1. Ewe Muhammad! Wanapo kujia wanaafiki, wanasema kwa ndimi
zao: Tunashuhudia kuwa hakika wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
anajua kwamba wewe ni Mtume wake; na Mwenyezi Mungu anashuhudia kwamba wanaafiki
hapana shaka ni waongo katika kujidai kwao wanaamini, kwani hawasadiki katika
nyoyo zao.
2. Wamezifanya yamini zao za uwongo ni kinga, au ngao za
kujikingia ili wasichukuliwe kuwa ni makafiri. Basi wakajizuia wenyewe
wasiishike Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka. Hakika ni mabaya mno hayo wanayo
yatenda ya unaafiki na kujitia imani ya uwongo.
3. Hayo waliyo yafanya ndiyo mazoea ya kudhihirisha yasiyo ya
kweli, na kuapa yamini za uwongo, kwa sababu hao wameamini kwa ndimi zao, kisha
wakakufuru katika nyoyo zao, basi nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa ukafiri huu.
Hao hawafahamu yepi ya kuwaokoa na adhabu za Mwenyezi Mungu.
4. Na ukiwaona miili yao inakupendeza kwa uzuri wao, na
wakizungumza unavutika kuwasikiliza kwa utamu wa maneno yao. Kumbe wao juu ya
yote hayo nyoyo zao zitupu, hazina Imani ndani yake. Kama magogo yaliyo
egemezwa, hayana uhai wowote. Wao hudhania kila linalo zuka basi linawalenga
wao, kwa sababu wanaitambua hali yao ya unaafiki. Hao ndio maadui, basi
tahadhari nao. Mwenyezi Mungu kesha wafukuza kwenye rehema yake. Vipi wanavyo
iacha Haki wakauendea unaafiki wanao ushikilia?
5. Na wakiambiwa: Jongeeni, apate Mtume wa Mwenyezi Mungu
kukuombeeni msamaha, hutikisa vichwa vyao kwa kejeli, na utawaona wanageuka kwa
kiburi hawataki kut'ii.
6. Ni sawa kwa hawa wanaafiki, ukiwaombea msamaha, au ukito
waombea. Kwa sababu hao hawauachi unaafiki wao. Basi Mwenyezi Mungu hatawasamehe
kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi kuwapeleka kwenye Haki wale wanao kataa
kufuata amri yake na kumuamini.
7. Hao wanaafiki ndio wanao waambia watu wa Madina: Msitoe
chochote kuwapa hao Waumini walio na Mtume wa Mwenyezi Mungu ili wapate
kumwacha! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina zote za mbinguni na duniani, na
riziki zote ziliomo humo. Lakini wanaafiki hawajui hayo.
8. Wanaafiki wanasema kwa kutoa ahadi: Tukirejea Madina hapana
shaka kikundi chetu, ambacho ndicho chenye nguvu zaidi, kitakitoa kikundi cha
Waumini ambao ni wanyonge! Nguvu anazo Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na
Waumini; sio hawa wanao jitia kuahidi. Lakini wanaafiki hawajui kitu.
9. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake!
Yasikuhangaisheni mali yenu, na watoto wenu, hata mkaacha kumkumbuka Mwenyezi
Mungu na kutekekeleza aliyo kuamrisheni kuyafanya. Na wenye kushughulishwa na
mali zao na watoto wao wakaacha hayo, basi hao ndio watao kuwa wamekhasiri Siku
ya Kiyama.
10. Enyi Waumini! Toeni katika mali tuliyo kuruzukuni upesi
upesi kabla mmoja wenu hayajamfikia mauti akasema kwa majuto: Ewe Mola wangu
Mlezi! Hebu hunipi muhula kidogo, nikapata kutoa sadaka, na nikawa
miongoni wa watu wema watendao vitendo vyema?
11. Wala Mwenyezi Mungu hampi muhula mtu yeyote ukisha fika wakati wake wa kufa. Na Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa kujua yote myatendayo, na Yeye atakulipeni kwa hayo.