1. Kila kiliomo katika mbingu na kiliomo katika ardhi kinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa ni laiki yake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye kuvishinda vitu vyote, Mwenye hikima iliyo fika ukomo.

 

2. Enyi mlio amini! Kwa ajili ya nini mnasema kwa ndimi zenu yasiyo hakikishwa na vitendo vyenu?

 

3. Mwenyezi Mungu anachukia mno kuwa nyinyi mnasema msiyo yatenda.

 

4. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigania kutaka kulinyanyua Neno lake nao wameshikamana kitu kimoja, kama kwamba wao ni jengo lilio simama imara.

 

5. Ewe Muhammad! Kumbuka pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi mimi, na hali nyinyi mnajua kwamba hakika mimi ni Mjumbe niliye tumwa na Mwenyezi Mungu nije kwenu? Walipo endelea na kuiacha Haki, Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo zao zisipokee uwongofu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio toka kwenye ut'iifu wake.

 

6. Na kumbuka pale Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume nimetumwa kwenu, mwenye kusadikisha yaliyo nitangulia yaliomo katika Taurati, na kukupeni bishara ya Mtume atakaye kuja baada yangu. Jina lake ni Ahmad. Alipo kuja huyo Mtume aliye bashiriwa kwa Ishara zilizo wazi wakasema: Haya uliyo tujia nayo ni uchawi dhaahiri!
(Kwa ushahidi wa kubashiriwa Nabii Muhammad s.a.w. katika vitabu vya Kikristo na Kiyahudi, tazama: Kumbukumbu la Torati 18.19-22, na Injili ya Yohana 16.5-14.)

 

7. Na nani aliye zidi kwa udhaalimu kuliko huyo aliye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, naye anaitwa aingie katika Dini ya Kiislamu, Dini ya haki na kheri? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio shikilia dhulma.

 

8. Wana wa Israili wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo, ili ati wapate kuizima nuru ya Dini yake kwa vinywa vyao, kama anaye taka kuizima nuru ya jua kwa kuipulizia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuikamilisha nuru yake kwa kuitimiza Dini yake hata hao makafiri wakiudhika.

 

9. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mtuma Mtume wake, Muhammad, pamoja na Qur'ani ambayo ni uwongofu kwa watu wote, na Uislamu ambao ndio Dini ya haki, ili autukuze juu ya dini zote, ijapo kuwa washirikina wataudhika.

 

10. Enyi mlio amini! Nikuongozeni kwenye biashara kubwa ambayo itakuokoeni na adhabu yenye machungu makali?

 

11. Biashara hii ni kuwa mumuamini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na mpigane Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu. Hayo aliyo kuonyesheni ndiyo kheri yenu ikiwa nyinyi mnajua.

 

12. Muamini na mpigane Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, ili akusameheni madhambi yenu, na akutieni katika Bustani zinazo pita kati yake mito, na maskani nzuri katika Bustani za milele. Hayo ndiyo malipo makubwa.

 

13. Na neema nyengine ambazo Waumini Mujahidina wanazo zipenda, ni msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu na ushindi wa karibu utakao kuleteeni kheri zake. Na ewe Muhammad! Wabashirie Waumini kuwa watapata malipo haya.

 

14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu anapo kutakeni Mtume wa Mwenyezi Mungu muwe wasaidizi wake. Kama walivyo kuwa masahaba wa Isa wasaidizi wa Mwenyezi Mungu alipo sema: Nani wa kunisaidia mimi kwa Mwenyezi Mungu? Basi kundi moja katika Wana wa Israili lilimuamini Isa, na kundi jengine likamkataa. Sisi tukawapa nguvu  walio amini juu ya maadui zao walio kufuru. Basi kwa kuwapa nguvu kwetu wakawa ni wenye kushinda.