1. Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya huyo mwanamke anaye kurejea wewe kwa shauri ya mumewe aliye jitenga naye kwa kudai ati anamwona kama mgongo wa mama yake, na akamlalamikia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia hayo maneno mnayo jibizana. Hakika Mwenyezi Mungu anayasikia vyema yote ya kusikiwa, anayaona vyema yote ya kuonekana. Imepokelewa kuwa Sahaba mmoja, aitwaye Aus bin Ass'amit, aliudhika na mkewe aitwaye, Khola bint Tha'labah, akamwambia: "Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu." Na katika siku za Ujahiliya ilikuwa ndio mwanamke kesha harimika kwa mumewe. Mwanamke akenda kumpa khabari Nabii s.a.w., na Mtume akamwambia: "Sijaamrishwa kitu katika kesi yako. Na sioni ila ni kuwa kweli umekwisha harimika kwake." Mwanamke akajadiliana na Mtume s.a.w. na akamrejea tena, na akawa anamshitakia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kukhofu kufarikiana na mume na kupotea mwanawe. Haukupita muda ila ikateremka Aya hii na tatu zilizo baada yake.
 

2. Enyi Waumini! Hao miongoni mwenu wanao jitenga na wake zao kwa kuwashabihisha katika kuharimikiana nao kuwa ati ni kama mama zao, ni wakosa. Wake zao sio mama zao. Ukitaka haki mama zao ni wale walio wazaa tu. Na hakika wanao watenga wake zao kwa kusema hivyo wanasema kauli inayo chusha, inayo udhi katika murwa mwema, na ni uwongo ulio tokana na haki. Na hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mkuu wa kusamehe na kughufiria kwa yaliyo kwisha pita kwenu.
 

3. Na wale wanao watenga wake zao na kisha wakarejeza kauli yao, wakayaona makosa yao, na wakataka kubaki na wake zao, basi juu yao kumkomboa mtumwa kabla ya kugusana. Hayo aliyo yawajibisha Mwenyezi Mungu, ya kukomboa mtumwa, ni mawaidha kwenu mnawaidhiwa ili msirejee tena katika makosa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vilivyo myatendayo.
 

4. Na asiye pata mtumwa wa kumkomboa, basi yampasa afunge miezi miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiye weza kufunga hivyo basi itampasa awalishe masikini sitini. Tumeyalazimisha hayo ili mpate kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mtende kwa mujibu wa Imani hiyo. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikiuke. Na makafiri watapata adhabu yenye machungu makali.
 

5. Hakika wanao mfanyia inda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kupingana nao watatupiliwa mbali kama walivyo tupiliwa mbali walio kuwa kabla yao. Na Sisi tumekwisha teremsha dalili zilizo wazi za kuonyesha Haki. Na hao wapinzani watapata adhabu ya kuwafedhehesha mno.
 

6. Siku Mwenyezi Mungu atapo wafufua wote baada ya kwisha kufa kwao, na awape khabari za yale waliyo yatenda. Mwenyezi Mungu amewawekea yote na ameyahifadhi, na wao wameyasahau. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa yote na anayajua yote.
 

7. Kwani hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na yaliomo katika ardhi, na wala hapana siri ya watu watatu ila Yeye Mwenyezi Mungu ndiye wane wao kwa kuyajua kwake wanayo fanyia siri, wala hawawi watano ila na Yeye ndiye wa sita wao. Wala duni kuliko hivyo, wala kuzidi hivyo, ila Yeye yuko pamoja nao, anayajua hayo wanayo yanong'ona, popote walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawapa khabari kwa kila walilo litenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ujuzi wake.
 

8. Ewe Mtume! Huwaoni hao walio katazwa kufanya njama za siri wao kwa wao kwa mambo ya kutia shaka katika nyoyo za Waumini, kisha wakayarejea yale yale waliyo katazwa? Na wanafanya njama kwa madhambi wanayo yatenda, na uadui wanao uazimia, na uasi dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na wanapo kuja kwako wanakuamkia kwa kauli ya kupotoa, sivyo anavyo kuamkia Mwenyezi Mungu. Na wao husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi Mungu hatuadhibu kwa haya tunayo yasema ikiwa huyu ni Mtume kweli? Inawatosha hao Jahannamu. Wataingia humo waungue kwa moto wake. Na marejeo maovu yalioje marejeo yao. Ilikuwako sulhu baina ya Waislamu na Mayahudi katika mji wa Madina. Na ikawa akipita mtu katika Waislamu kwao Mayahudi hunong'ona wao kwa wao ili adhani yule Muislamu kuwa wao wanapanga njama za kutaka kumuuwa, au lolote la kumdhuru apate kugeuza njia asiwapitie tena. Mtume s.a.w. akawakataza hayo, lakini hawakuacha mtindo wao, wakayarejea yale yale waliyo katazwa. Na wakawa akija Mtume s.a.w. wakimwamkia kwa maamkio ya kumuapiza. Ndiyo ikashuka Aya hii.
 

9. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mnapo sema siri, basi msiwe mkisema siri katika mambo ya madhambi, na kufanya uadui, na kwenda kinyume na Mtume. Semeni siri katika mambo ya kheri, na kuepukana na madhambi. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu ambaye kwake Yeye tu, si kwengineko, ndio mtakusanywa baada ya kufufuliwa.
 

10. Hakika kusema siri kwa kuchochea shaka shaka ni katika kuzainishwa na Shetani, ili apate kuingiza huzuni katika nyoyo za Waumini. Wala hayo hayawezi kuwaletea madhara yoyote wao ila kwa kupenda Mwenyezi Mungu. Basi Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu peke yake.
 

11. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mkitakiwa baadhi yenu kuwafanyia nafasi wenzenu mnapo kaa katika majlisi zenu, basi wafanyieni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na mkitakiwa kuondoka pale mlipo kaa basi ondokeni. Mwenyezi Mungu hutukuza vyeo vya Waumini, na wale walio pewa ilimu kwa daraja nyingi. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
 

12. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mkitaka kusema siri na Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi kabla ya mazungumzo yenu hayo tangulizeni kutoa sadaka. Hivyo ndio kheri yenu, na ni usafi zaidi kwa nyoyo zenu. Lakini ikiwa hamkupata cha kutoa sadaka, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa kusamehe, Mwenye kukusanya rehema zote.
 

13. Mnachelea kujilazimisha kutoa sadaka kabla ya mazungumzo yenu na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Na ikiwa hamkutoa, na Mwenyezi Mungu akakusameheni, basi hifadhini kushika Sala na kutoa Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo.
 

14. Ewe Mtume! Huwaoni wanaafiki walio wafanya marafiki watu ambao Mwenyezi Mungu ameghadhibika nao. Hawa wanao fanya urafiki si katika nyinyi, na hao wanao fanywa ni marafiki pia si katika nyinyi. Na wanaapa kwa uwongo, na huku wanajua kuwa wao ni waongo.
 

15. Mwenyezi Mungu amewatengenezea hawa wanaafiki adhabu ya mwisho wa ukali. Hakika vitendo vyao walivyo kuwa wakivitenda, vya unaafiki, na kuchukua viapo vya uwongo, ni viovu mno.
 

16. Wamefanya viapo vyao kuwa ndio viwe ni kinga ya kuwakinga wasiuliwe wenyewe, na watoto wao wasiwe mateka, na mali yao yasiwe ngawira. Kwa hayo wakaizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watapata adhabu ya fedheha.
 

17. Mali yao na watoto wao hayatawalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu hata chembe. Hao ni watu wa Motoni, wa kudumu humo milele.
 

18. Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu wote watamwapia kuwa hakika wao walikuwa ni Waumini, kama wanavyo kuapieni nyinyi hivi sasa. Na wanadhani kuwa kwa kuapa kwao huku ni ujanja utakao wafaa. Ama kweli, hakika hawa wamefika ukomo wa uwongo!
 

19. Shetani amewatawala na amewasahaulisha kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kuukumbuka utukufu wake. Hao ndio kundi la Shetani. Ama kweli, hakika kundi la Shetani ndilo lilio fikilia mwisho wa kukhasiri.
 

20. Hao wanao mfanyia inda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio katika hisabu ya walio fikilia ukomo wa udhalili.
 

21. Mwenyezi Mungu amekata hukumu: Bila ya shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu zilizo timia, hashindwi na yeyote.
 

22. Huwakuti watu wanao msadiki Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho wanapendana na wenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au ni watoto wao, au ni ndugu zao, au ni jamaa zao. Hao ambao hawafanyi urafiki na wanao mpinga Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ameithibitisha Imani katika nyoyo zao, na amewaunga mkono kwa nguvu zinazo tokana naye Yeye Mwenyewe, na atawatia katika Mabustani yapitayo mito kati yake wakikaa humo milele. Neema zake haziwakatikii. Mwenyezi Mungu amewapenda hao, na wao wamempenda. Hao ndio wanao ambiwa kuwa ni katika Hizbullahi, yaani Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika ni kweli Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufuzu.
 

Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani