufufuliwa
kunakuja bila ya shaka yoyote. Na Mwenyezi Mungu ana ujuzi wa kutumia kwa yote
yanayo tokana nanyi.
9. Siku atapo kukusanyeni katika Siku ya Mkusanyo wa walio
tangulia mwanzo na walio kuja mwisho, akulipeni kwa vitendo vyenu! Siku hiyo
ndiyo Siku ya Taghaabun, Kupunjana, kutapo dhihiri kupunjika kwa makafiri
kwa kuacha Imani, na kupunjika Waumini kwa kupuuza kuongeza ut'iifu. Na mwenye
kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema atamwondolea maovu yake, na atamtia
katika Bustani zenye kupita kati yake mito, wakae humo milele. Malipo hayo ndio
kufuzu kukubwa.
10. Na walio ikataa Imani, na wakaikanusha miujiza yetu tuliyo
wapa Mitume wetu kuwaunga mkono, hao ndio watu wa Motoni. Watadumu humo. Na
marudio maovu ni hayo walio yarudia hao.
11. Mja hasibiwi na balaa ila kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Na
mwenye kumsadiki Mwenyezi Mungu basi humwongoa moyo wake kwendea katika yanayo
mpendeza. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ujuzi wake.
12. Na mt'iini Mwenyezi Mungu kwa aliyo kuamrisheni, na
mt'iini Mtume kwa Ujumbe aliyo kufikishieni kutoka kwa Mola wake Mlezi.
Mkiupuuza ut'iifu huu, basi Yeye hadhuriki kitu kwa mapuuza yenu. Na hakika
Mtume wetu hana jukumu juu yake ila kufikisha Utume wake tu kwa uwazi.
13. Mwenyezi Mungu, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa
Yeye tu peke yake. Basi Waumini nawamtegemee Yeye tu katika mambo yao yote.
14. Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto
wenu wamo maadui zenu, ambao wanakuzuilieni msimt'ii Mwenyezi Mungu kwa kutaka
kuwatimizia hao matakwa yao. Basi kuweni na hadhari nao. Na mkiweza
kuyavuka makosa yao yanayo kubalika kusameheka, na mkayapuuza, na mkawafichia,
basi Mwenyezi Mungu naye atakughufirieni nyinyi. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni
Mkunjufu wa maghfira na rehema.
15. Hakika mali yenu na watoto wenu ni majaribio na mtihani.
Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa kwa anaye pendelea kumt'ii Mwenyezi
Mungu.
16. Basi tumieni juhudi zenu na nguvu zenu katika kumcha
Mwenyezi Mungu. Na sikieni mawaidha yake, na t'iini amri zake, na toeni katika
alicho kuruzukuni kwa ajili ya hicho alicho amrisha kitolewe kwa ajili yake. Na
tendeni kheri kwa sababu ya nafsi zenu. Na mwenye kuzuiliwa na Mwenyezi Mungu
ubakhili na uchoyo wa roho yake, basi watu kama hao ndio walio jaaliwa kupata
kila kheri.
17. Mkitoa katika mambo ya kheri kutoa kwa moyo safi, basi
Mwenyezi Mungu atazidisha mardufu thawabu za mlicho toa, na atakusameheni
madhambi yenu yaliyo kuponyokeni. Na Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa shukrani, na
kuwalipa watendao mema, na ni Mpole, hafanyi haraka kuwaadhibu wanao muasi.
18. Yeye ni Mjuzi wa vilivyo fichikana na vinavyo onekana, Mwenye nguvu, Mtenda nguvu, Mwenye hikima katika mipango ya viumbe vyake, Mwenye kuweka kila kitu kwa pahala pake.