1. Enyi mlio
msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Msiwafanye maadui wangu na maadui wenu
kuwa ni wenzenu mkiwapa mapenzi ya kweli, na hali wao wameyakataa yaliyo kujieni
nyinyi ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu chake. Wamemtoa Mtume
na wamekutoeni nyinyi kwenu kwenye majumba yenu, kwa sababu ya Imani yenu
kumuamini Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Mnapotoka makwenu kwenda pigana
Jihadi katika Njia yangu na kutaka radhi yangu, basi msifanye urafiki na adui
zangu, mkawapa mapenzi kisirisiri. Na Mimi nayajua vyema yote mnayo yaficha na
mnayo dhihirisha. Na yeyote mwenye kumfanya adui wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiye
rafiki yake basi ameikosea Njia Iliyo Nyooka.
2. Wakikutana
nanyi na wakakuwezeni, uadui wao kwenu unadhihiri, na wanakunyoosheeni mikono
yao na ndimi zao kukudhuruni. Na wanatamani muwe makafiri kama wao.
3.
Hawatakufaeni kitu jamaa zenu wala watoto wenu mlio wafanya kuwa ni marafiki, na
hali wao ni adui wa Mwenyezi Mungu na adui zenu. Katika Siku ya Kiyama Mwenyezi
Mungu atakutengeni mbali mbali. Atawatia maadui zake Motoni na marafiki zake
Peponi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote myatendayo.
4. Nyinyi mna
kiigizo kizuri cha kukiiga katika Ibrahim na walio amini pamoja naye, pale
walipo waambia watu wao: Hakika sisi tunajitenga nanyi, na tunajitenga na hiyo
miungu ya uwongo mnayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Sisi tunakukataeni, na
umekwisha dhihiri uadui na kuchukiana baina yetu na nyinyi. Hayo hayataondoka
kabisa mpaka mumuamini Mwenyezi Mungu peke yake. Lakini kauli ya Ibrahim
kumwambia baba yake: Nitakutakia maghfira, na similiki kwa Mwenyezi Mungu kitu
chochote - kauli hiyo si ya kufuatwa. Kwani hayo yalikuwa kabla hajajua huyo
baba yake kashikilia kuwa adui wa Mwenyezi Mungu wala hageuki. Ilipo dhihiri
kwake kuwa hakika huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu alijitenga naye. Enyi waumini!
Semeni: Mola wetu Mlezi! Kwako Wewe ndio tunategemea, na kwako Wewe tunarejea,
na kwako Wewe ndio mwisho wetu Akhera.
5. Mola wetu
Mlezi! Usitujaalie tukawa katika hali ya kuwa katika fitina za walio kufuru. Na
tusamehe madhambi yetu, ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu
usiye shindika, Mwenye hikima katika kutasarafu kwake.
6. Enyi
Waumini! Bila ya shaka katika Ibrahim na walio kuwa pamoja naye, kipo kiigizo
kizuri kwenu kwa vile walivyo wafanyia uadui maadui wa Mwenyezi Mungu. Kiigizo
hicho ni kwa mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na
mwenye kupuuza kufuata haya basi kajidhulumu nafsi yake. Kwani hakika Mwenyezi
Mungu si mhitaji wa mwenginewe. Yeye ni Mwenye kustahiki peke yake sifa zote
njema.
7. Asaa
Mwenyezi Mungu akajaalia yawepo mapenzi baina yenu na hao makafiri walio ni
maadui zenu, kwa kuwapa tawfiki, kuwawezesha, kuingia katika Imani. Na Mwenyezi
Mungu ana uweza ulio timia, ni Mkunjufu wa maghfira kwa mwenye kutubu, ni Mwenye
kuwarehemu waja wake.
8. Mwenyezi
Mungu hakukatazini kwa makafiri wasio kupigeni vita wala kukufukuzeni makwenu
kuwakirimu na kuwapa mawasiliano mema. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda watu
watendao ihsani na mawasiliano.
9. Ila Mwenyezi
Mungu anakukatazeni wale walio kupigeni vita katika Dini ili kukuzuieni nayo, na
wakakulazimisheni kutoka majumbani kwenu na nchi yenu, na wakasaidia katika
kukutoeni huko, msiwafanye hao kuwa ndio wenzenu wa kusaidiana nao. Na wenye
kuwafanya hao ndio wasaidizi wao, basi hao ndio wenye kujidhulumu nafsi zao.
10. Enyi mlio
amini! Wakikujieni wanawake Waumini walio hama kukimbia nchi ya ukafiri, basi
wachungueni ili mpate kujua ukweli wa Imani yao. Mwenyezi Mungu anajua zaidi
ukweli wa Imani yao. Mkiwaona kama ni Waumini, basi msiwarudishe kwa waume zao
makafiri. Wanawake Waumini si halali kwa makafiri, wala wanaume makafiri si
halali kwa wanawake Waumini. Na wapeni waume wa kikafiri mahari waliyo yatoa kwa
wake zao walio hamia kwenu. Wala hapana ubaya kwenu kuwaoa wanawake hao walio
hamia kwenu mkiwapa mahari yao. Wala msiwazuie kwa kifungo cha ndoa wanawake
makafiri walio bakia katika mji wa ukafiri au walio fungamana nao. Na takeni kwa
makafiri mahari mliyo yatoa kwa wenye kufungamana na mji wa ukafiri. Na wao hao
watake kulipwa walicho toa kuwapa wake zao walio hama wakaja kwenu. Hukumu hiyo
ni kwa mujibu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, anayo kufafanulieni. Na Mwenyezi
Mungu anajua vyema maslaha ya waja wake, ni Mwenye hikima katika kutoa sharia.
11. Na
wakitokea baadhi ya wake zenu wakakukimbieni kwenda kwa makafiri, kisha
mkapigana nao vita, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha mahari
waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
12. Ewe Nabii!
Wakikujia wanawake Waumini kukuahidi kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na
chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatwauwa watoto wao, wala
hawatawabandikiza waume zao watoto wao (wa haramu) kwa uzushi na uwongo wanao
uzua baina ya mikono yao na miguu yao. (yaani matumboni mwao, au kwa ndimi zao
na tupu zao); wala hawendi kinyume nawe katika jambo jema unalo waitia, basi
pokea ahadi zao juu ya hayo, na waombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na kurehemu. (Mtume s.a.w. haamrishi ila
jema, lakini sharia hapo inasema kuwa mtawala yeyote hut'iiwa akiamrisha jema
tu. Ama kwa lilio ovu, Mtume s.a.w. amesema: "Hapana kumtii kiumbe katika
kumuasi Muumba.")
13. Enyi mlio
msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake, msiwafanye kuwa rafiki zenu watu ambao
Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia. Hao wamekata tamaa na Akhera na yote yatakao
kuwapo huko, ya kulipwa na kuhisabiwa, kama makafiri walivyo kata tamaa
kufufuliwa waliomo makaburini.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani