* 1. Vitu vyote
viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio
laiki naye. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi na kitu. Mwenye
hikima katika mipango yake na vitendo vyake.
2. Yeye
Mwenyezi Mungu ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu, nao
ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nnadhir, kutoka kwenye majumba yao wakati wa kuwatoa
mara ya kwanza katika Bara Arabu. Enyi Waislamu! Hamkudhania kuwa watatoka
kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na wao wenyewe walidhani kwamba ngome
zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea
katika upande wasio utarajia, na akawatia katika nyoyo zao fazaa kubwa, wakawa
wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya
Waumini wapate kuzivunja zile ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika
haya yaliyo washukia hawa.
3. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu hakuwahukumia kuwatoa majumbani kwao kwa sura hii ya kuchusha,
basi hapana shaka angeli waadhibu katika dunia kwa shida zaidi kuliko huko
kuwatoa. Na Akhera, wao watapata adhabu ya Moto, mbali huku kutolewa majumbani
kwao duniani.
4. Hayo yaliyo
wapata duniani na yanayo wangojea Akhera ni kwa sabau ya kuwa wamemfanyia uadui
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, uadui mkubwa mno. Na mwenye kumfanyia uadui
Mwenyezi Mungu basi hawezi kupenya kuikimbia adhabu yake. Na hakika Mwenyezi
Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
5. Enyi
Waislamu! Mitende yoyote mliyo ikata au mkaiacha imebaki kama ilivyo kuwa, basi
ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hapana lawama juu yenu katika hayo, ili awape
nguvu Waumini, na awahizi wapotovu walio ziacha sharia zake.
6. Na aliyo
yaleta Mwenyezi Mungu na akayarudisha kwa Mtume wake katika mali ya Banu Nnadhir
hamkuyapigia mbio nyinyi kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa
madaraka Mitume wake kwa awatakao katika waja wake bila ya kupigana vita. Na
Mwenyezi Mungu ni Mtimilivu wa uweza juu ya kila kitu.
7. Alicho
rudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake katika mali ya watu wa vijiji hivi bila ya
kuwatimua farasi au ngamia, vitu hivyo ni vya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri. Haya ni hivyo ili yasiwe mali
yakizunguka katika mikono ya matajiri peke yao katika nyinyi. Na anacho kupeni
Mtume katika hukumu basi kishikeni, na anacho kukatazeni basi kiwacheni. Na
jilindeni na kughadhibika kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa
kuadhibu.
8. Na hivyo
yale mali ya watu wa vijiji aliyo yarudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake wapewe
mafakiri katika Wahajiri, walio kimbilia Madina, ambao wametolewa majumbani kwao
na mali yao huko Makka. Wao wanataraji ziada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika
riziki zao na radhi. Na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa nafsi zao
na mali yao. Hao ndio Waumini wa kweli.
9. Na
Ma-ansari, watu wa Madina walio mnusuru Mtume na Wahajiri, ambao wamekaa Madina
katika maskani zao, na Imani yao ikawa safi kabisa kabla ya kufika Wahajiri,
wanawapenda wale wageni Waislamu walio hamia kwao, na wala hawahisi ubaya wowote
katika nafsi zao kwa walicho pewa Wahajiri katika ngawira. Bali wanawakadimisha
Wahajiri kuliko nafsi zao, ijapo kuwa wakiwa wao nao ni wahitaji. Na mwenye
kuhifadhika, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, asione ubakhili katika nafsi yake,
basi watu kama hao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
10. Na Waumini
walio kuja baada ya Wahajiri na Ansari husema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi
zetu, sisi na ndugu zetu walio tutangulia katika Imani. Wala usijaalie kuwa
katika nyoyo zetu husda kuwahusudu walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe
umefika ukomo katika upole na kurehemu.
11. Hebu
huwaangalii hao wanaafiki ukastaajabu? Kazi yao ni kuwakariria kauli ndugu zao
walio kufuru katika Watu wa Kitabu - nao ni hao Banu Nnadhir - kuwaambia:
Wallahi! Mkilazimishwa kuihama Madina, basi hapana shaka na sisi tutatoka pamoja
nanyi. Wala hatutamt'ii katika jambo lenu mtu yeyote daima dawamu. Na pindi
ikiwa Waislamu watakupigeni vita, basi hapana shaka sisi tutakusaidieni. Na
Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hakika wanaafiki hapana shaka ni waongo katika
hizo ahadi zao wanazo zitoa.
