1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi
vinamsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa laiki, Yeye
ndiye Mfalme wa kila kitu, Mwenye kuendesha atakavyo bila ya mpinzani, Mwenye
kutakasika kwa ukamilifu na kila cha upungufu, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye
hikima ya kufika mwisho.
2. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mtuma Mtume kwa watu wasio jua
kuandika, naye ni katika wao wenyewe, anawasomea Aya zake Mwenyezi Mungu, na
anawasafisha na mambo machafu ya itikadi na tabia, na anawafundisha Qur'ani na
kuijua Dini. Na wao kabla ya kuletwa yeye walikuwa wamepotoka kabisa kuiacha
haki.
3. Na pia Mwenyezi Mungu amempeleka Muhammad kwa watu
wenginewe, ambao hawajaja bado, lakini watakuja. Na Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima ya kufikia ukomo katika vitendo
vyake.
4. Kuletwa Mtume huko ni fadhila inayo toka kwa Mwenyezi Mungu.
Anamkirimu kwayo aliye mkhitari katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu peke yake,
ndiye Mwenye fadhila kubwa.
5. Mfano wa Mayahudi walio funzwa Taurati, na wakalazimishwa
waifuate, na wao hawakuifuata kwa vitendo, ni mfano wa punda aliye beba vitabu
ambavyo hajui ndani yake mna nini. Ni mbaya mno mfano wa watu wanao kadhibisha
Ishara za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hawasaidii kufikilia uwongofu watu
ambao kazi yao ni kudhulumu.
6. Ewe Muhammad! Sema: Enyi nyinyi mlio Mayahudi! Kama mnadai
kwa uwongo kwamba nyinyi peke yenu ati ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, basi
takeni mauti kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika hayo madai ya
kwamba Mwenyezi Mungu anakupendeni.
7. Mwenyezi Mungu anasema: Wala Mayahudi hawatamani mauti
milele kwa sababu ya ukafiri na vitendo viovu walio kwisha vitenda. Na Mwenyezi
Mungu anawajua vyema walio dhulumu.
8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia hamwezi kuyakimbia, bila ya
shaka yatakukuteni tu. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kujua ya siri na ya
dhaahiri. Na Yeye atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, basi
nendeni kwa hima na hamu kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu, na wacheni
biashara. Hayo mliyo amrishwa yana nafuu zaidi kwenu nyinyi, ikiwa mnajua.
10. Mkisha maliza kusali basi tawanyikeni katika nchi kwa
ajili ya maslaha yenu, na mtake fadhila za Mwenyezi Mungu. Na mkumbukeni
Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenu na ndimi zenu kwa wingi, ili asaa mkafuzu katika
kheri za duniani na Akhera.
11. Na wakiona bidhaa za biashara, au pumbao lolote hutawanyika kuendea hayo, na wakakuacha wewe umesimama unakhutubu! Waambie: Fadhila na thawabu zilioko kwa Mwenyezi Mungu zina nafuu zaidi kwenu kuliko pumbao na kuliko biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao toa riziki. Basi itafuteni riziki yake kwa kumt'ii Yeye.