12. Wakitolewa
Mayahudi, wanaafiki hawatatoka pamoja nao. Na wakipigwa vita hawatawanusuru. Na
pindi wakiwasaidia basi hapana shaka watatoka mbio warudi kinyume nyume, wala
hawatawanusuru.
13. Hakika,
enyi Waislamu, mna kitisho zaidi katika vifua vya wanaafiki na Mayahudi kuliko
wanavyo mwogopa Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa sababu hakika wao ni watu wasio jua
ukweli wa Imani.
14. Mayahudi
hawapigani vita nanyi kwa pamoja ila wawe katika miji iliyo jengewa ngome, au
wajifiche nyuma ya kuta. Vita vyao baina ya wao kwa wao ni vikali. Utawadhani
kuwa wameshikamana, wote ni wamoja. Kumbe hakika nyoyo zao zimefarikiana mbali
mbali. Wao ni wenye sifa hizo, kwa sababu hao ni watu wasio zingatia nini
utakuwa mwisho wa mambo.
15. Mfano wa
Bani Nnadhir ni kama mfano wa walio kufuru kabla yao karibuni. Hao walionja hapa
hapa duniani matokeo ya ukafiri wao na kuvunja kwao mapatano. Na Akhera watapata
adhabu ya uchungu mkali.
16. Mfano wa
wanaafiki kuwashawishi Banu Nnadhir wamuasi Mtume wa Mwenyezi ni kama mfano wa
Shetani pale anapo mghuri mtu aiache Imani, akamwambia: Kufuru! Na alipo kufuru
akasema: Mimi niko mbali nawe, kwani mimi ninamkhofu Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wa walimwengu wote.
17. Ikawa basi
marejeo ya Shetani na huyo anaye mzaini ni kuishia Motoni wabaki humo milele. Na
kudumu humo dawamu ni malipo ya wenye kuasi wakaikiuka Njia ya Haki.
18. Enyi mlio
amini! Jiwekeeni kinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kumt'ii
Yeye. Na kila nafsi izingatie a'mali gani ya kuikadimisha kwa ajili ya Kesho. Na
jilazimisheni kumcha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari vilivyo
kwa yote myatendayo. Naye atakulipeni kwa hayo.
19. Enyi
Waumini! Msiwe kama wale walio sahau haki za Mwenyezi Mungu, na Yeye
akawasahaulisha nafsi zao, kwa kuwajaribu kwa mitihani, na wakawa hawajui linalo
wafaa na linalo wadhuru. Hao ndio walio toka wakaacha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
20. Hawawi
sawa watu wa Motoni wanao teswa, na watu wa Peponi wanao neemeshwa. Watu wa
Peponi peke yao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
21. Lau
tungeli iteremsha hii Qur'ani juu ya mlima wenye nguvu basi ungeli uona huo
mlima, juu ya nguvu zake, unanyenyekea na unapasuka kwa kumwogopa Mwenyezi
Mungu. Na hiyo ni mifano tunawaelezea watu ili wapate kuzingatia matokeo ya
mambo yao.
22. Yeye
Mwenyezi Mungu ambaye hapana wa kuabudiwa kikweli isipo kuwa Yeye peke yake,
Mwenye kujua lilio pita na lilioko sasa. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye
kurehemu.
23. Yeye
Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye, Mwenye kumiliki kila kitu
kwa hakika, Aliye safika na kila upungufu, Aliye takasika na kila lisio
mwelekea, Mwenye kusalimika na yote ya upungufu, Mwenye kuwaamini na kuwasadiki
Mitume wake aliyo wapa nguvu kwa miujiza, Mlinzi Mwenye kuangalia kila kitu,
Mwenye kushinda basi hashindwi na chochote, Mkubwa wa shani katika nguvu na
utawala, Mwenye kutukuka na kila kisicho kuwa laiki na uzuri wake na utukufu
wake, Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo.
24. Yeye ndiye
Mwenyezi Mungu, Mwenye kuviumba vitu vyote tangu mwanzo bila ya ruwaza ya kuigia
iliyo tangulia, Mwenye kuvipa sura kama vilivyo kwa mujibu wa atakavyo Yeye.
Yeye ndiye Mwenye Majina Mazuri, Mwenye kutakaswa na kila kisicho kuwa laiki
yake na kila kilichoko katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda,
asiye shindwa na kitu. Mwenye hikima katika kupanga kwake na sharia zake.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani